Habari za Punde

DC Kati atoa wiki moja daktari kuhamia Unguja Ukuu

Na Salum Vuai, MAELEZO
Mkuu wa Wilaya ya Kati Mashavu Sukwa Said, ametoa muda wa wiki moja kwa daktari wa kituo cha afya Unguja Ukuu kuhamia katika nyumba anayopaswa kuishi kijijini humo kuanzia jana Septemba 9, 2016.

Amesema kama kuna matatizo yoyote yanayosababisha daktari huyo ashindwe kuhamia kwenye nyumba hiyo, afike ofisini kwa kiongozi huyo kabla ya Septemba 15, mwaka huu kumueleza ili hatua za kurekebisha zichukuliwe.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya alisema nyumba hiyo imekamilika ikiwa na huduma zote muhimu, maji, umeme na pia iko safi, lakini anashangazwa kwa nini haijahamiwa hadi alipotoa agizo.

Amri hiyo ni ya pili kutolewa na Bi. Mashavu, ambapo wiki chache zilizopita alifika katika kituo hicho, akakikagua na kujiridhisha kwamba hakina tatizo na kuagiza kwa watendaji wa afya wilayani kuhakikisha daktari husika anahamia mara moja.

Alieleza kushangazwa kwake kuona hadi sasa hakuna daktari aliyehamia katika nyumba hiyo. 

Alilazimika kurejea kutoa agizo hilo, baada ya suala hilo kutajwa na baadhi ya wakaazi wa Unguja Ukuu juzi kuwa ni kero, wakati wa hafla ya uzinduzi wa mabaraza ya vijana wa shehia za Kaepwani, Tindini na Kaebona iliyofanyika kijijini hapo.

Alisema si vyema kwa daktari kuishi mjini na kuiacha nyumba hiyo bila kukaliwa, hali aliyoeleza kuwa ni usumbufu kwa wananchi wa huko hasa pale kunapotokezea dharura ya kuugua wakati wa usiku.

“Nyumba hii imejengwa ili daktari awepo karibu na wananchi na aweze kuwahudumia pale kunapokuwa na mgonjwa mwenye hali mbaya nyakati za usiku. Nataka ndani ya wiki moja daktari awe amehamia, na kama kuna tatizo waje wanione tutafute ufumbuzi,” alisisitiza.

Alieleza kuwa iko haja kwa daktari kuhamia haraka katika nyumba hiyo, kwani mbali na Unguja Ukuu, kituo hicho kinategemewa na shehia nne ikiwemo  jirani ya Kikungwi.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili, walikaririwa wakisema kwamba hakuna sababu ya kukosekana daktari wa kuishi kijijini hapo, kwani nyumba hiyo iko katika hali nzuri.

“Hali hii inatusumbua sana kwani mara nyingi akitokezea mgonjwa usiku na hulazimika kutafuta gari kwa ajili ya kwenda ama Makunduchi au mjii. Ni Tunaomba muhusika atekeleze agizo la DC kwa ajili ya kuwahudumia wananchi,” alifahamisha Salama Abdalla, mkaazi wa shehia ya Tindini.

Hata hivyo, akizungumzia suala hilo, sheha wa shehia ya Tindini Haroun Rashid Haroun, amesema ingawa nyumba hiyo imekamilika kiujenzi, lakini haina samani yoyote kama vile vitanda na vifaa vyengine vya matumizi.

Alisema, kwa mujibu wa daktari huyo, anachosubiri ni kupatiwa kwa vifaa hivo ili aweze kuhamia.

Aidha, alisema daktari huyo alikuwa likizoni na kwamba sasa ni wiki ya pili tu tangu aliporipoti kazini, lakini ukosefu wa samani ndio uliomzuia kuhamia katika nyumba hiyo.

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

9 SEPTEMBA, 2016   

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.