NEC-DODOMA
16.10.2017
Tume ya Taifa ya uchaguzi
imesema kuwa Wapiga kura waliopoteza vitambulisho vya kupigia kura watapata
fursa ya kupiga kura kwenye uchaguzi mdogo wa Madiwani wa Kata 43 unaotarajiwa
kufanyika Novemba 26, mwaka huu.
Hayo yamesemwa leo
(16.10.2017) na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Bw.
Ramadhani Kailima Mjini Dodoma ikiwa ni siku ya pili ya mafunzo ya siku tatu
kwa wasimamizi na wasimamizi wasiadizi wa uchaguzi yanayoratibiwa na kuendeshwa
na NEC.
Bw. Kailima amesema wapiga
kura hao wataruhusiwa kutumia vitambulisho vya uraia vinavyotolewa na Mamlaka
ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Hati ya kusafiria na Leseni ya udereva.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi
kwa kuzingatia kifungu namba 62 (a) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa, ambacho kinasema mpiga kura aliyeandikishwa kwenye daftari atakwenda
mwenyewe kwenye Kata aliyojiandikisha na kituo alichopangiwa” Amesema.
Ameeleza kuwa hatua hiyo
ni kumridhisha msimamizi wa kituo au msimamizi msaidizi wa uchaguzi kwamba yeye
ndiye mpiga kura halali na kuongeza kuwa kifungu hicho kinamtakaMpiga Kura
aonyeshekadi yake ya kupigia. Aidha, kinaeleza kwambaTume inaweza ikaelekeza
utambulisho mwingine wowote utakao msaidia mpiga kura kuweza kupiga kura iwapo hana kadi.
Bw.Kailima amesema kuwaTume
ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuzingatia kifungu hicho, katika uchaguzi mdogo utakaofanyika
Novemba 26, 2017 imetoa maelekezo kwa Wasimamizi wa Uchaguzi kuruhusu wapiga
Kura waliojiandikisha kwenye Dafatari la kudumu la Wapiga Kura kutumia Hati ya
kusafiria, kitambulisho cha Taifa kilichotolewa na NIDA na leseni ya udereva.
Bw. Kailima amesemaruhusa
hiyo imetolewa kwa sharti moja kwamba majina na herifu yaliyopo kwenye
kitambulisho hicho yafanane na majina na herufi zilizopo kwenye Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura.
Ameongeza kuwa NEC
itakutana na vyama vya siasa hivi karibuni kuwajulisha juu ya maagizo hayo na
kusisitiza kwamba tofauti yoyote itakayo kuwepo kwenye majina itamnyima mpiga
kura fursa ya kupiga kura.
Bw. Kailima amesema maamuzi
hayo yamefikiwa kutokana na kuwepo kwa changamoto kubwa kwenye daftari la
kudumu la wapiga kura ambalo kwa mara ya mwisho liliboreshwa mwaka 2015.
“ Katika kipindi chote
hichi (2015-2017) inawezekana kwa namna moja ama nyingine, kuna baadhi ya
wapiga kura wamepoteza kadi zao za kupigia kura na kwa sababu hatujaboresha na
sheria inasema watapata hizo kadi baada ya daftari kuboreshwa, wanaweza
wakakosa fursa ya kupiga kura kwenye uchaguzi wa madiwani wa kata 43, lakini
wengine kadi zao zimeharibika kiasi kwamba haziwezi kusomeka, na wengine kadi
zao zimechakaa kabisa kwa sababu moja ama nyingine kutokana na mazingira
yaliyopo,” amesema.
Wakitoa maoni yao juu ya
agizo hilo la NEC, washiriki wa mafunzo hayo wamepongeza hatua hiyo na kusema
kwamba itakuza wigo wa demokrasia nchini kwa kuwapa fursa wapiga kura halali
ambao kwa sababu zilizoko nje ya uwezo wao wamejikuta hawana kadi za kupigia kura
licha ya kwamba ni wapiga kura halali waliojiandikisha.
Bw. Abdul Kasembe ambaye
ni Afisa Uchaguzi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Mkoani Ruvuma
amesema kuwa amefurahishwa na uamuzi huo akieleza mambo mengi yamejitokeza kati
ya mwaka 2015 mpaka sasa.
“Sisi tumefurahia agizo
hili kwa kuwa litawapa fursa wananchi ambao pengine wangeikosa fursa kwa kuwa
hawana kadi japokuwa wamejiandikisha”.
Bi. MargaretNakayinga,
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Mkoani Tabora amesema
agizo hilo limeleta fursa kwa watu ambao pengine wangekosa fursa ya kupiga kura
kwa kupoteza kadi ya kupigia kura au kwa kuharibika kwa kadi zao. Tutakaporudi
huko tutawatangazia wananchi ili wajitokeze kwa wingi kupiga kura..”.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Mkoani Tanga, Bw. Kazimbaya
Makwega amesema kuwa agizo hilo ni muafaka na limezingatia mazingira ya
Kitanzania kwa kuwa watu wanaweza kupoteza kadi au kuharibikiwa na kadi zao na
kukosa fursa ya kupiga kura.
No comments:
Post a Comment