Habari za Punde

Masauni ahamasisha ujenzi wa nyumba za Polisi kisiwani Pemba, wadau wachangia milioni 400

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (katikati), akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mwajuma Majid Abdalla (kushoto) mabati yaliyochangwa na wadau mbalimbali aliowatafuta Naibu Waziri huyo kwa lengo kuchangia ujenzi wa nyumba za makazi ya Polisi katika Mkoa wa Kusini Pemba na Kaskazini Pemba. Makabidhiano hayo ya mabati, mifuko ya saruji, ndoo za rangi pamoja na nondo yalifanyika ndani ya Meli ya Azam Sealink katika Bandari ya Mkoani. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omari Khamis Othman.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (katikati), akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omari Khamis Othman, nondo zilizochangwa na wadau mbalimbali aliowatafuta Naibu Waziri huyo kwa lengo kuchangia ujenzi wa nyumba za makazi ya Polisi katika Mkoa wa Kusini Pemba na Kaskazini Pemba. Makabidhiano hayo ya mabati, mifuko ya saruji, ndoo za rangi pamoja na nondo yalifanyika ndani ya meli ya Azam Sealink katika Bandari ya Mkoani. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mwajuma Majid Abdalla.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akimuonyesha Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mwajuma Majid Abdalla (kushoto), na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omari Khamis Othman, mifuko ya saruji iliyochangwa na wadau mbalimbali aliowatafuta Naibu Waziri huyo kwa lengo kuchangia ujenzi wa nyumba za makazi ya Polisi katika Mkoa wa Kusini Pemba na Kaskazini Pemba. Makabidhiano hayo ya mabati, mifuko ya saruji, ndoo za rangi pamoja na nondo yalifanyika ndani ya meli ya Azam Sealink katika Bandari ya Mkoani mara baada ya meli hiyo kuwasili na mizigo hiyo kutoka jijini Dar es Salaam. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akizungumza na wananchi wa Pemba pamoja na waandishi wa habari (hawapo pichani) mara baada kukabidhi vifaa mbalimbali vya ujenzi wa nyumba za polisi katika Mikoa ya Kusini Pemba na Kaskazini Pemba, Zanzibar. Katika hotuba yake, Masauni alisema wadau wamemchangia shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 12 za Jeshi la Polisi ili kukabiliana na ukosefu wa nyumba za polisi katika mikoa hiyo. Awamu ya ujenzi wa nyumba hizo ni ya kwanza, na awamu ya pili itakua mikoa ya mipya nchini ambayo ni Geita, Simiyu, Katavi na Songwe. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini, Mwajuma Majid Abdalla, na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omari Khamis Othman.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (wapili kulia) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mwajuma Majid Abdalla (wapili kushoto), na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omari Khamis Othman (kulia), wakitoka ndani ya meli ya Azam Sealink katika bandari ya Mkoani, mara baada ya Naibu Waziri Masauni kuwakabidhi mifuko ya saruji, mabati, ndoo za rangi pamoja na nondo kwa ajili ya kuanza ujenzi wa nyumba za polisi katika mikoa hiyo ya Pemba.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omari Othman akimfafanulia jambo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (wapili kushoto), katika kikao cha ndani kilichofanyika katika ukumbi wa Bandari ya Mkoani, kabla ya Naibu Waziri Masauni hajawakabidhi vifaa vya ujenzi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi ya Polisi katika mikoa ya Pemba. Watatu kulia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Kazi, Ustawi wa Jamii, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto, Zanzibar, Shadia Mohamedi Suleiman, wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mwajuma Majid Abdalla, na kushoto ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Haji Khamis Haji.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akipokea tunda aina ya fenesi kutoka kwa Mkazi wa Chakechake Pemba, Kauthar Issihaka mara baada ya Naibu Waziri huyo kukabidhi vifaa vya ujenzi wa nyumba 12 za polisi katika Mikoa ya Pemba. Tukio hilo la makabidhiano lilifanyika katika Bandari ya Mkoani mara baada ya Meli ya Azam ya Sealink kufikisha vifaa hivyo kutoka jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mwajuma Majid Abdalla, Wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omari Khamis Othman na kulia ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Shahani Mohamed Shahani.


NAIBU Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amewahamasisha wadau mbalimbali wa maendeleo nchini na kufanikisha kupata vifaa vya ujenzi wa mradi wa awamu ya kwanza wa nyumba za Polisi Mikoa ya Pemba, Zanzibar.


