Habari za Punde

Waziri Ferej azindua kamati ya kitaalamu ya kitaifa ya kuratibu na udhibiti wa madawa ya kulevya


Na Ramadhan Ali-Maelezo  ZANZIBAR
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Fatma Abdulhabib Ferej amesema  juhudi za Serikali  ya  kuwasogezea wananchi  maendeleo  hazitokuwa na tija iwapo wimbi la vijana  wa Zanzibar watatumika  kusafirisha dawa za kulevya na wataendelea kuwa wahanga wa matumizi ya dawa hizo.
Amesema hatma ya maendeleo ya Taifa itategemea zaidi vijana wenye mwelekeo mzuri wa tabia na waliojiepusha na matumizi ya mihadharati ambayo inahatarisha  afya na akili zao.

Waziri Fatma Abdulhabib Ferej ameeleza hayo leo Ofisini kwake Migombani alipokuwa akizindua Kamati ya Kitaalamu  ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibi wa dawa za kulevya  yenye wajumbe  kutoka Taasisi mbali mbali za Serikali na binafsi.

Amesema kumekuwa na mwamko wa vijana katika kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya kupitia huduma za makaazi za Marekebisho ya tabia (Sober House)  lakini mwamko huo hautakuwa endelevu  iwapo harakati za usafirishaji, uingizaji na matumizi ya dawa za kulevya hazitoendelea kupigwa vita.


“Harakati za uzalishaji, usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya huleta mtikisiko katika mihimili ya dola na zimekuwa zikiandamana na majanga mbali mbali ikiwemo vifo na  kutoweka kwa amani, ”alisema waziri Fatma.

Amekumbusha kwamba matukio ya miaka ya karibuni ya hapa nchini ya kukamatwa  dawa za kulevya katika viwanja vya ndege unatoa changamoto ya kubuni mikakati imara zaidi  na endelevu ya kukabiliana kikamilifu na tatizo hilo.

Kutokana na hali hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais amesisitiza Kamati ya Kitaalamu kwamba dhima ya kuratibu na kusimamia mapambano dhidi ya dawa za kulevya kuanzia sasa imo mikoni mwao na ameitaka kutekeleza jukumu hilo kikamilifu ili kufikia  kauli mbiu ya “Zanzibar bila ya dawa za kulevya inawezekana”.

Waziri Fatma Abdulhabib Ferej ameihakikishia Kamati hiyo kwamba Ofisi ya Mkamu wa Kwanza wa Rais itakuwa pamoja nao kwa  kuwapatia msukumo na kila msaada katika kukamilisha jukumu linalowakabili.  

Mapema akimkaribisha Waziri Fatma kuzindua Kamati hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Mkamu wa Kwanza wa Rais Omar Dadi Shajak alimueleza kwamba  wajumbe wake wote ni watu mahiri wenye uelewa mzuri wa madawa ya kulvya.

Ameeleza matumaini yake kwamba katika kipindi kifupi kijacho kupitia Kamati hiyo Zanzibar inaweza kuona mwanga wa mafanikio.

Kuundwa kwa Kamati ya Kitaalamu ya Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za kulevya inatokana na mabadiliko ya Sheria ya udhibiti wa wa dawa za kulevya No. 12 ya mwaka 2011 ambapo moja kati ya jukumu lake ni kuishauri Tume katika suala la udhibiti wa matumizi na usafirisha wa dawa za kulveya nchini.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti  wake Kheriyangu Mussa Khamis inawajumbe 11 kutoka Kitengo  cha kuzuia dawa za kulevya cha Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Idara ya Forodha, Mkurugenzi wa Tiba, Sekta binafsi zinazoshughulikia mapambano dhidi ya dawa za kulevya  na wajumbe wawili kutoka  taasisi za dini.

1 comment:

  1. Mimi ningemshauri waziri Fereji angewaingiza maafisa wa JWTZ katika mapambano ya madawa ya kulevya. Hili ninazani lingesaidia kwasababu sina Imani na jeshi lapolisi katika vita hivi kwani wameshindwa takriban miaka 20 au Zaidi wanashulikia madawa ila hakuna mafanikio. Jeshi la Wananchi la TZ wananizamu na management yao ninaiamini kwani wapo na u-nationality kitu ambacho police zbar hawana lote limekuwa corrupted.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.