Habari za Punde

CCM Wete wachaguana


 NA HAJI NASSOR, PEMBA
MKUTANO mkuu wa uchaguzi wa CCM wilaya ya Wete kisiwani Pemba, umemrejesha tena madarakani Kombo Hamad Yussuf, kuwa Mwenyekiti wa chama hicho wilayani humo, baada ya kupata kura 134, dhidi ya mpinzani wake Ali Bakari Ali, aliejikuta na kura 128, ambazo hazikukumuwezesha kushika nafasi hiyo.
Mkutano huo pia, uliwachagua Rashid Hadid Rashid aliepata kura 185, Zulfa Abdalla Said kura 129 na Asaa Ali Salim aliejinyakulia kura 123 kuwa wajumbe wa Mkutano mkuu wa CCM taifa, baada ya kuwashinda wenzao kwenye kinyang’anyiro hicho.
Aidha mkutano huo mkuu wa uchaguzi uliofunguliwa na Makamu wa pili wa rais Zanzibar Mhe: Balozi Seif Ali Idd, uliwachagua Raya Mkoko Hassan aliepata kura 143 na Khamis Issa Khamis kwa kura 115, kuwa wajumbe wa Mkutano mkuu wa CCM Mkoa wa kaskazini Pemba.
Wajumbe wengine 10 waliochaguliwa kwa ajili ya kuingia kwenye Halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Wete ni pamoja na Hamad Ahmed Baucha, Omar Ali Omar, Khamis Dadi Khamis, Khamis Juma Silima.
Wengine ni Haji Hamad Bakar, Ali Hamad Khamis, Halima Shaame Hamad, Ali Juma Kombo, Ali Mgau Kombo na Salum Said Khamis.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo, Mwenyekiti mpya wa wilaya ya Wete Kombo Hamad Yussuf, aliwataka wajumbe wa mkutano huo na wanaccm wengine kuhakikisha wanashirikiana katika kukijenga chama chao.
“Uchaguzi umeshamalizika, sasa tuwe pamoja kukijenga chama chetu, ili wengine wavutike kujiunga na waliopo wasitamani kutoka”,alieleza.
Mapema akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu, Mjumbe wa Halmashauri Kuuu wa CCM taifa Asia Sharif Omar, alisema sasa makundi basi baada ya kumalizika kwa uchaguzi.
Alisema makundi hayana msingi ndani ya CCM maana yakiendelezwa hadi yakikutana na uchaguzi mkuu ujao wa vyama vingi mwaka 2020, ni hasara kwao na chama chao.
Alieleza kuwa uchaguzi huo ulikuwa baina ya wanaccm wenyewe kwa wenyewe, hivyo hakuna sababu wala haki ya kuendeleza makundi, maana haukushirikisha vyama vyama vyengine.
“Mimi ninanchoamini uchaguzi umekamilika na sote sisi CCM ni washindi, illa viongozi wetu tumeshawapa sasa tushirikiane kuhakikisha tunakirejesha tena Ikulu chama chetu kwa shangwe kwa kila uchaguzi unapofanyika ”,alifafanua.
Katika hatua nyengine Mjumbe huyo wa Halmashauri kuu ya CCM, aliwataka viongozi waliochaguliwa kujipanga upya ili kuhakikisha wanaongeza idadi ya wanachama.
Alisema dhamira ya CCM ni kuhakikisha kinaendelea kushika hatamu za uongozi na kuwaongoza wananchi wote kwa lengo la kuwaletea maendeleo bila ya ubaguzi.

Awali Mkutano huo mkuu wa CCM wa uchaguzi wilaya ya Wete ulifunguliwa na Makamu wa pili wa rais wa Zanzibar Mhe: Balozi Seif Ali Idd, ambae aliwataka wanaccm kuchagua viongozi imara, wenye nia ya kukijenga chama na wanachama wake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.