Habari za Punde

Jumia Travel :Mwaka 2018 Uwe wa Sekta ya Utalii Kukubali Mabadiliko ya Kiteknolojia Inayojitokeza

Sekta ya utalii nchini Tanzania imetakiwa kukubali kuendana na mifumo mipya inayotokana na maendeleo ya TEHAMA katika uendeshaji wa huduma zao na kuwahudumia wateja ili kujiongezea thamani na kuleta tija zaidi kwenye biashara zao.

Akizungumzia juu ya maendeleo ya mifumo ya kiteknolojia kwenye sekta ya utalii, Meneja Mkazi wa Jumia Travel Tanzania, ambayo ni kampuni inayojihusisha na huduma za hoteli kwa njia ya mtandao Afrika amebainisha kuwa tabia za wateja zinabadilika kwa kasi na zinachochewa na maendeleo ya tekinolojia duniani.
“Hapo nyuma kidogo hoteli zilikuwa ni sehemu za malazi ambazo watu walikuwa wanakwenda kupumzika tofauti na mahali wanapoishi.

Lakini sasa hivi mambo yamebadilika na kutoa wigo mpana kwani wateja hawaendi kwenye hoteli kupumzika tu bali kuwezeshwa kuendelea na shughuli zao kama kawaida. Shughuli hizo zinaweza kutegemea tekinolojia moja kwa moja au zisitegemee, kitu ambacho kimeifanya TEHAMA kuwa na umuhimu mkubwa kwa mameneja wa hoteli na kuwapatia uzoefu wateja juu ya huduma mbalimbali,” alisema Bw. Gerniers.

“Karibu ujihudumie. Leo hii, wateja wengi hupendelea zaidi kutumia tekinolojia kujihudumia wenyewe na mambo madogomadogo kuliko kukutana na wahudumu hotelini moja kwa moja. Zipo huduma kadhaa zinazopendekezwa na wateja ambazo zinaweza kuwekwa kwenye mifumo ya kitekinolojia na kujiendesha zenyewe. Hii itaweza kusaidia kuwapunguzia mzigo wa kazi mameneja na wahudumu wa hoteli na kuwaacha wateja wajihudumie wenyewe,” aliongezea.

Akifafanua zaidi namna Jumia Travel inavyosaidia kurahisisha uendeshaji wa huduma za hoteli kwa mameneja, Meneja Mkazi huyo amesema kuwa, “Tumeutambulisha mfumo rahisi wa uendeshaji wa shughuli za hoteli unaojulikana kama Extranet. Tekinolojia hii ya kisasa inayotumika duniani kote humpatia fursa meneja uwezo wa kusimamia shughuli mbalimbali kama vile; kujulishwa mteja anapotaka huduma mara moja; kupitia taarifa za huduma iliyoombwa na mteja; kuperuzi au kutafuta huduma zilizoombwa; na kuthibitisha au kukataa ombi la mteja papo hapo,” alisema na kuhitimisha, “Kwa kuongezea, meneja anaweza kubadili au kurekebisha bei za vyumba na upatikanaji wake katika siku husika au zijazo pia. Lakini kupitia mfumo huu ni rahisi kuelewa tabia za wateja kama vile; kujulisha mara mteja anapotembelea na kutathmini hoteli yako; kujifunza kilichowavutia wateja na wanachofikiria nini kiboreshwe; na kupata takwimu za utendaji wa hoteli kwenye mtandao wa Jumia Travel kupitia idadi ya wanaotembelea, kuomba na kutumia huduma.”     

Naye kwa upande wake Mshauri wa Huduma kwa Wateja kwenye kampuni hiyo, Flora Rwehumbiza ameongezea kwa kutoa maoni yake kwamba bado sekta ya hoteli nchini Tanzania inakumbwa na changamoto katika kupokea mabadiliko kwa upande wa kitekinolojia.

“Mbali na Jumia Travel kutoa fursa kwa mameneja wa hoteli na wateja kujiendesha wenyewe na kujihudumia mtandaoni, pia tuna dawati la huduma kwa wateja linalofanya kazi masaa 24. Dawati hili ni mbadala wa pale kunapotekea changamoto mbalimbali lakini pia kutoa msaada pale unapohitajika. Asilimia kubwa ya wateja wanajitahidi kufanya kila kitu wao wenyewe kwenye mtandao wetu lakini changamoto huja kwa upande wa hoteli,” alisema.

“Unakuta mara nyingi kuna masuala rahisi ambayo yanaweza kufanywa na mameneja lakini hayafanywi mpaka tuwapigie simu na kuwakumbusha mara kadhaa. Kwa mfano, mfumo wetu wa ‘Extranet’ umerahisisha huduma kama vile kuona maombi ya huduma za vyumba hotelini, kukubali au kukataa pamoja na kubadili bei za vyumba au upatikanaji wake kwa siku husika au ndani ya muda fulani ujao. Lakini mameneja hawafanyi hivyo mpaka tuwakumbushe kwa kuwapigia simu kitu ambacho huwa kinaleta mkanganyiko baina yetu, wateja na hoteli,” alihitimisha Bi. Rwehumbiza.

Kuhusu Jumia Travel
Jumia Travel (www.travel.jumia.com) ni kampuni nambari moja barani Afrika katika utoaji wa huduma za usafiri mtandaoni, inarahisisha huduma za usafiri kwa kumpatia uzoefu mtumiaji kwa kulinganisha bei na huduma zinazopatikana kwa njia ya haraka na salama zaidi.

Ikiwa ina hoteli zaidi ya 30,000 Afrika (na zaidi ya hoteli 300,000 duniani) na makampuni ya ndege zaidi ya mia moja kama washirika wake, Jumia Travel inalenga kutoa uhuru wa kusafiri kupitia kupunguza gharama za kusafiri, kutoa orodha kubwa ya hoteli na kuwezesha huduma bora na zenye viwango vya juu kwenye kila nchi husika ili kuwa mojawapo ya sehemu ambayo mteja atakidhi haja zake zote za kiusafiri barani.
Jumia Travel inafanya shughuli zake katika nchi zaidi ya 40 za Afrika, ikiwa na ofisi kwenye nchi 10 miongoni mwake, na wataalamu wa masuala ya kusafiri zaidi ya 400 ambao wapo tayari kuwahudumia wateja wakati wowote. Ofisi zetu kuu zinapatikana Lagos (Nigeria), Accra (Ghana), Dakar (Sénégal), Abidjan (Ivory Coast), Algiers (Algeria), Douala (Cameroon), Kampala (Uganda), Dar Es Salaam (Tanzania), Nairobi (Kenya) na Addis Ababa (Ethiopia). Kabla ya mwezi Juni 2016, Jumia Travel ilikuwa ikijulikana kama Jovago. Ilianzishwa 2013 na Jumia huku ikiendeshwa kwa ushirikiano wa MTN, Rocket Internet, Millicom, Orange, Axas na washirika wengine.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.