Habari za Punde

Michezo ya Majeshi Kuanza Kurindima Kesho Uwanja wa Amani kwa Ufunguzi Zanzibar.

Na.Mwinyimvua Abdi, Zanzibar.

MKUU wa majeshi ya ulinzi Tanzania ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMATA) Jenerali Vennance Mabeyo amewataka wananchi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi kushuhudia michezo mbali mbali itakayoshirikisha vikosi vya ulinzi na usalama wakati wa mashindano maalum waliyoandaliwa na baraza hilo yatakayoanza Machi 18, 2017.

Mashindano hayo yaliyoanzishwa mwaka 1984 na kushindwa kufanyika kwa muda wa miaka 13 kutokana na uchache wa rasilimali, yatahusisha michezo ya soka kwa wanaume, mpira wa pete, wanawake, mpira wa mikono (hand ball), mpira wa kikapu (basket ball), na mpira wa wavu (volley ball) kwa wanawake na wanaume yatazinduliwa rasmi na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein katika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.

Akitoa taarifa kwa umma hivi karibuni katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika makao makuu ya Brigedi ya Nyuki Migombani Zanzibar, Jenerali Mabeyo alisema kujitokeza kwao kutawaongezea ari ya ushindani wanamichezo hao na kufanya vizuri zaidi hali itakayoviimarisha vikosi hivyo kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.

Alisema kwa miaka mingi wanamichezo na timu za majeshi zimekuwa zikifanya vyema katika michezo mbali mbali ya kitaifa na kimataifa jambo lilioonekana kufifia katika miaka ya karibuni hivyo anaamini mashindano hayo yataibua ari na mwamko wa timu hizo kufanya vyema.

Mwenyekiti huyu alizitaja timu zitakazoshiriki kuwa ni ngome inayoundwa na jeshi la ulinzi wa wananchi wa Tanzania (JWTZ), jeshi la kujenga taifa (JKT), polisi, magereza, uhamiaji, zimamoto na timu ya vikosi vya idara maalum ya SMZ.

Mabeyo ambae ambae pia ni mkuu wa jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) aliyataja mashindano hayo pia kuwa ni miongoni mwa majukwaa yanayowakutanisha wanajeshi kwa lengo la kuimarisha upendo na maelewano miongoni mwao ndio maana bamata imeona haja ya kuyaendeleza.

“Pamoja na kushindana katika michezo mbali mbali, mwisho wa yote sote tutakuwa washindi kwa kuwa mashindano haya yapo kwa ajili ya kuendeleza umoja na mashirikiano yetu kama wadau katika ulinzi na maendeleo ya taifa letu”, alisema Mkuu huyo wa majeshi.

Aidha Jenerali Mabeyo alivipongeza vyombo vya habari nchini kwa kuwa karibu na kutangaza habari na matukio mbali mbali yanayolihusisha jeshi hilo, na kuwaomba kufanya hivyo katika mashindano hayo ili kuwahamasisha watazamaji na washiriki wa michezo hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.