Na Bakar Mussa, Pemba
Viongozi wa Chama kikuu cha
Ushirika cha akiba na mikopo Zanzibar,
(ZASCUU) wametakiwa kuwa na uadilifu , nidhamu katika utunzaji wa fedha ili
kuepusha migogoro kwa Wanachama wa taasisi hiyo.
Akizungumza katika ufunguzi wa
mkutano mkuu wa Chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya
ya Chake Chake Pemba, Naibu Katibu mkuu Wizara ya Fedha ya Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, Ali Khamis Juma, alisema kuwa iwapo uadilifu na Nidhamu
katika utunzaji wa Fedha za Wanachama utakuwa na mashaka ni wazi kuwa juhudi za
kufikia malengo ya maendeleo kupitia sekta hiyo yatakwama.
Alieleza ili malengo ya chama hicho
yaweze kufikiwa ni lazima kwa Viongozi wa
taasisi hiyo kufuata sheria zilizowekwa kwa kufanya mikutano inayowahusu
wao na Wanachama wao kwa kuzingatia uwazi na Uwajibikaji kwa kukumbuka kuwa
lengo lwa kuanzishwa kwa taasisi kama hizo ni kuwafanya Wananchi wapate
mkombozi wao katika harakati za kupambana na umaskini wakipato.
“Nidhamu, uadilifu na usimamizi wa
majukumu katika sehemu zozote za kazi ni kitu muhimu , hivyo ni lazima kila
mmoja awajibike kwa sehemu aliyopo ili kujenga utendaji bora na wenye maslahi
kwa umma,” alisema Naibu Waziri wa Fedha.
Naibu Waziri huyo, alifahamisha
kuwa ili ZASCUU, iweze kuwa endelevu ni lazima kuwepo makubaliano ya kweli
baina ya Viongozi na wanaoongozwa, zikiwemo utekelezaji wa ahadi zilizowekwa
ili kujenga Kuaminiana baina ya Viongozi na Wanachama.
Hata hivyo aliwataka Wanachama wa
taasisi hiyo kutowa michango yao iwe ya fedha ama mawazo ya kujenga , yatakayo
saidia kupatikana maendeleo endelevu
ambayo yatawawezesha kufikia malengo yao kwa kuinuwa uchumi wa mtu mmoja mmoja
na Taifa kwa ujumla.
“ Nitafurahi sana nikiona kuwa
chama hichi cha ZASCUU, kinaendelea kuwepo na kutowa tija kwa Wanachama wake ,
jambo ambalo litakwenda sambamba na mkakati wa Serikali wa kukuza Uchumi na
kupambana na Umaskini Zanzibar (MKUZA),”alifahamisha .
Juma , aliwasihi Wanachama wa
Ushirika huo kuwa wadadisi wakubwa juu
ya ahadi wanazopewa na Viongozi wao jambo ambalo litajenga Nidhamu kwa viongozi
wa taasisi hiyo , kwani Viongozi waliowengi wa taasisi hizo
husahau kuwa wao ni Watumishi wa WanaSaccos .
Aliitaka ZASCUU kwa upande wa
kisiwa cha Pemba , kujenga utamaduni wa kusaidiana bila ya kuweka mbele faida (Riba)
kwani lengo lao ni kuona chama chao kinamuwa endelevu na kinatowa mafanikio
makubwa kwa walengwa.
Hata hivyo alitowa wito kwa
Viongozi wa Chama hicho kuwa na ratiba ya utendaji wa kazi za kila siku, jambo
ambalo litaleta ufanisi na kuondowa malalamiko
yasiokuwa ya lazima.
Kwa upande wake , Ofisa Mdhamini
Wizara ya Uwezeshaji , Ustawi wa Jamii Pemba, Mauwa Makame Rajab,
alimuhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa ZASCUU, itafanya juhudi kujitangaza
Kisiwani humo ili kuweza kupata Wanachama wengi zaidi na kukuza mtaji wao.
Aliwataka WanaSaccos , kuondosha
migogoro ndani ya Vyama vyao ili ziweze kuendelea na kuleta mafanikio kwa
Wanachama wake , ambao bila wao haziwezi kustawi.
Hadi
sasa ZASCUU, inajumla ya Vyama (Saccos) 45 wanachama , kati ya hizo 17 ziko Kisiwani
Pemba na 28 Unguja , ambapo malengo yao ni kuhakikisha ina Vyama visivyopunguwa
150 vya akiba na mikopo kwa Zanzibar mzima na vinakuwa Wanachama ifikapo mwaka
2018
No comments:
Post a Comment