Mradi huo umeanza katika Mikoa ya Kusini Pemba na Kaskazini Pemba ambapo nyumba kumi na mbili zinatarajiwa kujengwa ili kufanikisha askari na Maafisa wa Jeshi la Polisi ndani ya mikoa hiyo waweze kuishi katika nyumba za jeshi pamoja na kupunguza tatizo kubwa la ukosefu wa nyumba za makazi ya polisi hao, pia mradi huo utajenga nyumba katika mikoa mipya nchini pamoja na makao ya nchi Dodoma.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo, katika Bandari ya Mkoani katika Mkoa wa Kusini Pemba, jana, Mhandisi Masauni alisema, ujenzi wa nyumba hizo utakua ni wa hatua ya awali, lakini mipango mbalimbali itaendelea kuwezesha nyumba nyingi zaidi kujengwa katika eneo hilo ili kuhakikisha baadhi ya askari wanaoishi nje ya kambi za polisi waweze kuishi kambini ili kuliwezesha Jeshi la Polisi kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa zaidi.

“Leo nimewakabidhi wakuu wa mikoa hawa vifaa vya ujenzi ambavyo ni mifuko ya saruji, nondo, ndoo za rangi na mabati ili waweze kusimamia zoezi hili la ujenzi wa nyumba za askari wetu kwa umakini mkubwa,” alisema Masauni na kuongeza;

“Tunajenga nyumba hapa Pemba ni mradi wa awamu ya kwanza, kwa awamu ya pili tutaenda katika maeneo mengine ya nchi, hususani mikoa mipya yaSimiyu, Geita, Katavi na Songwe na pamoja na Makao ya nchi Dodoma, kwa kuwa askari wetu hawa wanafanya kazi kubwa sana kwa kuwalinda raia wa nchi hii kuendelea kuwa salama kwa wao wenyewe pamoja na mali zao.”

Alisema anawashukuru wadau mbalimbali kwa kujitolea kutoa vifaa hivyo ili kufanikisha suala hilo na aliwataka watanzania wawe na moyo kama wadau hao kwa kuipenda nchi yao, kupenda maendeleo kwa kutoa misaada mbalimbali.

Masauni alifafanua kuwa, suala la maendeleo halina siasa, tuijenga nchi, katika mazingira mengi ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa maana ya Unguja katika suala la kujitolea wamekua wanafanya hivyo, ila kuna changamoto kidogo kwa upande waPemba pana tatizo la masuala ya kisiasa, watu wamekua wakiingiza siasa mbele katika masuala ya nchi katika mikoa hiyo ya Pemba, ambapo alisema jambo hilo sio jema katika maeneleo ya nchi.

“Serikali zote mbili ya Bara na Visiwani zipo kuwahudumia wananchi wote, wakati wa siasa umepita, sasa hivi tunataka kila mmoja ashiriki katika masuala yote ya kimaendeleo, askari hawa wanaangalia usalama wa watu wote, bila kujali hitikadi, dini ya mtu, wapi anatoka, bila kujali rangi yake bila kujali kabila lake,” alisema Masauni.

Alisema viongozi wa Serikali katika mikoa ya pemba wamekua wakipata tabu kuhamasisha katika masuala mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao, hivyo wao kama serikali kuu wameamua kupeleka maendeleo katika maeneo ambayo yanakua yana tabu katika kuhamasisha masuala ya maendeleo, hivyo wakaamua waje mikoa hiyo ya Pemba katika awamu hiyo ya kwanza ya mradi.

Akizungumzia ujio huo wa Naibu Waziri pamoja na ujenzi wa nyumba hizo, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mwajuma Majid Abdalla, alisema anamshukuru kiongozi huyo kwa kuwaletea maendeleo hayo makubwa ya ujenzi wa nyumba za polisina kumuhkikishia vifaa walivyopokea watasimamia ujenzi wa nyumba hizo kwa nguvu zao zote.

“Sisi wakuu wa mikoa tunakushuru naibu waziri kwa hili ulilolifanya, tunakuhakikishia tutasimamia ujenzi huu kwa juhudi zote mpaka nyumba zitakapokamilika, tunasema asante sana kwa kuhamasisha wadau na hatimaye kufanikiwa kupata vifaa hivi,” alisema Mwajuma.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.