RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa Serikali imejidhatiti
kuzifikisha huduma za umeme katika maeneo yote wanayoishi wananchi kwa kutambua
kuwa huduma hizo zinaenda sambamba na maendeleo ya dunia na siyo anasa kama
ilivyokuwa hapo zamani.
Dk. Shein
aliyasema hayo leo mara baada ya kuzindua umeme katika kisiwa cha Fundo
kilichopo Jimbo la Gando, Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni miongoni mwa
shamrashamra za kutimiza miaka 54 ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.
Rais Dk.
Shein alisema kuwa ukosefu wa huduma hizo unadumaza juhudi za wananchi katika
kujitafutia maendeleo kwani umeme ni msingi wa maendeleo.
Hivyo,
Dk. Shein alitoa nasaha zake kwa wananchi wa kisiwa hicho kuongeza kasi, ari na
hamasa ya kutafuta maendeleo hasa kwa kujishughulisha na miradi ambayo mwanzo
walishindwa kuifanya kwa kukosekana nishati hiyo.
“Ni jambo la faraja kuona kwamba tumepiga
hatua kubwa kufikisha huduma muhimu katika visiwa vidogo vidogo na vijiji
vilivyo katika maeneo ya mbali kwani lengo letu ni kuhakikisha kila mwananchi
wa Zanzibar popote alipo anapata huduma za umeme, afya, elimu, maji safi na
salama na huduma nyenginezo”,alisema Dk. Shein.
Aidha,
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa viongozi wote wa Wizara ya
Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira pamoja na Shirika la Umeme (ZECO) na Bodi
yake kwa kuwa wepesi wa kutekeleza maagizo yake kwa kusimamia vyema Ilani ya
CCM ya Uchaguzi kwa kipindi kilichomalizika na kilichopo hivi sasa cha
2015-2020.
Alieleza
kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa Ilani hiyo na kutumia fursa ya kukisoma
kipengele kinachoelezea utekelezaji huo mbele ya maelfu ya wananchi
waliohudhuria katika hafla hiyo kutoka Mikoa na wilaya zote za Pemba.
Pia, Dk.
Shein alieleza kufurahishwa kwake kwa kumekuwepo na wataalamu wa hapa hapa
Zanzibar ambao wamefanya kazi hiyo kutokana na ujuzi wao na uwezo wa kuufikisha
umeme kwenye visiwa kwa kuzipitisha nyaya za umeme chini ya bahari.
Aliwapongeza
wananchi wote wa kisiwa cha Fundo kwa kushirikiana na ZECO tangu hatua za
mwanzo za utekelezaji wa mradi huo hadi pale umeme ulipoanza kuwaka pamoja na
ukarimu na mashirikiano walioyonayo na umoja wao.
Dk. Shein
aliongeza kuwa yeye anapotoa ahadi kwa wananchi huwa hasahau kwani anakumbuka
wakati akiwa katika Kampeni za Uchaguzi mwaka 2010 akiwa Chanjani Chokocho
katika uwanja wa “Black Wizard” aliahidi kuwa kisiwa cha Makongwe na Kisiwa
Panza ataufikisha umeme ahadi ambayo tayari ameshaitekeleza.
Alieleza
kuwa hivi sasa Serikali imeshafikisha umeme katika visiwa saba vya Zanzibar
ambapo visiwa hivyo ni Tumbatu na Uzi kwa upande wa Unguja na Kojani, Kisiwa
Panza, Makongwe, Mwambe Shamiani na Fundo kwa upande wa Pemba.
Dk. Shein
alisema kuwa hivi sasa Serikali inaendelea na visiwa vitatu vilivyobaki ambavyo
ni Uvinje, Kokota na Njau vyote vipo Pemba ambapo Serikali imejipanga kufikisha
umeme katika visiwa hivyo kabla ya kumalizika mwaka 2020.
Sambamba
na hayo, Dk. Shein aliwaleza wananchi wa kisiwa cha Fundo kuwa ameliona tatizo
la usafiri wa bahari wanaoupata wananchi wa kisiwa hicho na kuahidi kuwa
Serikali italitafuatia muwarubaini wa tatizo hilo.
