Habari za Punde

WAZIRI MBARAWA ATOA MAAGIZO MAZITO KWA TANROAD KUSIMAMIA UJENZI WA DARAJA LA MLALAKUWA JIJINI DAR ES SALAAM

Na Ismail Ngayonga,Maelezo Dar es Slaam. 
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ameiagiza Wakala wa Barabara Nchini (TANROAD) kusimamia viwango, muda na gharama inayolingana na thamani ya mradi kwa Kampuni ya Milembe KIKA JV inayojenga Daraja la Mlakakuwa lililopo Barababa ya Mwai Kibaki Jijini Dar es Salaam.

Waziri Mbarawa aliyasema hayo leo Jumanne (Septemba 26, 2017) Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya mradi ujenzi wa Daraja hilo ambao ni sehemu ya upanuzi wa barabara ya Mwai Kibaki yenye urefu wa Kilometa 5.3 inayopanuliwa kutoka njia mbili za sasa hadi njia nne.
Profesa Mbarawa alisema malengo ya Serikali ni kuhakikisha kuwa Daraja hilo linakuwa imara na kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kipindi kirefu zaidi, hivyo ni wajibu wa TANROAD kuhakikisha kuwa Mkandarasi wa ujenzi wa mradi huo anaikamilisha kazi hiyo kwa kwa wakati kwa mujibu wa mkataba.
“Malengo yetu ni kuhakikisha hadi kufikia mwezi Desemba mwaka huu upande mmoja wa njia mbili unafuguliwa mradi huo unaopaswa kukamilika katika kipindi cha miezi 24 kulingana na Mkataba tuliosaini na Watanzania wanasubiri kwa hamu kukamilika kwa mradi huu kwa kuwa utapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la msongamano”
Waziri Mbarawa anasema hadi sasa Serikali imeshatoa kiasi cha Tsh. Bilioni 1.1 kati ya Tsh. Bilioni 4.8 zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ambao hadi sasa umefikisha asilimia 20 ya kukamilika kwake na hivyo aliigiza TANROAD kuhakikisha kuwa Mkandarasi wa mradi anaikamailisha kazi hiyo kwa wakati.
Alisema Serikali ina imani kubwa na Mkandarasi wa Mradi huo Kampuni ya Milembe Kika JV kuwa itafanya kazi hiyo kwa uzalendo mkubwa kwani kufanikiwa kwao katika kutekeleza mradi huo kutawawezesha kupata zabuni nyingine za kazi kutoka Taasisi mbalimbali za Umma.
Kwa upande wake Mhandisi Miradi wa TANROAD Mkoa wa Dar es Salaam, Julius Ngusa alisema mradi huo ulianza Oktoba mwaka 2016 na unatarajia kukamilika Oktoba 2018, ambapo mpaka kufikia Mwezi Agosti 2017 Mkandarasi amekamilisha ujenzi wa nguzo 56 za awamu ya kwanza.
Aliongeza Daraja hilo litakuwa na njia mbili za magari na njia ya waenda kwa miguu na baiskeli pamoja na daraja la Mabasi yaendayo haraka (BRT) litakalojengwa katikati ya madaraja yatakayojengwa.
Kwa mujibu wa Ngusa alisema awali mradi huo ulikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mvua zilizonyesha kuanzia Mwezi Machi  hadi Juni mwaka huu, ambapo hata hivyo katika kufidia muda uliopotea Mkandarasi huyo amekuwa akifanya kazi kwa kipindi cha masaa 24 kila siku kabla ya kuanza kwa mvua za Mwezi Desemba.
Naye Mkandarasi wa Kampini ya Milembe KIKA JV, Epharaim Kakubanga alisema kampuni hiyo imejipanga kikamilifu kutekeleza mradi huo kwa mujibu wa mkataba walioafikiana baina yao na Serikali ikiwemo kuzingatia muda, ubora na kiwango cha ujenzi wa mradi wa Daraja hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.