Habari za Punde

Mwambusi wa Yanga Avutiwa na Vipaji Vilivyojificha Kisiwani Pemba

Na Haji Nassor, Pemba
MSADIZI Kocha wa klabu ya Yanga inayokipiga Ligi kuu ya Tanzania bara, Juma Mwambusi, amekunwa na wanandinga wa klabu ya Cossovo ya Wambaa, inayoshiriki ligi daraja la kwanza taifa Pemba, na akisema ndani ya kikosi hicho, wamo wachezaji wanafaa kwenye kikosi cha pili cha klabu yake.

Alisema ingawa hana mpango wa kuwafuatilia, maana hiyo ni kazi ya Idara nyengine ndani ya Yanga, lakini kama ingekuwa anasaka wachezaji basi ndani ya Cossovo, wapo baadhi ambao kama wakifundishwa wanaweza kufika mbali kisoka.

Mwambusi alitoa ya maoyoni ndani ya uwanja wa Gombani Chakechake, siku moja baada ya kuwasiliki kisiwani Pemba, kujiwinda na mchezo wa ligi kuu ya Vodacom na Azam, wakati akizungumza na mwanadishi wa habari hizi.

Alisema kisiwa cha Pemba, kimejaaliwa kuwa na wachezaji wazuri wa kusakata kambumbu, ingawa wanapoteza mwelekeo kwa baadhi ya vilabu kukosa waalimu wenye sifa za kufundisha.


Alitolea mfano mchezo huo wa ligi daraja la kwanza taifa Pemba alioushuhudia baina ya Cossovo na Masota, akisema kutokaa na nidhamu ya wachezaji wa vikosi viwili hivyo, pindi vikipata waalimu wenye sifa, miaka michache ijayo kungezaliwa wachezaji bora.

‘Unajua mwandishi sikuwa makini sana kuangalia mechi hii, lakini hizi dakika 45 ambazo nimeshuhudia basi, nakiri vipaji Pemba vipo, maana klabu mbili hizi vimenitosha kuthibitisha hilo’’,alisema.

Msaidizi Kocha huyo aliwataja wachezaji wa Cossovo ambao anadhani kwamba wanaweza kufika mbali ni pamoja na washambuliaji Shaali Ramadhan Hassa na Abdalla Kombo Abdalla, ambapo kwa Masota Khamis Abdalla.

Hata hivyo, aliwataka makocha wa vilabu vyote kisiwani Pemba, kuwa makini wanapowafundisha vijana kucheza soka, maana sasa mpira umepiga hatua kubwa mbele, ikiwa ni pamoja na kutengeneza ajira.

Mwambusi alisema alimshangaa kocha mwenzake wa klabu ya Masota, kwa kuchelewa kwenye mchezo wa ligi na kisha wachazaji wake kukosa kufanya mazoezi madogo kabla ya kuingia uwanjani.

“Timu inapochelewa uwanjani, basi kabla ya kucheza lazima japo sekunde 45 wafanye ‘warm up’maana kinyume chake, mara mchezaji anaumia’’,alifafanua.


Klabu ya Yanga ikiwa na Kocha wake Mkuu Hans van Der Puljim, iliwasili juzi Febuari 29 kwa ajili ya kuweka kambi kisiwani Pemba, kwa mara ya pili, ili kujitayarisha kwa ajili ya mchezo mkali baina yake na Azam unaotarajiwa kufanyika Machi 5 uwanja wa Taifa Da-es salaam.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.