Habari za Punde

Naibu Waziri wa Afya akagua vituo vya afya wilaya ya kati

Na Mwashungi Tahir, Maelezo Zanzibar

NAIBU Waziri wa Afya  Harusi Said Suleiman, amewataka wafanyakazi wa vituo vya afya nchini kutumia lugha nzuri wakati wanapowahudumia wagonjwa ili kuwajengea imani na mapenzi kwao.

Aidha, amewasisitiza kuwa na huruma wakielewa wagonjwa ni binadamu wanaohitaji kufarijiwa wanapokuwa wanaumwa.

Wito huo ameutoa leo Disemba 21, 2016  katika ziara aliyoifanya kukagua vituo vya afya vilivyoko wilaya ya Kati na kuzungumza na wafanyakazi  wa vituo hivyo.

Naibu Waziri huyo amesema, mbali ya dawa zinazotolewa kwa wagonjwa, lakini lugha nzuri na unyenyekevu wa madaktari na wauguzi katika kuwahudumia, ni tabibu mzuri kwao.

Amefahamisha kuwa, lugha nzuri, imani na upendo, ndio njia pekee inayoweza kuwafariji wagonjwa na kuwahamasisha kuvitumia vituo vya afya kila wanapopatwa na maradhi.

Aidha, amewahimiza wafanyakazi wa vituo hivyo kuongeza ushirikiano kazini kati yao wenyewe pamoja na viongozi wao ili kuleta ufanisi katika utendaji wa kazi.

Akiwa katika ziara hiyo, amepata fursa ya kufahamu changamoto mbalimbali zinazovikabili vituo vilivyomo wilayani humo, ikiwemo ukosefu wa vitendea kazi,  uhaba wa madaktari.

Katika kituo cha Bambi, Naibu Waziri huyo alibaini tatizo la kuvuja kwa paa pamoja na ukosefu wa maji safi na salama.
Hata hivyo, ameeleza kufurahishwa na moyo wa kujituma walionao wafanyakazi licha ya kukabiliwa na mazingira magumu.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Kati Mashavu Sukwa Said, ameuomba uongozi wa Wizara ya Afya kupunguza tabia ya kuwahamisha madaktari mara kwa mara, akisema kufanya hivyo ni usumbufu kwao pamoja na wagonjwa.

Mkurugenzi Kinga Dk. Fadhil Mohammed Abdalla, amesema wizara inatambua kuwepo na uhaba wa wafanyakazi katika vituo mbalimbali lakini akasema tayari tatizo hilo linashughulikiwa.

Vituo vya afya vilivyotembelewa ni Uzini, Bambi na Mwera.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.