Habari za Punde

Serikali kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na changamoto sekta ya Elimu




STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                   19.09.2016
---
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kuchukua juhudi za makusudi katika kukabiliana na changamoto zote zinazoikabili sekta ya elimu, hatua kwa hatua ili kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa kuanzia ngazi ya elimu ya maandalizi, msingi, sekondari hadi elimu ya vyuo vikuu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo  katika kilele cha sherehe za Tamasha la Elimu Bila Malipo huko katika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba imeamua kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha katika sekta ya elimu kwa lengo la kuimarisha miundombinu na huduma ili kuongeza ubora wa elimu.

Dk. Shein alisema kuwa Serikali itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kufanya jitihada katika kuimarisha sekta ya elimu kutokana na umuhimu wake wa kuandaa wataalamu wa nyanja zote muhimu za kuchochea maendeleo ya nchi.

Alisema kuwa Zanzibar kama ilivyo kwa nchi nyengine, inahitaji wataalamu wa fani mbali mbali wakiwemo wahandisi, madaktari wa fani mbali mbali, warusha ndege, wachimbaji mafuta na gesi, wavuvi na wafugaji wataalamu walimu, wataalamu wa utashi na mabingwa wengine wa fani tofauti.

“Tutaendelea kuhakikisha kwamba tunazikabili changamoto zote zinazoathiri katika kufikia lengo letu la kutoa elimu bora kwa wananchi wetu”,alisema Dk. Shein.

Aidha, alisisitiza kuwa katika utekelezaji wa azma hiyo Serikali, itahakikisha kuwa mafanikio yanazidi kupatikana katika utekelezaji wa uamuzi wa Serikali wa kuondoa michango kwa wazazi katika elimu ya Msingi na katika mitihani ya Taifa ya skuli za sekondari huku serikali ikiangalia uwezekano wa kuondoa michango yote kwa skuli za sekondari pale hali ya mapato itakaporuhusu.

Alisema kuwa Serikali imefidia michango ya wazee ili kuwapa fursa watoto wote kupata haki yao ya msingi ya kupata elimu kwa dhamira ile ile ya Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ya kutangaza elimu bure hapo tarehe 23 Septemba, miaka 52 iliyopita.

Dk. Shein alieleza kuwa mbali ya vifaa walivyopewa wanafunzi wa skuli za maandalizi na msingi zikiwemo chaki, madaftari ya kuandikia na ya mahudhurio pia, skuli zote za serikali zenye wanafunzi wa maandalizi, ikiwa ni za maandalizi au msingi zimeingiziwa fedha taslim kulingana na idadi ya wanafunzi wao kwa ajili ya kuwapatia chakula wanafunzi.

Alisema kuwa Serikali ina lengo la kuhakikisha  kila mtoto aliyefikia umri wa kuanza skuli, anapata fursa hiyo na kuipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa mafanikio yanayoendelea kupatikana katika kuitekeleza azma hiyo kwa ufanisi mkubwa.

Dk. Shein alisema kuwa hatua iliyofikiwa katika kipindi cha miaka 52 tangu kutangazwa kwa elimu bure ni ya mafanikio makubwa na si ya kubezwa hata kidogo kwani kabla ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 idadi ya skuli ilikuwa ni cgache sana mbali na elimu yenyewe kutolewa kwa misingi ya ubaguzi.

Alieleza kuwa Serikali tayari imeanza ujenzi wa vyuo vipya vya mafunzo ya Elimu na Amali huko Makunduchi hapa Unguja na Daya Mtambwe huko Pemba, ili kuwawezesha vijana kupata ujuzi na kuweza kujiajiri wenyewe.

Vile vile alieleza kuwa katika muda mfupi ujao serikali itakamilisha ujenzi wa skuli za sekondari Donge, Kibuteni na Mkanyageni huku akieleza azma ya serikali ya Awamu ya Saba kuliondoa tatizo la madawati.

Dk. Shein pia alitoa agizo kwa Wizara ya  Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kufanya haraka katika kuwaajiri walimu maalum waliopata mafunzo katika ngazi ya Stashahada na Shahada ya Kwanza masomo ya Hesabati na Sayansi.

Aidha, aliongeza kuwa amefanya makusudi katika kuiunda Idara ya Michezo na Utamaduni kwa lengo la kuimarisha shughuli za michezo na utamaduni katika skuli za hapa nchini ili kutoa fursa kwa vijana kushiriki katika shughuli za michezo na utamaduni wakiwa skuli.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma alitoa pongezi kwa Dk. Shein kutokana na jitihada zake katika kuimarisha sekta ya elimu huku akieleza kuwa Sherehe za Tamasha la Elimu Bila ya Malipo limeweza kuwaweka pamoja kama ndugu vijana 2000 wakiwemo 800 kutoka Pemba.

Waziri Pembe aliahidi kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali itaendelea kutoa elimu bora na kufufua vipaji kwa vijana hasa vile vilivyopo na kupongeza hatua za Rais za kuunda Idara ya Michezo na Utamaduni pamoja na kutoa shukurani kwa wale wote waliochangia sherehe hizo.

Mapema Dk. Shein alipokea maandamano ya wanamichezo wote walioshiriki mashindano ya Elimu Bila ya Malipo mwaka huu, aidha sherehe hizo zilipambwa kwa gwaride la wanafunzi, michezo ya watoto wa maandalizi, mbio za vijiti, pamoja na ngoma ya mwanandege iliyochezwa na wanafunzi kutoka skuli ya Kombeni.

Sherehe hizo zilizofikia kilele chake hivi leo tarehe 23 Septemba 2016 zina lengo la kuienzi siku hii ya kihistoria katika maendeleo ya elimu sambamba na kumkumbuka mwasisi wa Mapinduzi Marehemu Mzee Abeid Amani Karume kwa kutangaza huduza za elimu bila ya malipo kwa watoto wa wakwezi na wakulima wa Zanzibar ambao walikosa elimu kutokana na unyonge wao wa kutawaliwa.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.