Habari za Punde

Maalim Seif awapongeza wananchi wa Kisiwapanza kwa mshikamano waliounesha wakati wa maafa



Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad akitembelea maeneo yaliyoathiriwa na upepo mkali huko Kisiwa Panza, Wilaya ya Mkoani Pemba (Picha na OMKR)




Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amewapongeza wananchi wa Kisiwa Panza kwa mshikamano waliouonesha wakati yalipotekea maafa ya upepo mkali Jumatano iliyopita.

Amesema mshikamano huo unadhihirisha jinsi wananchi wanavyoweza kushirikiana katika masuala ya kijamii na kuweka kando tofauti za kisiasa ambazo mara nyingi huwagawa wananchi.

Maalim Seif ameeleza hayo baada ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na upepo huo, na kuelezea kufarajika kwake kwa jinsi wananchi walivyoweza kushirikiana katika kukabiliana na maafa hayo.

Amesema umoja na mshikamano ndio msingi imara wa kuleta maendeleo katika jamii, na kuwataka wananchi kuendeleza utamaduni huo wa mashirikiano wakati wowote yanapotokea masuala ya kijamii.

Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Hemed Suleiman Abdallah, amesema jumla ya nyumba ishirini na tano (25) na familia mia moja na kumi na nne (114) zimeathirika kutokana na upepo huo uliovuma usiku wa kuamkia tarehe 22/04/2015.

Amesema athari nyengine zimetokea kwa vipando vikiwemo migomba pamoja na miti mbali mbali ikiwemo miembe na mikarafuu.

Mapema akitoa neno la shurani kwa niaba ya wananchi waliokumbwa na maafa hayo Bw. Faki Makame Faki ameishukuru seriakali kwa kuwaunga mkono katika maafa hayo.

Ameiomba serikali kuendelea na moyo huo kwa wananchi wakati wote yanapotokea maafa, na kuahidi kuwa misaada inayotolewa itatumika kuwasaidia wananchi walioathiriwa na upepo huo.

Maalim Seif ameungana na wadau wengine kusaidia gharama zilizotokana na maafa hayo na ameahidi kuchagia shilingi milioni tatu (3,000,000)
Hassan Hamad (OMKR).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.