A K Khiari
Hivi karibuni Scotland
itapiga kura ya maoni (Referendum) kuamua kwamba inataka kubaki katika United
Kingdom ama laa.
Kura hii ni muhimu sana kwa
mustakabali wa nchi ya Scotland ambayo kwa miaka mingi imekuwa chini ya himaya
ya Uingereza baada ya kujiunga pamoja na kuunda United Kingdom of Great Britain
and Northern Ireland.
Umoja huu uliundwa mwaka
1801.
Kura ya maoni itafanyika
tarehe 18 Septemba 2014 na kwenye karatasi ya kura kutakuwa na suala moja tu
nalo ni : Je unataka Scotland iwe ni nchi huru? Na jibu liwe ima ni ‘Ndiyo’ au ‘Hapana’.
Scotland, kama Zanzibar,
ilikuwa ni nchi huru ambayo kwa kuungana na Uingereza mwaka 1801 ikapoteza
utaifa wake kama Zanzibar ilivyopoteza utaifa wake walipoungana na Tanganyika.
Scotland, kama Zanzibar,
illiingia katika muungano huu kwa kupoteza utaifa wake na kubakia raia wake
kuwa raia wa Uingereza kama walivyobaki raia wa Zanzibar kuwa ni raia wa
Tanzania baada ya kuungana na Tanganyika.
Scotland, kama Zanzibar,
ilipoteza sarafu yake na benki Kuu na hivi kuamuliwa chini ya UK wakitumia
Pauni ya kiingereza kama ilivyo kwa Zanzibar kutumia sarafu ya Shilingi.
Scotland, kama Zanzibar,
ilibakia na bunge lake dogo ambalo huchaguliwa na wapiga kura na kuwepo kwa
miaka mine na Zanzibar tuna baraza la wawakilishi ambalo pia huchaguliwa kwa
kura kwa muda wa miaka mitano.
Scotland, tofauti na
Zanzibar, imeweza kupata uanachama wa FIFA na hivyo kuweza kushiriki katika
michuano inayotambuliwa na FIFA kama ni nchi kamili licha ya kutokuwa na
mamlaka (Sovereignty) wakati Zanzibar imekosa uwakilishi huu.
Scotland, tofauti na
Zanzibar, imeweza kuienzi na kuitunza historia yake na ya nchi yake wakati
Zanzibar inaonesha mwelekeo wa kupoteza historia yake kwa kutoitunza
kikamilifu.
Scotland, tofauti na
Zanzibar, ilivienzi na kuviboresha vituo vyake vya elimu kama vyuo vikuu na
kuwa kitovu cha elimu kwa vyuo vyake hasa vikuu wakati Zanzibar iliyokuwa
kitovu cha elimu kabla ya Mapinduzi kupoteza umaarufu wake huo.
Moja katika hoja kuu ambazo
Scortland imeamua kuzitumia katika kutafuta uhuru wao kupitia kura ya maoni ni
kwamba Scotland iliyo huru itaweza kukuza uchumi kwa kasi kubwa na kuweza
kufungua milango mingi ya ajira kwa vizazi vijavyo .
Waziri wa kwanza wa Scotland,
bwana Alex Salmond, alitaja mambo makuu 6 ambayo kama yakiwa chini ya
himaya ya Scotland iliyo huru na mamlaka kamili yana viashiria vizuri vya
maendeleo
- Udhibiti
wa moja kwa moja wa kodi ya Biashara
- Udhibiti
wa mapato kwa ujumla
- Udhibiti
wa kodi ya usafiri wa anga
- Udhibiti
katika kuajiri
- Udhibiti
katika sera za kibiashara
- Udhibiti
katika uhamiaji
Mambo haya sita kwa mujibu wa Alex Salmond
yakiwa chini ya Scotland iliyo huru yenye mamlaka kamili na inajitegemea , basi
Scotland itakuwa ni nchi yenye kukua kwa kasi kiuchumi kwani itakuwa na uwezo
kamili wa kutengeneza ajira zitakazowanufaisha waskotishi.
Mambo haya sita yanaweza kufanana kwa
kiasi kikubwa na hoja za kimsingi ambazo Zanzibar, ndani ya kivuli cha muungano,
imeona zinawakandamiza na kama tulivyosikia karibuni kuwepo mjadala wa kuvutana
ilipokuwa ikijadiliwa sura ya 14 ya Katiba inayohusisha mapato na matumizi ndani ya
muungano.
Wakati tukishuhudia na kuona kasi ya
kimaendeleo upande wa pili wa muungano haiendani sambamba na kasi ya maendeleo
upande wa Zanzibar ambayo haina vyanzo muhimu vya kiuchumi vya kujitegemea na
kujikuta imebaki tegemezi wa muungano wakati, kama ni mshirika katika muungano,anatakiwa apate haki kwa kulingana
na uhusiano wake.
Zanzibar pia inaweza kujifunza mengi
kutoka Scotland hasa katika mfumo mzima na utaratibu wa kujenga hoja mpaka
kufikia suala la kuamuliwa ifanyike kura ya maoni na waulizwe wananchi kama
wanataka kubaki katika muungano na ama laa.
Moja katika fundisho la kuzingatia ni
uwezo wa upande mmoja wa muungano kuweza kuleta hoja ya kura ya maoni ya
kujiridhisha kama muungano uliopo uendelee au uvunjike. Upande mmoja wa
muungano, kwa mfano Zanzibar, una uwezo kisheria na kikatiba kuileta hoja hii
na kura ya maoni ikapigwa Zanzibar tu wakati Tanganyika hawatokuwa na haja ya
kupiga kura hii.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwahi
kunukuliwa kwamba kama wangelijua mapema hili jinamizi la muungano liko kubwa
kiasi hiki wangekwenda kuwauliza wananchi kwanza ni muungano upi wanaoutaka
kabla ya kufikiria masuala ya katiba mpya.
Serikali ya umoja wa kitaifa kama
imeliona jambo hili kuwa ni muhimu kwao japo kwa kuweza kupata kujifunza tu
vipi mfumo hii unatumika ingelifanya busara ya kuingia hasara ya leo kwa faida
ya kesho kwa kutuma viongozi wake waandamizi hasa Tume ya uchaguzi, kwenda kuwa
kama Watazamaji “observers” kwenye kura hii ya kihistoria ambayo kimazingira
inawezekana kufanyika Zanzibar na kujifunza kivitendo vipi mfumo wa kura ya
maoni unavyofanyika katika kutafuta mamlaka kamili.
Hapa wasisubiri mwaliko kutoka Scotland
bali wafanye haraka kutafuta njia ya kuweza kuhudhuria kura hii hata kama ni
kwa gharama ya walipa kodi kwani ninaamini kutakuwa na maslahi muhimu kwa taifa
letu ambalo linapita katika kipindi kigumu katika kuwepo kwake.
Ni kweli tayari tumeweza kufanikisha
kura ya maoni kwa mara ya kwanza Zanzibar iliyopelekea kuundwa Serikali ya
umoja wa kitaifa, na kama tutaitumia fursa hii ya kushuhudia kura hii ya maoni
itakayofanyika Scotland mwezi ujao, ninaamini tutapata mengi yenye faida kwa
mustakbali wa nchi yetu bila ya kujali kitu gani waskotishi wataamua kama ni
kubaki au kujitoa katika muungano wao na Uingereza.
No comments:
Post a Comment