Habari za Punde

Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Yaadhimishwa Kisiwani Pemba.

Balozi Seif akizindua Kitabu cha Mkakati wa Awamu ya Tatu wa mapambano dhidi ya Ukimwi Zanzibar mwenye Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani.
Mwakilishi wa Jumuiya ya Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Zanziubar { ZAPHA + } Bibi Sharifa Shaaban akitoa taarifa ya Jumuiya hiyo kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani zilizofanyika Gombani Chake chake Pemba.
Mwakilishi wa Taasisi za Umoja wa Mataifa Nchini Bibi Marie akitoa salamu za Taasisi za Umoja huo kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani zilizofanyika Gombani Chake chake Pemba.
Balozi Seif akimpongeza Mtoto Farhat Abdulla anayeishi na Virusi vya Ukimwi baada ya kutoa ushuhuda wa maisha yake na mtazamo wa Jamii  iliyomzunguuka kutokana na mazingira ya Afya yake kwa takriban Miaka 11 sasa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akihutubia Wananchi katika Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani zilizofanyika Kitaifa Uwanja wa Gombani Kisiwani Pemba. Kulia ya Balozi Seif ni Naibu Waziri Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma Nhunga na kushoto ya Balozi

Seif ni Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Mh. Mwanajuma Majid.

Baadhi ya Wanafunzi wa Skuli tofauti Kisiwani Pemba walioshiriki na kushuhudia Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi. 
Mwakilishi wa Taasisi za Umoja wa Mataifa Nchini Bibi Marie akiagana na Balozi Seif mara baada ya kumalizika kwa Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani zilizofanyika Gombani Chake

chake Pemba. Aliyesimama kati kati yao ni Mwenyekiti wa Tume ya Ukimwi Zanzibar Dr.

Salhia Ali Muhsin. Picha na – OMPR – ZNZ.



Na. Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Jamii ina wajibu wa kulilinda dhidi ya maambukizi  mapya ya Virusi vya Ukimwi Kundi kubwa la Vijana linaloanzia miaka 10 hadi 24 katika njia za Kitaalamu  bila ya kusahau mazingatio ya mila na desturi za Jamii.


Alisema tafiti zimethibitisha wazi kwamba kundi hilo ndilo linalokumbwa  na kuathirika zaidi na maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi licha ya juhudi kubwa zinayochukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo katika kudhibiti maradhi hayo thakili.


Akizungumza katika maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Ukimwi Duniani yaliyoyanyika Kitaifa katika Uwanja wa Gombani Chake Chake Kisiwani Pemba Balozi Seif alisema tatizo kubwa linalokwamisha juhudi za kumaliza Ukimwi ni tabia ya Watu wengi kuogopa kupima Afya zao kama wako salama au wameshaambukizwa na maradhi.


Balozi Seif  alisema utaratibu wa upimaji wa afya ndio utakaolifikisha Taifa kwenye shabaha ya Tisini Tatu  { 90 ,90, 90 } ifikapo Mwaka 2020 ikimaanisha asilimia 90% ya walioambukizwa Virusi wanajitambua, asilimia 90% ya waliojitambua wanaanza matibabu na asilimia 90% wanaopata Tiba waweze kupunguza wingi wa Virusi ndani ya damu zao.


Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba  kiwango cha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi Zanzibar kimefikia asilimia 0.4% ikimaanisha kwamba asilimia hiyo ya Wazanzibari wenye umri wa Miaka 15

hadi 49 wanaishi na Virusi vya Ukimwi.


Alisema kufuatia utafiti uliofanywa hivi karibuni kuangalia viashiria vya maambukizo ya Virusi vya Ukimwi kiwango hicho kinatofautiana baina ya Visiwa vya Zanzibar ambapo Mkoa wa Kaskazini  unaongoza kwa asilimia 0.8% kwa Kisiwa cha Unguja wakati Pemba unaongoza Mkoa wa Kusini kwa asilimia 0.4% .


Balozi Seif alifahamisha kwamba jitihada za mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi zinatoa matumaini  makubwa Nchini  tokea kubainika kwa maradhi hayo takriban miaka 31iliyopita, lakini bado mkazo zaidi uongezwe katika kufikia lengo la kumaliza maradhi ya Ukimwi ifikapo Mwaka 2030.


“Takwimu zinaonyesha kwamba kwa kipindi chote hicho kiwango cha watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi kipo chini ya asilimia Moja ikiwa ni mafanikio kwa kiasi fulani licha ya  jitihada kubwa zinahitajika ili kufikia lengo ”. Alisema Balozi Seif.


Alieleza kwamba Serikali Kuu inaendelea kufanya juhudi za kupatikana kwa huduma za Afya sambamba na kuziondoa changamoto zinazojitokeza ambazo husababisha  kuviza juhudi hizo.


