Habari za Punde

Taasisi ya ZANRDEF Atowa Msaada wa Uchimbaji wa Kisima Skuli ya Mahonda Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifika Skuli ya Mahonda kukagua uchimbaji Kisima cha Maji safi na salama kitakachowaondoshea usumbufu Wanafunzi na Walimu wa Skuli hiyo.
Balozi Seif pamoja na Uongozi wa Wilaya ya Kaskazini B na Kamati ya Maendeleo ya Jimbo la Mahonda wakishuhudia harakati za Uchimbwaji wa Kisima cha Maji safi na Salama katika Skuli ya Mahonda Msingi na Sekondari chini ya usimamizi wa Mhandisi wa Taasisi hiyo Bwana Doto Saleh wa kwanza Kulia aliyevaa Kofia ya Manjano.
Balozi Seif Kati Kati akipongeza na Kuishukuru Taasisi ya Kiraia kwa uamuzi wake wa kusaidia huduma za Maji Safi na Salama Ndani ya Skuli ya Msingi na Sekondari ya Mahonda.Kushoto ya Balozi Seif ni Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini B Nd. Rajab Ali Rajab na Kulia yake ni Katibu wa ZANRDEF Bwana Ali Mohamed Haji.
Harakti za uchimbwaji wa Kisima cha Maji safi na Salama katika Skuli ya Mahonda zikiendelea licha ya mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha muda mrefu.
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B”  Nd. Rajab Ali Rajab akitoa shukrani kwa Uongozi wa Jimbo la Mahonda na Taasisi ya Kiraia ya ZANRDEF kwa jitihada za kusogeza huduma za Maji safi katika Skuli ya Mahonda Msingi na Sekondari.

Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  aliishukuru na kuipongeza Taasisi ya Kiraia ya Zanzibar Relief  and Development Foundation      { ZANRDEF} kwa uamuzi wake wa kusaidia huduma za msingi ya Kijamii za Maji safi katika azma yake ya kuona maisha ya Wananchi yanaendelea kustawika.
Alisema uamuzi huo wa ZANRDEF utasaidia kuwapunguzia machungu Wananchi walio wengi kupata huduma hizo sambamba na kuiunga Mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  katika mipango yake ya kuwasogezea karibu mahitaji ya msingi Wananchi wake.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda alitoa shukrani hizo wakati akizungumza na Viongozi wa Kamati ya Maendeleo ya Jimbo la Mahonda mara baada ya kukikagua Kisima cha Maji safi na salama kinachochimbwa  katika Skuli ya Mahonda kwa msaada wa Taasisi ya ZANRDEF.
Alisema zipo changamoto nyingi za upatikanaji wa huduma za Maji safi na salama kwa Wananchi walio wengi Visiwani Zanzibar licha ya juhudi kubwa inayoendelea kuchukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na washirika wa Maendeleo kuitafutia  ufumbuzi changamoto hiyo.
Balozi Seif  aliutolea mfano Mkoa wa Kaskazini Unguja ukiwa ni miongni mwa Mikoa inayokumbwa na changamoto hiyo hasa kwa baadhi ya Vijiji, Majengo ya huduma za Kijamii kama Hospitali na Maskuli lakini kukosekana kwa huduma hiyo kwa baadhi ya maeneo wakati mwengine husababishwa kwa makusudi na baadhi ya Watu kwa sababu za itikadi za Kisiasa.
Aliwanasihi Wananchi kuendelea kuheshimu Miundombinu mbali mbali inayowekwa na Serikali sambamba na baadhi ya Watu kuacha tabia ya kuiharibu kwa makusudi Miuondombinu hiyo kwani inaweza kulisababishia hasara kubwa Taifa.
Mapema Katibu wa Taasisi ya Kiraia ya Zanzibar Relief and Development Foundation  Bwana Ali Mohamed Haji alisema Taasisi hiyo inayoshirikiana na Ubalozi wa Uturuki Nchini Tanzania imeazimia Kuchimba Visima  40 Zanzibar ili kusaidia kupatikana kwa huduma ya Maji safi na salama.
Bwana Ali alisema Visima Vitano vya mwanzo vinatarajiwa kuchimbwa ndani ya Jimbo la Mahonda ambapo kile cha Skuli ya Mahonda kikiwa cha kwanza katika idadi hiyo ya awamu ya kwanza.
Alisema Awamu ya Pili ya uchimbaji Visima hivyo inatarajiwa kuanza ndani ya Mwezi wa Mei kwa Visima 35  vitakavyotumia Nishati ya Umeme wa Jua ambavyo kati ya hivyo 15 vitachimbwa ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B” inayoonekana kukumbwa zaidi na changamoto ya huduma ya Maji safi na salama.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B”  Ndugu Rajab Ali Rajab alisema  huduma za maji safi na salama ndani ya Wilaya hiyo zimekuwa na upungufu unaoleta athari kwa Jamii hasa katika Vituo vya Afya na Maskuli.
Nd. Raj alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif  kwamba Wilaya ya Kaskazini “B” ina Vituo 14 vya Afya  na Skuli 31 ambazo asilimia kubwa ya Majengo yake yanakabilia na changamoto za huduma za maji safi na salama.
Alisema hali hiyo wakati mwengine inaleta na kusababisha hatari ya kuchafuka kwa mazingira na kuwapa kazi nzito zaidi akina Mama Wajawazito wanaofika katika Vituo vya Afya kwa ajili ya kujifungua.
Uchimbaji wa Kisima cha maji safi na salama ndani ya Skuli ya Mahonda  unatarajiwa kukamilika muda mfupi kutokana na ubora wa mashine zinazotumiwa na Taasisi ya ZANRDEF ambapo utasaidia kuwaondoshea shida Wanafunzi wake pamoja na Wananchi wa Vijiji vinavyoizunguuka Skuli hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.