Mkurugenzi
Mipango Idara ya Mafunzo ya Amali, Khalid
Masoud Waziri akizindua Warsha ya siku mbili huko chuo cha Walimu Suza katika mradi
ulioandaliwa Idara ya Elimu ya kuwawezesha walimu wa sanaa (Art) kuwa Walimu wa
sayansi. (Picha na Miza Othman –Maelezo Zanzibar).
Walimu
wakuu, Wasaidizi na Maofisa wa Elimu wa Wilaya za Unguja wakimsikiliza Mgeni
Rasmi alipokuwa akizindua Warsha hiyo. (Picha na Miza Othman –Maelezo Zanzibar).
Mkurugenzi Khalid Masoud
akiwa katika picha ya pamoja na Wahadhiri wa (SUZA), Walimu wakuu na
wasaidizi wa Skuli za Unguja na Maofisa wa Elimu wa Wilaya. (Picha na Miza
Othman –Maelezo Zanzibar).
Waandishi wa Habari wakipata Maelezo kutoka kwa Mkuu wa Divisheni ya Vituo vya
Ualimu Maulid Omar Hamad wakati wa mafunzo ya walimu wakuu na
wasaidizi wao yanayoendelea katika ukumbi wa chuo kikuu cha Walimu-SUZA. (Picha
na Miza Othman –Maelezo Zanzibar).
Na
Bahati Habibu - Maelezo Zanzibar.
Walimu
Wakuu wa skuli mbalimbali za Zanzibar, wametakiwa kuwafuatilia vyema walimu walio
chini yao ili kuhakikisha ufaulu mzuri katika masomo ya sayansi.
Akizindua
warsha ya kuwabadilisha walimu wa masomo ya sanaa kuwa wa sayansi iliyofanyika
katika Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) kampasi ya Nkrumah, Mkurugenzi Mipango Idara
ya Mafunzo ya Amali Khalid Masoud
Waziri, amesema iko haja kwa walimu kubadilika ili kufikia malengo ya wizara.
Alieleza
kuwa walimu wanapaswa kuhakikisha idadi ya wanafunzi wanaofaulu masomo ya
sayansi, hesabati na Kiingereza inaongezeka ili kuwajengea mazingira ya
kuhimili soko la ajira kwa sasa.
Katika
warsha hiyo ya siku mbili kupitia mradi ulioandaliwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya Amali chini ya usimamizi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Mkurugenzi
huyo alisema taasisi nyingi zinapotoa ajira mpya, huangalia zaidi vijana
wanaofaulu vizuri masomo ya sayansi kulingana na mahitaji yao.
Nae
Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo ya Walimu Salha Said, amewasisitiza walimu
kuyafanyia kazi mafunzo watakayopata ili waweze kwenda sambamba na sera ya
Serikali ya Viwanda na Masoko kwa kuwaandaa wanafunzi mapema ili taifa lipate wanasayansi
walio bora kwa maendeleo.
Ili kufikia
lengo hilo, amewataka Walimu Wakuu, Wasaidizi na Maofisa wa Elimu Wilaya za
Unguja, kuongeza ushirikiano katika kuhakikisha walimu wanatumia mbinu zilizo bora
za ufundishaji katika masomo hayo.
Dk. Maryam
Jaffar Ismail, Mshauri Elekezi wa mradi huo, pia amesema, ili kuongeza ufaulu
wa wa wanafunzi, ipo haja kwa walimu kupatiwa mafunzo ya lugha ya Kiingereza ambayo
ndiyo inayotumika katika ufundishaji wa masomo ya Sayansi na Hesabati.
“Tafauti
na ilivyo sasa, walimu wengi wanatumia lugha ya Kiswahili kwa asilimia 98
katika kufundisha masomo ya sayansi, hali inayosababisha wanafunzi wasifaulu
vizuri kwa kuwa mitihani huandikwa kwa Kiingereza,” alisema Dk. Maryam.
Aidha,
alisema kupitia mradi huo, wanapanga kuwaandalia zawadi walimu na wanafunzi
watakaofanya vizuri katika masomo hayo.
Mradi
huo wa miaka minne, utahusisha uandaaji wa vitabu vya Sayansi na Hesabu pamoja
na lugha ya Kiingereza, na kuwapa mbinu mbalimbali walimu ili kuongeza kiwango
cha ufaulu wa daraja la juu kwa wanafunzi.
No comments:
Post a Comment