Pia,
alitumia fursa hiyo kueleza historia ya umeme hapa Zanzibar na kusema kuwa
Zanzibar ni nchi ya mwanzo kupata huduma hiyo katika nchi za Afrika mashariki
na kati na kwa upande wa umeme wa barabarani Zanzibar ulianza kuwaka mwanzo
kuliko mji wa London.
“Umeme
huu ni wa kweli na sio umeme feki … natoa pongezi kwa ZECO kwa kuwakopesha
wananchi hawa umeme pamoja na kuwapunguzia malipo ya kuwaungia umeme, nasema
ahsanteni sana”, alisema Dk. Shein.
Aidha,
aliwataka wananchi wa kisiwa cha Fundo kujiandaa kuwa walipaji wazuri wa umeme
hasa ikizingatiwa kuwa Srerikali inalipa fedha nyingi kutoka Tanzania Bara
unakotoka umeme huo, hivyo kila mmoja aone fahari kulipa kwa wakati na kwa
mujibu wa matumizi yake, ili huduma hizo ziweze kupatiakna kwa wote.
Kwa
upande mwengine Dk. Shein alitoa indhari kuwa umeme ni hatari na kuwataka
wananchi wa kisiwa hicho kuchukua tahadhari wakati wanapoutumia.
Sambamba
na hayo, Dk. Shein alisisitiza kuendeleza umoja wao na mshikamano wao kwani
umoja wao na ndio uliopelekea MwenyeziMungu kuwapelekea neema hiyo ya umeme na
kuwataka wasihasimiane kwa siasa na kuwataka kuengeza nguvu katika maendeleo
huku wakitambua kuwa vyama vya siasa ni sare tu ya dunia.
Nae
Waziri wa Ardhi, Maji,Nishati na Mazingira Salama Aboud Talib alimpongeza Dk.
Shein kwa kuwa makini katika kutekeleza ahadi anazoziahidi kwa wananchi huku
akieleza mashirikiano makubwa yaliopatikana kutoka kwa wananchi.
Mapema
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Alhalil Mirza, alieleza kuwa mradi huo wa usambazaji
wa umeme umehusisha ujenzi wa njia kuu za umeme wa kilovolti 33 kutoka Ukunjwi
hadi
Ras Ukunjwi na pia ndani ya kisiwa cha Fundo wenye jumla ya kilomita 7.29.
Uwekaji
wa transfoma nne katika vijiji vya Kimeleani, Ngagu, Ndooni na Mabaoni, ujenzi
wa njia ndogo za umeme zenye jumla ya kilomita 8 na ulazaji wa waya wa
bahari wenye urefu wa kilomita 2.5.
Aliongeza
kuwa mradi huo umegharamiwa na Searikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jumla ya
TZS Bilioni 2,078,222,518 ambapo kati ya fedha hizo Serikali imetoa Bilioni 1.7
na ZECO imechangia milioni 302.2
Alieleza
kuwa kazi ya ujenzi wa umeme mkubwa, umeme mdogo na uwekaji wa transfoma
zilimalizika mwezi Aprili, 2017 na kazi ya ulazaji wa waya baharini ilimalizika
tarehe 6 Agosti 2017 na kumalizika tarehe 11 Agosti 2017.
Katibu
Mkuu huyo alieleza kuwa kazi zote za upelekeaji wa umeme kisiwani humo
zimefanywa na kusimamiwa na wataalamu wazalendo wa ZECO huku akieleza kuwa
tayari nyumba 340 kati ya nyumba 640 zimeshatiwa umeme kisiwani humo.
Alisema
kuwa katika kufikia malengo ya Dira 2020 na MKUZA III Serikali kupitia ZECO
imeshafikisha huduma ya umeme kwa asilimia mia moja 100% kwa Shehia zote za
Unguja na Pemba ambapo ni sawa na asilimia 91% kwa ngazi ya Vitongoji.
Nao
wananchi wa kisiwa hicho walitoa pongezi kubwa kwa Dk. Shein kwa kutimiza ahadi
hiyo ya kuwapelekea umeme na kumuombea dua Mungu ampe nguvu zaidi ili azidi
kuendelea kuwasaidia wananchi wake anaowaongoza.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment