Na Mwandishi wetu
WATENDAJI na wafanyakazi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na
Michezo, wametakiwa kuendelea kushirikiana katika kutekeleza majukumu
waliyopangiwa katika taasisi zao.
Wito huo umetolewa jana na Naibu Waziri
wa Wizara hiyo, Mhe. Bihindi Hamad Khamis katika tafrija iliyoandaliwa na
uongozi wa Wizara hiyo kuwapongeza watendaji na wafanyakazi wake kwa
ushirikiano waliotoa kufanikisha utekelezaji malengo ya Wizara na kupitishwa
kwa bajeti yake ya mwaka wa fedha 2014-2015.
Mhe. Bihindi aliwaambia wafanyakazi hao
kwamba mafanikio ya Wizara hiyo katika kuwapatia huduma bora wananchi
yanategemea utendaji kazi wa pamoja wa wafanyakazi hao katika sehemu zao za
kazi.
“Kufanikiwa kwa Wizara katika kutekeleza
malengo yake na hatimae kupitishwa bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha
2014-2015, kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano, hivyo endelezeni
ushirikiano huo,” alisisitiza.
Aidha Mhe. Bihindi ameipongeza Kamati ya
Baraza la Wawakilishi ya Mifugo, Utalii, Uwezeshaji na Habari kwa kufanya kazi
kwa karibu na Wizara, pamoja na kuishauri vyema hali iliyosaidia Wizara
kutekeleza vyema majukumu yake, pamoja na kupitishwa bajeti yake ya mwaka wa
fedha 2014-2015.
Mhe. Bihindi aliiahidi Kamati hiyo kwamba
Wizara itaendelea kuipa ushirikiano na kuomba ushauri mara kwa mara katika
utekelezaji majukumu yake.
Akitoa shukurani katika hafla hiyo,
Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Asha Bakari Makame, alisisitiza ushirikiano kwa
watendaji na wafanyakazi wa Wizara hiyo ili waweze kuitumikia vyema jamii
ikizingatiwa kuwa inahusika na mambo yanayohusu maisha ya kila siku ya
wananchi.
Pia aliihakikishia Wizara hiyo kwamba
Kamati itaendelea kutoa ushirikiano na ushauri kila itapoombwa na uongozi wa
Wizara.
Katika hafla hiyo iliyofanyika ukumbi wa
Salama hoteli ya
Bwawani Mjini Zanzibar, iliyoshirikisha watendaji na
wafanyakazi wa Wizara hiyo wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,
Utamaduni, Utalii na Michezo, Dk. Ali Mwinyikai, pia ilihudhuriwa na Wajumbe wa
Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Mifugo, Utalii, Uwezeshaji na Habari
ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Mlinde Mabrouk Juma.
No comments:
Post a Comment