Habari za Punde

Oman yatoa fursa kwa waandishi habari wa Zanzibar kujifunza habari za mafuta, gesi

Na.Haji. Nassor - Pemba.
WIZARA ya Mafuta na Gesi ya Oman, imesema iko tayari kuwapokea watendaji mbali mbali wakiwemo waandishi wa habari wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kwenda nchini humo, kujifunza jinsi nchi hiyo, ilivyofanya kwenye utafutaji na uchimbaji wa rasilimali hiyo.

Kauli hiyi imetolewa na waziri wa wizara hiyo, Mohammed Bin – Hamel Al Ruhim wakati alipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya kumaliza ziara yake ya kutwa moja kisiwani Pemba.

Alisema tayari ameshafanya mazungumzo na waziri wa  wizara ya Habari ya Zanzibar juu ya azma, kwa watendaji wake wakiwemo waandishi kupewa taaluma ya utafutaji na uchimbaji wa gesi, ili wawe wajuzi wa kuwafahamisha kupitia vyombo vya habari.

Alisema ingawa utafutaji na uchimbaji wa mafuta, taaluma yake inatofautiana kutoka sehemu moja na nyengine, lakini kama waandishi wa habari na watendaji wengine wa wizara ya Habari hapa Zanzibar, wakikubaliana watakwenda nchini Oman kujifunza.

“Niwaambie waandishi wa habari, hata juzi nimeshafanya mazungumzo na waziri wenu wa habari, juu ya jambo hili la waandishi kupatiwa taaluma nchini Oman, sasa wacha tuone maana sisi tunachimba mafuta nchi kavu na huwenda kwa Zanzibar mkayatafuta baharini”,alisema.

Akizungumzia kuhusu harakati hizo za uchimbaji wa mafuta wa gesi alisema, Oman imekuwa ikizungumza na makampuni kadhaa juu ya hilo kwa Zanzibar.

Alisema ijapokuwa makampuni hayo yamekuwa yakiwaeleza kwenda visiwa Zanzibar kwa ajili ya utafiti huo, lakini hawana taarifa za wapi wamefikia.

“Tunasoma sana kwenye vyombo vya habari kama magazeti, lakini hawajatueleza kitu hasa wamefanya juu ya utafutaji wa uchimbaji wa mafuta na gesi kwa Zanzibar, na hata Tanzania yote”,alisema.

Kuhusu sekta ya utalii, alisema amevutiwa na ukarimu na bashasha ya wananchi wa Zanzibar, maana hilo ni sehemu ya kuvutio cha watalii, jambo ambalo nchi nyengine hakuna.

Alisema kutokana na hali ya amani na utulivu alioushuhudia kisiwani Pemba, anajipanga ili kuhakikisha anarudi tena kisiwani humo, ili atembee zaidi.

Mapema Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mwanajuma Majid Abdalla, aliushukuru ujumbe huyo wa serikali ya Oman ukiongozwa na waziri wake wa Mafuta na Gesi.

Alisema ujio wao kisiwani Pemba, ni ishara ya kuendeleza udugu wa kweli uliopo miongoni mwa nchi hizo, ambao uliasisiwa na viongozi wa nchi mbili hizo.

Waziri huyo wa mafuta akiambatana na balozi mdogo wa Oman nchini, waziri wa habari, wakiwa na mwenyeji wao Mkuu wa Mkoa wa kusini Pemba, ulitembelea hospitali ya Abdulla mzee, Skuli ya Uweleni, bandarini Mkoani, kiwanda cha makonyo na msitu wa hifadhi wa Ngezi wilaya ya Micheweni

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.