Habari za Punde

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba ahimiza ukusanyaji wa mapato ya Serikali

Na Masanja Mabula –Pemba 
 
MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Omar Khamis Othman amesema Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya pamoja na Baraza la Mji Wete, ambaye atashindwa kutekeleza wajibu wake , atatumia nguvu alizonazo  kisheria  kumuweka rumande masaa 24 , kwani atakuwa ni chanzo cha kukosekana mapato ya Serikali .
 
Alisema kuwa ni wajibu wa kila mfanyabiashara kukata leseni za biashara yake ili aweze kuchangia mapato ya Serikali Kuu ambayo baadaye hurejea kusaidia miradi ya maendeleo ya wananchi .
 
Alisema kuwa mapato ya Serikali hupotea kutokana na watendaji wanaohusika na ukusanyaji wa mapato kushindwa kuwajibika kutokana na suala la rushwa na muhali, jambo ambalo alisema  serikali ya Mkoa haitalivumilia .
 
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na watendaji wa Halmashauri za Wilaya ya Wete na Micheweni , watendaji wa Baraza ka Mji wete pamoja na watendaji kutoka Serikali za Wilaya juu ya kuimarisha suala la ukusanyaji wa mapato
 
Aidha aliwataka wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya  na Baraza la Mji Wete kuondoa muhali katika suala la ukusanyaji wa mapato kwa kuhakikisha wafanya biashara wanakata leseni za biashara zao.
 
“Ninao uwezo na nguvu kisheria wa kumweka rumande mtumishi wa Serikali masaa 24 , ambaye atashindwa kutekeleza wajibu wake, mimi sitangoja kutumbuliwa jipu nitaanza  na atakaye onyesha uzembe katika agizo hili ”alieleza.
 
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa mapato ya Serikali hupotea kutokana na watendaji wanaohusika na ukusanyaji wa mapato kushindwa kuwajibika kutokana na suala la rushwa muhali , jambo ambalo amesema  haitalivumilia .
 
Pia aliwataka kutumia lugha nzuri kwa wateja wao kwa kuwaelimisha , na wakiendelea kukaidi wawafiishe ofisini kwa Mkuu wa Wilaya kwa hatua zaidi .
 
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Micheweni  Abeid Juma Ali amewasisitiza watendaji wa Halmashauri na baraza la Mji kufuata sheria na miongozo wakati wanapotekeleza majukumu ya kazi zao 

 Alisema kwamba iwapo sheria zitatumika ipasavyo kila mfanyabiashara atakata leseni yake bila ya usumbufu na kuwasisitiza kuwachukulia hatua wanaoendesha biashara bila ya kuwa na leseni .
 
“Sheria zipo lakini hazitumiki , zitumieni kuhakikisha kwamba kila mfanyabiashara abakuwa na leseni na ambaye anakiuka mchukulieni  hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kumfikisha mahakamani ”alifahamisha .
 
Akichangia katika Mkutano huo , Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Wete Mmanga Juma Ali  alisema ili kuzipatiwa ufumbuzi changamoto zinazowakabili wanahitaji kupatiwa askari watakaoongozana nao kupita madukani na kudai leseni .
 
Alisema kuwa kipindi cha vuguvugu la kisiasa , mapato ya Halmashauri yamepungua kutokana na wafanyabiashara wengi kuendesha biashara bila ya kukata leseni .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.