Habari za Punde

Wanaushirika wa Kitandu wasema siasa kwao si kegezo cha kuendesha shughuli zao


 Akinamama wa kikundi cha ushirika na  Kitundu Co-0p cha Jundamiti Kiwani Mkoani Pemba, wakipalilia Viazi lishe katika Ushirika wao bila ya kujali Itikadi zao zao kisiasa wakati wako katika Itikadi tafauti za kisiasa.


Katibu wa kikundi cha Ushirika cha Kitundu Co-op, cha Jundamiti Kiwani , Abdalla Talib, akizungumza na Mwandishi wa habari juu ya kikundi chao cha Ushirika kilivyo na wafuasi wa Vyama tafauti lakini katika kazi zao siasa huwa haipewi nafasi na huwa wanasaidiana kwa hali na mali.

Picha na Mchanga Haroub -Pemba.

Na Mchanga Haroub- Pemba.

Ama kwa hakika umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu na haipendezi hata kidogo kuona katika visiwa hivi vya Unguja na Pemba watu wake hawaishi  kwa kuunganisha nguvu zao ili kutatuwa kero mbali mbali ambazo zimo ndani ya uwezo wao eti kwa tofauti za kisiasa haipendezi.

Mshikamano wa njia ya kuishi kwa kusaidiana ndio njia pekee itakayoleta maendeleo ya haraka katika vijiji na mifarakano isio msingi huleta mabalaa na mtafaruku miongoni mwa jamii na kudumaza hata shuhuli za kiuchumi.

Uwepo mfumo wa vyama vingi katika nchi isiwe sababu ya watu kutokushirikiana kutokana na misimamo tofauti ya vyama vyao bali ichukuliwe kama njia ya ushindani wa kuleta mabadiliko ya kimaendeleo.


Nilimnukuu katibu wa ushirika wa Kitandu Co –operative society akisema…’’siasa isitushuhulishe kwani siasa ni jambo jengine na maisha ni kitu chengine’’alisema hivyo akiwa na maana kwamba hakuna sababu ya watu kuacha kufanya kazi zao za maendeleo na kuanza kujadili siasa.

Aliwaasa sana wananchi wenzake kuachana na siasa za chuki ambazo zinaweza kusababisha uhasama miongoni mwa jamiina kupelekea kutoweka kwa amani ya nchi.

Alisitiza kusema kwamba amani ikitoweka hakuna faida itakayopatikana zaidi ya madhara makubwa kwa jamii na alimalizia kusema kwamba ni lazima jamii iweka mikakati ya makusudi ya kuienzi amani iliopo kwa vile wao wamerithi amani basi wairithishe pia amani hii kwa vizazi vijavyo.

 ‘’Kwenye kazi ni kazi tuu, katu hatuchanganyi kazi na siasa .’’ndivyo anavyosema Abdalla Talib Abdalla, katibu wa ushirika wa Kitandu Co –operative Society uliopo Kitondooni shehia ya Jutamiti Kiwani Pemba.

Alisema “ uwepo wa marudio ya uchaguzi haijawa sababu ya kusitisha kazi zetu  za ushirika kwa kushuhulika na siasa ,kwani siasa kwetu  tunaona ni mchezo tu hivyo tunajali zaidi kujipanga katika maisha kwa faida yatu na vizazi vyetu   kwa ujumla”.

Abdalla, alieleza kwamba pamoja na kuwa katika ushirika wao kuna watu wa vyama tofauti lakini wanapokuwa katika ushirika wao hawatoi mwanya wa kuzungumza mambo yanayohusu vyama vyao vya siasa kwakuwa wanajuwa kwamba sio pahala pake kwani wanataka kila mmoja awe huru kufanya kazi zake za ushirika.

Akizungumzia suala la baadhi ya watu kugomeana katika vijiji vyengine, alisema yeye hilo haoni kama ni jambo la busara kwani watu wote ni ndugu hivyo haipaswi kutengana au kutokusaidiana katika shuhuli za kijamii.

Alisema kila mtu anamuhitaji mwenzake kwa njia moja au nyengine hivyo wakiendesha siasa za chuki watashindwa kusaidiana kitu ambacho hakipendezi kutokea miongoni mwa jamii kwani hakuna mkamilifu.

‘’Ili jamii iendelee inahitaji mashirikiano ,na mashirikiano hayawezi kupatikana ikiwa wananchi wataichukulia siasa kinguvu nguvu’’ alisema katibu huyo wa ushirika wa kitandu co operative society.

Katibu huyo, alieleza mshikamano wao na kuondoa tofauti zao za kisiasa kumewawezesha kujikusanya pamoja na kuanzisha kikundi hicho cha ushirika ambacho kwa sasa kimekuwa ni mkombozi katika kijiji chao.

Umoja wao huo umewawezesha kutatua baadhi ya changamoto zilizopo katika kijiji chao ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa maji ya uhakika ya kumwagilia mashamba yao ya mboga mboga na kuwafanya waweze kuendeleza kilimo hicho kwa mda wote kwani sasa hawategemei zaidi mvua.

Alisema’’ baada ya kuchimba kisima tulizidi kuimarisha kilimo cha mboga mboga na viazi lishe na kimsingi tunafanya kilimo cha mzunguko ili kuepuka matumizi ya mbolea za kemikali hivyo mboga zetu ni salama zaidi’’  alijisifia katibu huyo.

Bibi Khadija Mussa ni mwanachama wa ushirika huo, alisema  kwa upande wao akina mama uwepo wa ushirika huo umewasaidia sana kupunguza umasikini na kamwe hawako tayari kuusambaratisha kwa njia yoyote ile.

‘’Sisi kwa upande wetu ushirika huu umetufanya tushikamane zaidi kwani ikiwa mwenzio hujamuona kwenye ushirika lazima wapata wasi wasi na kumfutilia ukajuwa tatizo lake’’alisema.

 Alifahamisha kupitia ushirika huo  pia huwa wanapata muda wakujifunza mambo mengine mbali mbali ya kijamii kutokana na mambo mengi ambayo hayaingilii itikadi ya mwanachama wa Ushirika huo.  

Alisema kupitia ushirika huo akina mama wa kijiji cha Kitondooni wamejuwa namna ya kutengeneza lishe bora kwa ajili yao na watoto wao kwa kutumia vazi lishe ambavyo wanazalisha katika ushirika wao.

Khadija  alifahamisha katika kijiji chao Afya za akina mama zimeimarika zaidi kwani viazi lishe vina sifa ya kuongeza damu na inavirutubisho vya kutosha kwa akina mama wajawazito, hivyo kutokana na hilo aliwasisitiza sana akina mama kujitolea kwa hali na mali kuhakikisha ushirika wao unadumu na haukumbwi na dhoruba za kisiasa zilizopo nchini.

Alieleza kwa vile wanaupendo wa dhati katika ushirika wao, ikitokea mwanaushirika anatatizo basi wote hushirikiana kumsaidia kutatuwa tatizo lake au hata kumpatia pesa za mkopo kutatuwa tatizo lake lakini zaidi hutegemea na uzito wa tatizo ndio apatiwe mkopo.

Hivyo alisema  wa ichukulie siasa kama jina lake kwani siasa ni utaratibu hivyo wasiichukulie nguvu kwani itawaadhibu na kamwe wasikubali kutawaliwa na jazba kwani jazba siku zote hazijengi hubomoa na mwishowe ni majuto. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.