Na Haji Nassor, Pemba
WIZARA ya elimu na mafunzo ya amali Pemba, imesema mafanikio makubwa ya kielimu yaliopatikana katika miaka ya hivi karibuni hasa kwa somo la uraia, yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa kituo cha huduma za sheria Zanzibar ZLSC hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa jana na mkuu wa taaluma wa wizara hiyo, Mkubwa Ahmed Omar wakati alipokua akiyafungua mafunzo ya haki za binadamu kwa walimu wa sekondari wanaosomesha somo la uraia, yaliofanyika ukumbi wa skuli ya maandalizi Madungu mjini Chake chake.
Alisema Wizara imekuwa ikiona mafanikio makubwa katika skuli zake mbali mbali kisiwani Pemba na hasa kwa somo la uraia (civis), ambapo ameamini hilo linatokana na ushirikiano mkubwa uliopo baina ya kituo hicho cha huduma za sheria na wizara ya elimu.
Alisema ‘ZLSC’ kimekuwa karibu mno na wizara ya elimu kwa kuwapa elimu ya somo la uraia waalimu wa skuli mbali, jambo ambalo huwajengea uhodari na uwelewa waalimu kulisomesha vyema somo hilo.
Alifafanua kuwa, ijapokuwa waalimu huwa tayari wanauwelewa nalo somo hilo, lakini Kituo cha huduma kimekuwa chachu cha kuwajengea uwelewa kutokana na kuwapa mafunzo kila wakati bila ya malipo.
“Mimi kila siku husikia kwamba kituo cha huduma za sheria kinawaomba waalimu kushiriki katika mafunzo, nasema yamezaa matunda maana sasa twajivunia mafanikio yaliofikiwa’’,alisema.
Aidha mkuu huyo wa taluma kutoka wizara ya elimu, alisema hata wanafunzi wamekuwa wakijengewa uwelewa kupitia kituo hicho, kwa kuelewesha haki, wajibu na hata sheria ya mtoto ya mwaka 2011.
Nae Mratibu wa kituo cha sheria Zanzibar ZLSC, tawi la Pemba Fatma Khamis Hemed, alisema miongoni mwa malengo ya baadae ya kituo hicho ni kuhakikisha jamii inauwelewa wa haki na wajibu wao.
Aidha Mratibu huyo aliwataka waalimu hao kuhakikisha wanakuwa watulivu na kusikiliza kwa makini ili waulize maswali ambayo yatawajengea uwelewa.
Baadhi ya walimu wakichangia mada mbali mbali walisema wamekiri kwamba hawana uwelewa mkubwa wa somo hilo, kwa kutokua na uchache wa ufahamu mkubwa wa katiba ambayo ndio msingi mkuu wa somo hilo.
Mafunzo hayo ya siku mbili ambayo yameandaliwa na kituo cha huduma za sheria Zanzibar ZLSC , ni mfululizo ya mafunzo yanayoendelea kutolewa na kituo cha huduma za sheria Zanzibar, ili kuwajengea uwezo waalimu wa somo la uraia hapa Zanzibar
No comments:
Post a Comment