Habari za Punde

Taarifa ya Umoja wa Vijana wa CCM Kwa Wote Walioomba Kuteuliwa Kugombea Nafasi za Uongozi Ngazi ya Mikoa na Taifa.

Kwa Wana Jumuiya wote hususan wale wote walioomba kuteuliwa kugombea nafasi mbali mbali za uongozi kwenye UVCCM ngazi ya Mikoa na Taifa. Kila mmoja anapaswa kuusoma, kujilinda, kuzingatia, kuufahamu na kuuelewa ujumbe huu muhimu.

Zipo taarifa za uhakika zenye vielelezo vyenye ushahidi kuwa baadhi ya walioomba nafasi za kuteuliwa kugombea ndani ya UVCCM, wameanza kuitisha vikao vya mizengwe na kufanya kampeni za chini kwa chini kinyume na Kanuni, Taratibu  na mwenendo wetu wa Uchaguzi.

Ukusanyaji wajumbe kwa maana ya wapiga kura katika eneo ambalo si halali kikanuni na kiutaratibu linatoa tafsiri na kujenga  mazingira ya rushwa pia ukiukaji na uvunjaji wa kanuni  za Uchaguzi za Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi.  

Ifahamike kuwa uchaguzi huongozwa na Katiba, Kanuni, Taratibu, miongozo na maadili halali hivyo kila mgombea anapaswa kuheshimu taratibu hizo, sambamba na kuheshimu miiko ya uchaguzi. 

Hadi sasa hakuna mwombaji wa nafasi yoyote aidha wa nafasi ya Mkoa au Taifa aliyeteuliwa jina lake na kuwa mgombea halali. Mamlaka za uteuzi kwa mujibu wa Katiba, Kanuni hazijatangaza majina ya wagombea walioteuliwa kutoka miongoni mwa waomba nafasi waliojaza fomu ndani ya UVCCM.

Ni kosa na marufuku Kikanuni na Kikatiba kwa muomba nafasi yeyote kuanza kupitapita Wilayani, Mikoani, mitaani, vichochoroni, kuitisha vikao haramu vya kampeni , kujinadi na kujieleza kabla ya ukamilishaji wa mchakato wa uteuzi na majina  kutangazwa.

Vitendo vyovyote vitakavyofanywa namuombaji wa nafasi aidha kwa kujinadi kwa kuitisha vikao haramu,  kujielezea, kutaja malengo au kuwashawishi wapiga  kura kwa njia ambayo si ya kidemokrasia ni kinyume na taratibu. Ushahidi ukipatikana na  kuthibitika kunaweza kukuondolea sifa ya kuteuliwa katika nafasi uliyoomba.

Tunaendelea kukumbusha kuwa hatutasita kumchukulia hatua za kimaadili mpambe wa muomba nafasi yoyote atakayebainika anakwenda kinyume na maelekezo haya pamoja na matakwa ya Katiba ya Chama Chama Mapinduzi na Kanuni za UVCCM.

Hata baada ya vikao vya uteuzi kukamilika mwongozo utatolewa kwa ngazi ya Mkoa hadi Taifa namna ya kufanikisha chaguzi hizo.

Chama Cha Mapinduzi ni baba na kinara wa demokrasia Tanzania, Afrika Mashariki na Dunia kwa ujumla, chaguzi hizi zinazoendelea ndani ya Chama na Jumuiya zake ni kielelezo tosha cha ukomavu wa demokrasia na kioo kinachoakisi heshima ya Chama na Jumuiya ndani na nje hasa katika kusimamia mambo yake ya msingi ya Kikatiba na Kikanuni.

Naendelea kuwakumbusha Vijana wote kuendelea kuishi katika maneno ya Usia ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk. John Pombe Joseph Magufuli aliyowahi kutuasa wakati chaguzi hizi zikiendelea nanukuu

Natambua mnaendelea na Uchaguzi ni lazima kuheshimu Katiba ya Chama chetu na Kanuni zetu katika mchakato wa kuwapata Viongozi tutakaowapa dhamana. Vijana lazima wachague Viongozi wazuri, wazalendo, waadilifu, wachapa kazi watakaolinda maslahi ya CCM na UVCCM  na si maslahi binafsi kataeni na kupiga vita rushwa kwa nguvu zote na watakaobainika kutoa au kupokea rushwa hatua za haraka zichukuliwe”; Dk. John Pombe Joseph Magufuli.

Nachukua nafasi hii kwa sauti ya juu kabisa kuwaonya, kuwaasa, kuwakanya na kuwazuia wale wote ambao aidha wanafanya kwa makusudi au kujisahau waelewe kuwa Kanuni ya Uchaguzi iko pale pale na itatenda haki kama msumeno. Vile vile watambue kuwa tunawamulika na kuwafuatilia nyendo zao zote na ikibainika, taarifa zao zitawasilishwa katika vikao kwa hatua zaidi za Kimaadili.

Ahsanteni 

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Shaka Hamdu Shaka (MNEC)
KAIMU KATIBU MKUU

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.