Habari za Punde

Rais Dk Shein awasamehe wanafunzi 12


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa msamaha kwa wanafunzi kumi na mbili (12) ambao bado walikuwa wakiendelea kutumikia vyuo vya Mafunzo vya Unguja na Pemba ikiwa ni miongoni mwa Sherehe za miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahaya Mzee ilieleza kuwa kwa uwezo aliopewa chini ya kifungu cha 59 cha Katiba ya Zanzibar 1984, Mheshimiwa Rais ameamuru kuwa kifungo kilichobaki cha wanafunzi walionufaika na msamaha huo, ambao bado wanaendelea kutumikia katika vyuo vya Mafunzo vya Unguja na Pemba kuwa kipindi hicho chote kinafutwa na kwamba wanafunzi hao waachiwe huru kuanzia tarehe 11 Januari 2018.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, kwa kuwa Zanzibar itakuwa inasherehekea miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar hapo tarehe 12 Januari 2018, na kwa kuwa Mhe. Rais ameridhika kuwa kuna sababu za kutosha za kutumia uwezo wake huo katika sherehe hii, wanafunzi hao waachiwe huru.

Walionufaika na msamaha huo kwa Unguja ni Abdul-Azizi Abdalla Mohamed, Omar Abdalla Nuhu, Ali Khamis Mrau, Mussa Ali Vuai, Hassan Seif Khamis, Nassor Abeid Issa, Jihadi Jalala Jihadi na Edward Jeremia Magaja.

Aidha, wengine walionufaika na msamaha huo kwa upande wa Pemba ni Sleiman Abdalla Amir, Mtumwa Khamis Kaimu, Said Seif Omar na Masoud Seif Nassor.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.