Habari za Punde

Maalim Seif afungua jengo jipya la chuo cha maendeleo ya utalii

 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akikata utepe kuashiria ufunguzi wa jengo jipya la chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar kilichoko Maruhubi.
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiongozana na Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar Bi. Zuleikha Kombo Khamis pamoja na Waziri wa Habari Mhe. Said Ali Mbarouk, wakati wakitembelea eneo la Chuo hicho baada ya kufungua jengo jipya.
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa jengo jipya la chuo cha maendeleo ya utalii Zanzibar kilichoko Maruhubi mjini Zanzibar.
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar, wakimsubiri Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad kwa ajili ya ufunguzi wa jengo jipya la chuo hicho (Picha na Salmin Said, OMKR)
 
Na Hassan Hamad OMKR
 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema ujenzi wa jengo jipya la chuo cha maendeleo ya utalii Zanzibar utasaidia kuimarisha sekta ya utalii nchini.
 
Amesema ujenzi huo unakwenda sambamba na kuinua hadhi ya chuo hicho kitaaluma, pamoja na kutekeleza malengo ya Mapinduzi ambayo ni pamoja na kuleta maendeleo kwa wananchi.
 
Mhe. Maalim Seif ameeleza hayo katika hafla ya ufunguzi wa jengo jipya la chuo hicho ikiwa ni shamrashamra za maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
 
Amefahamisha kuwa lengo la Serikali ni kukifanya chuo hicho kuwa kituo bora cha utoaji wa taaluma ili kuimarisha sekta ya utalii ambayo ndio sekta kiongozi kwa uchumi wa Zanzibar.
Amewataka wanafunzi wa Chuo hicho kujiendeleza kitaaluma, ili waweze kushika nafasi za ajira ambazo kwa sasa baadhi yake zinachukuliwa na wageni.
 
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Said Ali Mbarouk amesema katika kukijengea hadhi chuo hicho, wanakusudia kujenga jengo la ghorofa nne ambapo ujenzi wake unatarajiwa kuanza mwaka ujao.
 
Nae Mkuu wa Chuo hicho Bi. Zuleikha Kombo Khamis amesema ujenzi wa jengo hilo la kisasa umeondoa usumbufu waliokuwa wakiupata kwa kipindi kirefu.
 
Amesema kabla ya ujenzi huo walikuwa wakikabiliwa na tatizo la upungufu wa madarasa ya kusomea pamoja na maktaba, mambo ambayo sasa yamepatiwa ufumbuzi.
 
Ujenzi huo wa vyumba 23 vikiwemo vyoo vinne vya watu wenye ulemavu, umegharimu shilingi milioni mia nane (800 mil.)
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.