Alisema Kauli Mbiu ya Mwaka huu ya Siku ya Ukimwi Duniani inayoeleza “Haki ya Afya ” inatoa msukumo na msisitizo kwa Nchi zote Duniani ikiwemo Tanzania haja ya Watu wote, bila ya kujali hali zao, hadhi zao

pamoja na umaarufu wao kupatiwa huduma za kiwango cha juu ili waweze kuwa na afya ya Kiakili na Kimwili.


Akigusia changamoto ya muda mrefu wa upatikanaji wa Vipimo  vya kuangalia kiwango cha virusi mwilini { ViralLoad } pamoja na Vipimo vya kujua maambukizo kwa Mtoto aliyezaliwa na Mama mwenye Virusi

Balozi Seif alisema kwamba Mashine ya  kupimia vipimo hivyo tayari imeshapatikana.


Alisema kupatikana kwa Mashine hiyo inayotarajiwa kuanza kazi hivi karibuni kutawezesha vipimo vyote kufanywa Zanzibar badala ya kusafirisha  sampuli kupeleka Mjini Dar es salaam. Balozi Seif alifahamisha kwamba uliobaki ni wajibu wa watoaji huduma kufanya kazi zao kwa mujibu wa utaalamu waliofundishwa na kutoa huduma

hizo kwa kujali utu na heshima ya wanaowahudumia.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliziagiza Mamlaka za Mikoa, Wilaya na Taasisi husika ziwajibike kudhibiti tabia hatarishi katika maeneo yao na kuzisimamia kikamilifu sheria na kanuni zilizopo. Balozi Seif alisisitiza zaidi kwamba juhudi za pamoja zielekezwe pia katika kupunguza  maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi mwaka hadi

mwaka  katika mipango ya kuumaliza kabisa ugonjwa wa Ukimwi.


Amezishukuru na kuzipongeza Taasisi zote za kiraia na jumuiya za Kidini  kwa mchango wao mkubwa zilizotoa katika kusaidia nguvu za mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatoa shukrani za pekee kwa washirika wa Maendeleo ambao wameamua kuisaidia Zanzibar kwa hali na mali katika kuimarisha muitiko

wa Taifa wa Ukimwi.


Alisema misaada ya washirika hao imechangia kuiweka Zanzibar  katika kiwango cha Maambukizi kisichozidi asilimia Moja hadi hivi sasa .


Akitoa salamu za Mashirika ya Umoja wa Mataifa Mwakilishi wa Taasisi za Umoja huo Nchini Bibi Marie alisema dhamira ya Umoja huo kupitia Taasisi zake ni kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika Mkakati wa Awamu ya Tatu wa mapambano dhidi ya Ukimwi.


Bibi Marie alisema Jamii imetoka katika hali ya kukata tamaa na hivi sasa imekuwa na matumaini katika mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi licha ya baadhi ya wakati kukosekana kwa haki sawa ya huduma za Afya.


Alisema juhudi za ziada zinapaswa kuchukuliwa na pande zote husika katika kuendeleza matumaini yaliyojichomoza ndani ya mchakato wa mapambano hayo ambapo kwa sasa Ukimwi umekuwa sio tishio tena kama ilivyokuwa ikionekana mwanzoni mwa kuibuka kwa maradhi hayo.


Mapema akitoa Taarifa ya Siku ya Ukimwi Duniani Mwakilishi wa Jumuiya ya Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Zanzibar { ZAPHA + } Bibi Sharifa Shaaban  alisema Katioba ya Zanzibar ya Mwaka 1984  imeweka wazi jinsi Serikali inavyotakiwa kuwajibika  kusimamia suala la huduma za Afya kwa Watu wake.

Bibi Sharifa alisema aliikumbushusha Jamii kujiepusha na unyanyapaji unaoonekana katika baadhi ya Familia kwa vile haitoi sura nzuri kwa waathirika wa Virusi vya Ukimwi na pia si Utamaduni wala Mila za Mzanzibari kumnyanyapaa Mtu mwenye Ugonjwa wa Ukimwi.


Akigusia changamoto zinazowakumba watu wenye virusi vya Ukimwi Mwakilishi huyo wa ZAPHA+  alilitaja tatizo la uhaba wa Dawa nyemelezi ambazo wengi wa waathirika hao wa virusi vya Ukimwi hawana uwezo wa

kuzinunua Dawa hizo ili haki ya Afya ipatikane kikamilifu.


Alisema dawa hizo ni vyema zikaenda sambamba na ule utaratibu wa upatikanaji wa kurejeshwa huduma za vyakula  kwa watoto wanaohudumiwa na Jumuiya ya Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi.


Bibi Sharifa alifahamisha kwamba mpango huo  ulikuwa ukitekelezwa wakati wa kipindi cha nyuma na kuungwa mkono na baadhi ya Taasisi, Mashirika na hata Jumuiya za Kiraia za Kitaifa na Kimataifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.