STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 26.09.2016
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba imedhamiria kwa makusudi kuitilia
mkazo na kuiimarisha sekta ya uwekezaji ambayo matunda yake yatawasaidia
wananchi wote wa Zanzibar.
Dk. Shein aliyasema hayo leo alipofanya
mahojiano na waaandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali mara baada ya
kumaliza ziara yake ya kuitembelea miradi ya Kampuni ya Bakhresa ikiwemo ujenzi
wa nyumba huko Fumba pamoja na ujenzi wa hoteli ya kisasa huko Mtoni mjini
Zanzibar.
Dk. Shein alisema kuwa mradi mkubwa wa
ujenzi wa nyumba za kisasa huko Fumba utasaidia kwa kiasi kikubwa kutokana na Serikali
kuweza kupata pato sambamba na wananchi wa Fumba na maeneo jirani kuweza kupata
ajira.
“Fumba ilikuwa imefumba lakini hivi sasa
itafumbuka kwani kukamilika kwa mradi huu Fumba itakuwa ni sehemu ya pekee
katika kukuza uchumi wetu pamoja na kuwasaidia wananchi wote kutokana na pato
litakalopatikana katika maradi huo”,alisema Dk. Shein.
Alisema kuwa matarajio ya ujenzi huo ambao
kwa maelezo ya uongozi wa Kampuni hiyo, eneo hilo litakuwa ni Dubai ya Zanzibar
linatoa matumaini makubwa katika kuuimarisha uchumi wa Zanzibar, ambapo mradi
huo utajulikana kwa jina la ‘Uptown Living’.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa nchi nyingi
duniani ziliazia na miradi kama hiyo ambazo zilikuwa ni masikini kuliko Zanzibar
lakini hivi sasa zimeweza kupiga hatua kubwa na kuwa nchi tajiri kutokana na
kuwepo miradi kama hiyo na kueleza kuwa kinachofanywa na serikali katika suala
zima la uwekezaji ni tija kwa wananchi wote,
Kutokana na juhudi hizo Dk. Shein alitoa
wito kwa wananchi wa Zanzibar kuheshimu na kufuata taratibu zote zilizowekwa na
Serikali juu ya suala zima la matumizi ya ardhi.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisikitishwa
na tabia ya baadhi ya wananchi kuvunja sheria na taratibu zilizowekwa juu ya
umili wa ardhi huku wakitambua kuwa ardhi ni mali ya serikali hivyo kila mmoja
ana jukumu la kuilinda na kuitunza ardhi iliopo.
Kwa upande changamoto ya ajira kwa vijana
wa Zanzibar hasa katika sekta ya utalii, Dk. Shein alieleza kuwa jambo muhimu
ambalo litawapa vijana wa Zanzibar kuajiriwa kwa haraka katika sekta hiyo ni
kuwa na elimu ya fani hiyo.
Alisema kuwa suala la elimu ni muhimu sana
na kutoa wito kwa vijana wa Zanzibar kujikita zaidi katika kujitafuatia elimu
na ndio maana Serikali anayoiongoza imeweza kutilia mkazo suala hilo kwa
kukiimarisha Chuo chake cha Huduma za Watalii kiliopo Maruhubi kwa kutoa
mafunzo ya Cheti, Diploma huku kukiwa na mchakato wa kukiingiza kuwa ni sehemu
ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Dk. Shein alisisitiza kuwa iwapo vijana
watakuwa na elimu ya kutosha suala la upendeleo halitochukua nafasi huku akitoa
inzari umuhimu wa elimu kwa hi sasa kwa vijana hao hasa katika ushindani wa ajira
katika soko la Afrika Mashariki.
Mapema Dk. Shein alipata nafasi kutembelea
mradi ya nyumba za kisasa zinazojengwa na Kampuni ya Bakhresa huko Fumba akiwa
na mwenyeji wake Said Salim Bakhresa na kupata maelezo juu ya uendelezaji wa
mradi huo utakaojenwga nyumba 600 ambapo awamu ya kwanza ni wa nyumba 92 za
kisasa zinazoendelea kujengwa ambazo zitakuwa kwa ajili ya wananchi wenye
kipato cha juu na kipato cha kati.
Mradi huo ambao mbali ya nyumba utakuwa na
eneo maalum la bustani kwa ajili ya wananchi, bandari ambayo itawasafirisha
wakaazi wa eneo hilo kutoka eneo hilo hadi Dar-es-Salaa kwa boti maalum
zitakazokuwepo eneo hilo huku uongozi huo ukieleza hatua zitakazochukuliwa
katika kuhakikisha suala ziama la ulinzi na usalama linaimarishwa.
Pia, Dk. Shein alipata fursa ya kuangalia
mtambo wa kisasa wa kupikia lami unaomilikiwa na Kampuni hiyo ya Bakhresa na
baadae kukagua barabara itakayotoka eneo hilo hadi uwanja wa ndege.
Ziara ya Dk. Shein ilimalizia huko Mtoni
nje kidogo ya mji wa Zanzibar ambapo alijionea ujenzi wa hoteli hiyo
itakayokuwa na sifa ya kimazingira ‘Eco Friend’ ambayo inajengwa kwa umiliki wa
Kampuni hiyo ambayo inatarajiwa itakuwa ni ya pekee katika ukanda wa Afrika
Mashariki.
Kwa mujibu wa maelezo ya Mkuu wa ujenzi wa
mradi huo Salim Aziz, alisema kuwa hoteli hiyo itajitosheleza kwa huduma za
maji na umeme na kupunguza gharama
katika matumizi hayo.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alitembela eneo
la bahari kuona shughuli za ufukiaji bahari ‘Land Reclamation’ lenye ukubwa wa
heka 4 ambalo ni eneo la hoteli hiyo linalotarajiwa kuwa na maegesho ya meli
ndogo na meli kubwa, huduma za bustani ya maji ambayo inajumuisha michezo ya
kila aina itakayochezwa na wananchi pamoja na watalii.
Akimalizia Ziara yake, Dk. Shein
alitembelea Gofu la Mtoni ‘Mtoni Palace Ruins’ na kupata maelezo ya kihistoria na
hatimae alipata mapumziko yalioambatana na burudani mwanana kutoka kikundi cha
Rahatul-zaman na kutumbuizwa kwa nyimbo zilizoibwa na Kitukuu cha Siti Bint
Saada pamoja na mpiga Ganon maarufu Zanzibar
Nasor Mohamed hapo katika mkahawa wa hoteli hiyo.
Katika ziara yake hiyo, Dk. Shein alifuatana
na viongozi mbali mbali wa vyama na Serikali.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment