Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Apokea Matembezi ya Vijana Kumuenzi Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.

Vijana wa Umoja wa Vijana wa CCM wakiimba Wimbo Maalum wa Sisi Sote Tumekombora mara baada ya kumaliza matembezi yao hapo Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui.
Balozi Seif na baadhi ya Viongozi wa Chama cha Mapinduzi wakiungana na Vijana hao kuimba Wimbo huo Maalum unaowakumbusha Ukombozi wa Visiwa vya Zanzibar.
 Vijana 400 wa Umoja wa Vijana wa CCM wakiingia katika Viwanja vya Afisi Kuu ya CCM Kisiwanduzi kumalizia Matembezi yao yaliyoanzia Mwera Kiongozi Kijiji alichozaliwa Mzee Karume na Kupokewa na Balozi Seif.
 Balozi Seif akiweka Shada la Maua kwenye Kaburi la Marehemu Mzee Karume Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui kabla ya kuyapokea Matembezi ya Vijana wa CCM ya kumuenzi Kiongozi huyo wa Mapinduzi hayo.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana  na Mke wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar aliyeongoza Mapinduzi Matukufu ya Mwaka 1964 Mzee Abeid Karume Mama Fatma Karume hapo Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui.
Balozi Seif akiwa pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa akiwahutubia Vijana wa Chama cha Mapinduzi {UVCCM} hapo Afisi Kuu ya CCM  Kisiwandui baada ya kumaliza matembezi yao. 


Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na mamlaka husika itatafakari namna bora zaidi ya kukusanywa kwa Kumbukumbu muhimu za Kiongozi wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar  Marehemu Mzee Abeid Aman Karume  ili ziwe kielelezo cha Taaluma kwa Kizazi cha sasa.
Alisema Kumbukumbu hizo ndio njia pekee ya kuendelea kumuenzi Kiongozi huyo  kwa kufuata fikra na mawazo aliyowaachia  Wananchi wa Zanzibar wakielewa kwamba yeye ndie aliyeongoza mapambano dhidi ya Wakoloni na hatimae kupatikana kwa Ukombozi wa Visiwa vya Zanzibar.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo baada ya kuyapokea Matembezi  Maalum ya Vijana  400 wa Chama cha Mapinduzi ya kumuenzi Mzee Abeid Aman Karume  yaliyoanzia Kijiji alichozaliwa cha Mwera Kiongoni na kumalizia katika Viwanja vya Afisi Kuu ya CCM  Kisiwanduzi Mjini Zanzibar.
Alisema Maisha ya Mzee Abeid Amani Karume Kisiasa  yanastahiki  kuenziwa ili iwe Darasa Maalum  kwa Vijana, Wageni sambamba na Wataalamu wa Kigeni wanaofika Zanzibar kujifunza Hitoria ya Visiwa Vya Zanzibar  kabla na baada ya Ukombozi.
Balozi Seif aliwataka Vijana kutambua  wajibu wao kwa  kuepuka kutenganishwa  ili  waendelee kuimarisha Umoja miongoni mwao mambo ambayo itakuwa vigumu kwa Watu au Vikundi  vyenye nia ya kutaka kuwafitinisha  kwa kuwapandisha cheche ya dharau, kejeli na hatimae kuzaa makundi yatakayosababisha kuwepo kwa sumu ya Umoja wao.
Alisema Serikali zote mbili Nchini Tanzania pamoja na Chama cha Mapinduzi ziko madhubuti katika kuwatumikia Wananchi wake huku zikielewa kuwategemea Vijana wake wanaopaswa kulitambua hilo bila ya kukata tamaa pale zinapotokea changamoto mbali mbali.
Balozi Seif  aliwatahadharisha Vijana kutambua kwamba bado wapo Watu wanaodhani kwamba Sultani na Vibaraka wao waliopeperushwa katika Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari Mwaka 1964 wanaendelea na kasumba ya kuhisi wameonewa.
Alitanabahisha na kuweka wazi kwamba Mapinduzi hayo ya Januari Mwaka 1964  ndio yaliyoleta Heshima na Utu wa Mwafrika  wa Zanzibar  na Watanzania  wote ikiwa ni chanzo kikubwa cha Umoja wa Wananchi wote wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Balozi Seif aliwapongeza Watembeaji hao kwa ajili ya Kumuenzi Mzee Karume  kwa kuendelea kulinda pamoja na kutunza Amani ya Taifa hili huku wakitambua kwamba Bila ya Amani na utulivu hakuna Maendeleo ye yote  yanayoweza kupatikana.
Alifahamisha kwamba Amani na Utulivu uliopo Nchini umesababisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupiga hatua kubwa za Maendeleo ikiwemo ongeaeko la Kiwango cha Mishahara kwa asilimia 100% kwa kima cha chini ambacho kwa sasa ni Shilingi Laki Tatu.
Balozi Seif alieleza kwamba Serikali Kuu tayari imeshaandaa  mazingira Rafiki kwa ajili ya Wawekezaji pamoja na Ujenzi wa Vyuo vya Amali  kila Wilaya ili kurahisisha maisha ya Vijana wa Zanzibar na Wananchi kwa ujumla.
Aliwaomba Vijana kujiunga na Vyuo vya Wajasiri Amali ili watakapomaliza na kuhitimu kuwa na ujuzi utaoweza kuwasaidia katika Ajira kwa vile Serikali kuu kwa sasa haimudu kuajiri Vijana wote hasa ikizingatiwa uboreshaji wa mazingira  yua Kielimu.
Mapema akitoa Taarifa ya Matembezi hao Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM { UVCCM} Zanzibar Nd. Abdulghafar   Idrisa aliushukuru Umoja wa Askari Wastaafu Zanzibar {UMAWA} kwa msimamo wao wa kuwaunga mkono Vijana katika Matembezi hayo.
Nd. Abdulghafar alisema Uzalendo  wa Wazee hao umeonyesha jinsi gani walivyojikubalisha kuendelea kuyaunga Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoongozwa na Jemadari wao Marehemu Mzee Karume aliyeuawa kikatili na wapinga Maendeleo wa Visiwa vya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Vijana wa CCM Zanzibar alifafanua kwamba Mzee Karume aliuawa kwa sababu ya msimamo wake wa kuyalinda, kuyatunza na kuyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 akiwa Kiongozi wa Mapinduzi hayo.
Akitoa salamu  Mlezi wa Vijana hao Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar Dr. Abdulla Juma Abdulla { Mabodi }alisema lile wazo la kutaka kuanzishwa kwa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mzee Karume { Karume Foundation } hivi sasa linafanyiwa kazi ili kuona ile kiu ya Wazalendo waliofikiria jambo hilo muhimu inafanikiwa ipasavyo.
Alisema kuanzishwa kwa Taasisi hiyo muhimu kutawawezesha Wananchi kufahamu kwa undani ndoto na dhamira ya Muasisi huyo wa Chama cha Afro Shiray Party aliyokuwa  inatimia  katika  kusimamia haki ya Wananchi waliowengi Wakulima na Wafanyakazi.
Vijana hao 400 wa Umoja wa Vijana wa CCM kutoka Mikoa yote ya Zanzibar walipata  Mafunzo ya Historia ya vugu vugu la Ukombozi  Zanzibar  wakati wa usiku na alfajiri kuanza matembezi yaliyoanzia Kijiji alichozaliwa Jemedari wa Mapinduzi ya Zanzibar Mzee Karume huko Mwera Kiongoni Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.