NA HAJI NASSOR, PEMBA
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Mhe: Dk Ali Mohamed Shein, amesema baada kuitangaza Ilani
ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, lazima sasa kuhama ofisini na kwenda kwa
wananchi, kuona utekelezaji wake ulipofikia.
Dk
Shein, ameeleza hayo ukumbi wa chuo cha SUZA Mchanga mdogo wilaya ya Wete
kisiwani Pemba, wakati akuzungumza na wananchi, viongozi wa chama na serikali,
mara baada ya kupokea taarifa ya kikazi ya Mkoa wa kaskazini Pemba.
Alisema,
huu sio wakati tena wa kuganda ofisini ni lazima kuziacha kwa muda, na kwenda
kwa wananchi waliomchagua, ili kuangalia kile alichokiahidi juu ya utekelezaji
wake.
Alisema
kukaa ofisini kwa muda mrefu, hakuwasaidii wananchi na wala hakuna ushuhuda wa
kile kilichofanyika, hivyo ni lazima kuwatembelea.
Alieleza
kuwa, ndio maana kwenye ripoti hiyo ya Mkoa, hataki kusema chochote, hadi hapo
atakapoisoma na kutembelea maeneo husika, kuona utekelezaji wake.
“Mimi nimeshaipokea ripoti, na kwa vile nipo Pemba mwenyewe ntakwenda kuona haya
yaliomo kwenye taarifa, maana sasa lazima sisi viongozi tuhame ofisini na
twende moja kwa moja kwa wananchi kujiridhisha”,alifafanua.
Akizungumzia
kuhusu ripoti hiyo, rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
aliupongeza mkoa huo kwa taarifa nzuri na ilioshiba.
Alisema
ijapokuwa hajaisoma yote ripoti hiyo, lakini kutokana na uwasilishwaji wake na
alivyopokea taarifa, imeandaliwa vya kutosha na ina utekelezaji ndani yake.
“Taarifa
yenu ya kikazi kwa kweli imeshiba na imebeba utendaji wa kazi wa kila idara,
lakini leo sisemi kitu hadi nikimaliza ziara yangu, nasubiri kwenye majumuisho
ntasema na kuuliza”,alisema Dk Shein.
Katika
hatua nyengine, rais huyo wa Zanzibar, amewapongeza wananchi, viongozi wa chama
na serikali kwa kuhudhuria kwenye uwasilishaji wa taarifa hiyo, na kusema hapo
ndio watapata taarifa sahihi.
“Mimi
nashangaa kuona baadhi ya mawaziri, makatibu wakuu na viongozi wengine
hawashiriki ziara kama hizi ambazo ni za kiutendaji, na wala sio za
kujifurahisha”,alifafanua.
Aliongeza
kuwa, yeye baada ya kuchaguliwa na wananchi aliamua kuwachagua wasaidizi wake,
sio kwa kujuana wala kuangalia sura bali, ni kwa kumsaidia hivyo kama kwenye
ziara hiyo hawashiriki anashindwa kuwafahamu.
“Kiongozi
wa chama kwenye utekelezaji wa Ilani hii ya CCM ya mwaka 2015/2020 ana nafasi
yake na halikadhalika sisi viongozi wa serikali kama mawaziri tunawajibu wetu
mkubwa, lazima tuwepo”,alifafanua.
Akiwasilisha
taarifa hiyo ya kikazi, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mhe: Omar Khamis
Othman alisema maendeleo makubwa yameshapatikana ndani ya Mkoa huo, ikiwa ni
pamoja na maji safi na salama.
Hata
hivyo Mkuu huyo wa Mkoa, alimueleza rais huyo wa Zanzibar kuwa, changamoto
kubwa inayowakabili katika kuzimaliza kesi za udhalilishaji ni wananchi
kutokuwa tayari kutoa ushahidi mahakamani.
“Tumefanikuwa
kuunda kamati za mkoa na wilaya juu ya kupinga udhalilishaji, lakini sasa
wananchi bado baadhi yao wamekuwa wasugu kushirikiana na vyombo vya
kisheria”,alilalmikia.
Aidha
alifafanua kuwa, ushirikiano mkubwa uliopo baina ya wananchi na kamati ya
ulinzi na usalama August 20, mwaka huu, walikamata kete 560 zinazodhaniwa kuwa
dawa za kulevya.
Wakati
huo huo, Rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe: dk Ali
Mohamed Shein, mara baada ya kuweka jiwe la msingi skuli Chimba wilaya ya
Micheweni aliwapongea wananchi hao kwa uamuzi huo wa kujenga skuli kwa nguvu zao
Alisema
uamuzi wa kujiletea maendeleo ndio unaofaa kuungwa mkono na kuigwa na kila
mmoja, kwani maendeleo hasa ya sekta ya elimu inategemea pia nguvu za wananchi.
“Mimi
niwapongeze wananchi wa Shehia ya Chimba kwa uamuzi sahihi na adhimu wa
kuwajengea watoto wenu skuli ya karibu na sasa masafa ya kilomita sita
yatawaondoka”,alieleza.
Hata
hivyo Rais huyo wa Zanzibar amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa kaskazini Pemba,
kuzipitia skuli zote za mkoa huo, na iwapo atabaini kuna waalimu watoro atoe
taarifa kwa waziri wa elimu ili wafukuzwe kazi.
“Wapo
waalimu kwanza ni watoro skuli na hujifanya wanaumwa, lakini hawaendi hospitali
na hujikalia nyumbani na wanakula mshahara, waripoti na kisha wafukuzwe
kazi”,alifafanua.
Akisoma
risala ya ujenzi huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Micheweni Hamad
Mbwana Shehe alisema, ujenzi huo wa madarasa matano na ofisi mbili za waalimu,
umeshagharimu shilingi million 37.35.
Alisema
kati ya fedha hizo shilingi 600,000 ni nguvu za wananchi, shilingi 900,000 ni
mchango wa Jumuia ya Maendeleo Tumbe, shilingi 3,500,000 kutoka Halmashauri,
wakati mfuko wa jimbo wa mwakilishi na mbunge jimbo la Tumbe umechangia zaidi
ya shilingi 31.4 milioni
Aidha
amesema kwa sasa wanahitaji zaidi ya shilingi million 17, 534,000 kwa ajili ya
milango, madirisha, rangi, dari na vyoo, ili wanafunzi waanze kuitumia.
Rais
huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pamoja na ujumbe wake,
utaendelea na ziara yake ya siku tano asubuhi wilaya ya Wete kwa kukagua
shughuli mbali mbali za kimaendeleo ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa kituo cha
afya cha mama na mtoto cha Junguni.
No comments:
Post a Comment