Habari za Punde

Ziara ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli Mkoa wa Pwani Imejaa Tija.

Na.Emmanuel John Shilatu
Rais Magufuli amemaliza ziara ya siku 3 mkoani Pwani iliyoanza tarehe Juni 20, 2017 kwa mafanikio yenye tija lukuki kwa Wana wa mkoa wa Pwani na Taifa kwa ujumla.
Katika ziara hiyo, Rais Magufuli amezindua viwanda vitano ambavyo ni viwanda vya vifungashia, kiwanda cha Matrekta, kiwanda cha chuma, kiwanda cha kukausha matunda na kiwanda cha vinywaji baridi cha Sayona.

Uzinduzi wa viwanda hivyo ni muendelezo wa kutekeleza ahadi yake aliyoitoa wakati wa uchaguzi mkuu 2015 wa kuhakikisha Tanzania inakuwa Tanzania ya viwanda. Viwanda hivyo vitasaidia kuondoa tatizo la ajira nchini na pia vitasaidia kupunguza bei za bidhaa husika kwenye soko la kibiashara.

Wawekezaji hao walilalamika juu ya urasimu wakati wa mchakato wa kuanzisha viwanda ambapo Rais Magufuli alitumia ziara hiyo kuagiza urasimu huo ukomeshwe na kuagiza baadhi ya malipo wakati wa kusajilii kiwanda kufutwa ili kuvutia wawekezaji zaidi nchini.

Serikali ya awamu ya 5 ya Dk. Magufuli ambayo ina miaka 2 tangu iingie madarakani imefanikiwa kupata viwanda 393 ndani ya mkoa wa Pwani ambavyo kati ya hivyo viwanda 85 ni viwanda vikubwa. Hakika Tanzania ya viwanda inawezekana

Rais Magufuli huyo huyo amefanya ziara ya kushtukiza katika kiwanda cha kutengeneza dawa za kuulia vimelea vya mbu wanaosababisha malaria kilichopo Kibaha, Pwani ambapo Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Fedha kutoa Sh1.3 bilioni  kwa ajili ya kulipia lita 100 ya dawa  hizo za kuua vimelea vya mbu zilizopo katika kiwanda hicho.

Wizara inatumia gharama kubwa kununua madawa ya kutibu nje ya nchi na kuacha dawa inayozuia maleria ikikosa mnunuzi hapa nchini. Nina uhakika uamuzi huu wa Rais utasaidia kupunguza kuenea kwa ugonjwa wa Maleria hapa nchini.

Katika ziara hiyo, Rais Magufuli amezindua Barabara ya Bagamoyo - Msata ambayo imejengwa kwa fedha zetu wenyewe na walioijenga ni wakandarasi wazawa. Barabara hiyo itasaidia kupunguza foleni ya Barabara ya Dar Kibaha, itaongeza uchaguzi wa njia ya kutoka na kuingia mkoa wa Dar, utasaidia kusafirisha watu na mizigo yao yakiwemo mazao kutoka mashambani na kuyafikisha masokoni kwa gharama ndogo. Hakika Barabara hii ina tija kubwa kwa maendeleo ya Taifa.

Ziara hiyo ya Rais Magufuli imezindua mradi mkubwa wa maji wa Ruvu ambapo utasaidia kuondoa tatizo la maji kwenye mkoa wa Pwani na Mkoa wa Dar es Salaam. Hakika ziara hii imejaa tija.

Katika mkutano wa hadhara wa mwisho wa kuhitimisha ziara yake, Rais John Magufuli amewapa wakazi wa Bagamoyo, eneo la Magereza lenye ukubwa wa heka 65. Alichukua hatua hiyo baada ya wanawake waliokuwa wamebeba mabango, kumtaka awape eneo lao kwa kuwa ni wazaliwa wa Bagamoyo, ni wajane na wana uhaba wa maeneo ya biashara. Amelitaka Jeshi la Magereza kufanya mabadiliko katika hati ili eneo hilo liwe la wananchi.

Pengine bila ya ziara ya Rais Magufuli ni dhahiri wakazi hao wangeendelea kupata mateso yasiyo na kuwasaidia.

Hakika ziara hii ya Rais Magufuli mkoa wa Pwani imejaa tija sana kwa wakazi wa mkoa wa Pwani na Taifa kwa ujumla. Ni wakati sasa wa viongozi ngazi za chini nao kuamua kutoka maofisini na kufanya ziara ili kujua na kujionea matatizo ya Wananchi ili wajue namna gani ya kuwasaidia kuondoa kero zao. JPM ameanzisha mwendo, viongozi wengineo wa ngazi za chini waige mfano huu bora wa JPM kwa jamii.

Emmanuel John Shilatu
0767488622
22/06/2017

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.