Na Khadija Khamis –Maelezo
Zaidi ya shilingi million 73 za Kitanzania zimetumika kwa ajili ya kufanikisha mradi wa maji safi na salama katika kijiji cha kinduni wilaya ya kaskazini B Unguja ambapo zaidi ya wananchi 5582 watafaidika na mradi huo.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Makaazi Maji na Nishati Ali Khalili Mirza ameeleza hayo mbele ya Waziri wa Kilimo na Maliasili Mhe.Dkt. Sira Ubwa Mamboya wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji safi Kinduni ikiwa ni muendelezo wa shamrashamra za Sherehe ya Miaka 52 ya Mapinduzi Zanzibar .
Alisema fedha zilizotumika kwa kufanikisha mradi huo ni nyingi hivyo iko haja kwa wananchi kuhakikisha wanalinda na kuenzi rasilimali hiyo ili iwe chachu ya kuleta maendeleo katika kijiji hicho na vijiji vya karibu ambavyo vitafaidika na huduma hiyo .
Waziri wa Kilimo aliwataka wananchi wa vijiji hivyo kujenga mashirikiano katika kulinda na kutunza vianziao vya maji ili viweze kudumu kwa muda mrefu na kuondondosha usumbufu wa tatizo hilo .
“Tone moja la maji ni gharama hivyo tunapaswa kuongeza ushirikiano katika kulinda, kutunza na kudumisha rasilimali hiyo tuliopewa,“ Alisema Dkt. Sira .
Hata hiyo Waziri Mamboya aliwataka wananchi kuchangia huduma hiyo ili kukabiliana na gharama ndogo ndogo za uchakavu wa vifaa na kurahisisha kufanyiwa matengenezo haraka iwezekanavyo.
Aliwashukuru wahisani ambao wameunga mkono juhudi za Serikali katika kufanikisha mradi huo wakiwemo Raas Alkheima, Viongozi mbali mbali na wananchi.
No comments:
Post a Comment