STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 05.04.2018
HOSPITALI ya Drum Tower ya Mjini Naijing katika Jimbo la
Jiangsu ya nchini China imeahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika
kuimarisha sekta ya afya.
Rais wa Hospitali hiyo
Han Gungshu akiwa na ujumbe wake wa madaktari kutoka nchini China aliyasema
hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu Mjini Zanzibar.
Katika maelezo yake,
Kiongozi huyo ambaye yupo Zanzibar kwa lengo la kuendeleza mashirikiano na
mahusiano mema katika sekta ya afya kati ya Serikali ya China na Zanzibar,
alieleza kuwa Hospitali hiyo itaendeleza mashirikiano na hospitali za Zanzibar
ikiwemo hospitali ya Mnazi Mmoja.
Alieleza kuwa tayari
mipango kabambe imeshaandaliwa katika kuanzisha programu mbali mbali kati ya Hospitali
hiyo na hospitali ya MnaziMmoja ikiwa ni pamoja na kuanzisha huduma za saratani
ya mlango wa kizazi.
Aliongeza kuwa huduma
hiyo itatolewa kwa wananchi wa Unguja na Pemba wa mjini na vijijini kwa lengo
la kuhakikisha maradhi hayo yanatokomezwa kwa akina mama wa Zanzibar.
Gungshu alimueleza
Rais Dk. Shein kuwa Hospitali hiyo iko tayari kutoa ushirikiano wake katika
kuendeleza huduma za afya hapa Zanzibar kwa kushirikiana na madaktari wa hapa
nchini kwa kuanzisha programu mbali mbali za tiba ambazo zitatoa huduma kwa
wananchi wa Zanzibar.
Aidha, kiongozi huyo
alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa Jimbo hilo litaendeleza utamaduni wake wa
kuleta madaktari kwa awamu hapa Zanzibar ambao wataendelea kufanya kazi za
kutoa huduma za afya kwa wananchi wa Unguja na Pemba.
Pamoja na hayo, kiongozi huyo alimueleza Rais Dk. Shein
kuwa mashirikiano zaidi yataendelezwa kati ya hospitali hiyo na hospitali za
hapa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuendeleza programu za rasilimali watu katika
kada mbali mbali.
Kiongozi huyo ambaye
mama yake mzazi aliwahi kufanya kazi katika hospitali Kuu ya MnaziMmoja mnamo
miaka ya 70, alisifu mashirikiano wanayopata madaktari kutoka nchini China
kutoka kwa wananchi wa Zanzibar hali ambayo huwafanya madaktari hao nao
kuzidisha mapenzi na utoaji huduma za afya kwa ndugu zao wa Zanzibar.
Nae Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alimpongeza kiongozi
huyo pamoja na hospitali hiyo ya Drum Tower ya Mjini Naijing katika Jimbo la
Jiangsu ya nchini China kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta
ya afya.
Katika mazungumzo
hayo, Dk. Shein alisema kuwa Jimbo la Jiangsu limekuwa na utamaduni wa
kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya kwa muda mrefu ambapo
tokea mwaka 1965 lilianza kuleta madaktari hapa Zanzibar.
Aidha, Rais Dk. Shein
alimueleza kiongozi huyo juhudi za makusudi zinazochukuliwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya na kusisitiza haja ya
kuendelea kuungwa mkono na Hospitali hiyo pamoja na Jimbo lake.
Dk. Shein alimueleza
kiongozi huyo azma ya Serikali kuanzisha kitengo cha upasuaji wa moyo na
kueleza haja ya mashirikiano kati ya pande mbili hizo ili kuimarisha sekta ya
afya hapa Zanzibar huku akipongeza azma ya hospitali hiyo ya kuanzisha huduma
za saratani ya mlango wa kizazi kwa mashirikiano na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo juhudi zinazochukuliwa na Serikali
anayoiongoza katika kutoa mafunzo ya udaktari ndani na nje ya Zanzibar ikiwa ni
pamoja na kuanzisha Skuli ya Udaktari katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar
(SUZA).
Kutokana na juhudi
hizo,Dk. Shein alieleza haja kwa hospitali hiyo kuendeleza ushirikiano wake kwa
kutoa nafasi za masomo katika fani mbali mbali za udaktari wakiwemo madaktari
wa meno ili kuondosha kabisa uhaba wa madaktari bingwa katika Hospitali Kuu ya
Mnazi Mmoja na Hospitali ya Abdala Mzee pamoja na kuleta madaktari
watakaosomesha fani mbali mbali za udaktari katika Chuo hicho.
Pia, Rais Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Serikali ya China chini ya kiongozi wake
Rais Xi Jingpig kwa msaada wake mkubwa kwa kuifanyia matengenezo makubwa
Hopsitali ya Abdalla Mzee sambamba na kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika
kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo
ikiwemo sekta hiyo ya afya hapa Zanzibar.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment