Habari za Punde

Balozi Seif: Uchumi wa Zanzibar umeimarika

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisoma Hotuba ya Bajeti ya Ofisi yake katika Kikao cha Baraza la Wawakilishi kilichoanza mapema leo asubuhi kwenye ukumbi wa Baraza hilo uliopo Chukwanik nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
 Baadhi ya Mawaziri na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakifuatilia Hotuba ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar iliyowasilishwa na Balozi Seif.
 Timu ya Watendaji na Viongozi Wakuu wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wakifuatilia Hotuba ya Bajeti ya Ofisi yao iliyowasilishwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Kijana Mahsusi anayetafsiri Lugha ya alama  kwa ajili ya Watu wenye Mahitaji Maalum katika Vipindi vya Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC} ambavyo vimeanza kuwa hewani katika mwanzo wa Vikao vya Baraza la Wawakilishi.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua, kuthamini pamoja na kupongeza jitihada kubwa zinazochukuliwa na Wawekezaji walioamuwa kuwekeza Zanzibar hasa wale Wazalendo zilizochangia mabadiliko makubwa ya mwenendo wa ukuaji wa Uchumi ambayo ni matokeo ya uwekezaji huo.
Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika Kikao cha Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar kilichoanza leo asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisaema Uchumi wa Zanzibar unakua kwa kasi nzuri ya wastani wa asilimia 6.8% kwa takriban miaka kumi sasa.
Balozi Seif alisema tokea kuasisiwa kwa Sera iliyoruhusu mchango wa Sekta Binafsi karti kati ya Miaka ya 1980 Sekta hiyo imechangia sana katika Uwekezaji wa Rasilmali Nchini hususan katika Sekta ya Utalii hali ambayo Mapato ya Taifa yamekuwa yakiongezeka kwa takriban asilimia 30% mwaka hadi mwaka.
Alisema Uwekezaji huo umekuwa chachu ya Maendeleo kwa Serikali kutekeleza Miradi mbali mbali ya Maendeleo hasa kwa kuwekeza katika Miundombinu ya msingi kama Bara bara, Umeme na Maji ili kwenda sambamba na jitihada za Sekta Binafsi.
Alieleza kwamba Taifa bado halijafikia lengo lililojipangia la kujitegemea lenyenye kwa kutegemea Mapato yake ya ndani kutosheleza mahitaji yake kwa ukamilifu.
“ Leo hii ruzuku kutoka Nje  inachangia chini ya shilingi 8 kwa kila shilingi Mia Moja tunazotumia. Miaka ya nyuma  ruzuku ikichangia  hadi asilimia 40% ya Bajeti ta Serikali”. Alisema Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Hata hivyo Balozi Seif alifahamisha kwamba hali ya sasa imepunguza utegemezi wa misaada kutoka nje ya Nchi katika kugharamia shughuli za Serikali ambapo kwa sasa imeweza kuimarishwa kwa Mishahara ya Watumishi wa Umma.
Licha ya kutoa pongezi Maalum kwa Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar. TRA na ZRB kwa kazi nzuri ya Makusanyo ya Kodi mbali mbali Nchini Balozi Seif alisema bado kuna upotevu wa Mapato unaosababishwa na udanganyifu wa baadhi ya walipa Kodi wakisaidiwa na baadhi ya Wafanyakazi wasio waaminifu wa Taasisi hizo.
Balozi Seif alirudia kusema kwamba Serikali haitamvumilia Mtu ye yote anayehujumu jitihada za Serikali za kuimarisha huduma kwa Wananchi na kuharakisha Maendeleo ya Taifa kwa kukidhi tu tamaa Binafsi.
“ Natamka leo hapa kwamba tutawachukulia hatua, iwe Mwekezaji, Mfanyabiashara au Mfanyakazi wa Taasisi yoyote ya Umma”. Aliendelea kuonya Balozi Seif.
Alitahadharisha kwamba Mapato lazima yakusanywe kwa ukamilifu kwa mujibu wa sheria na Taratibu zilizopo ili yaendelee kutumika  kwa madhumuni yaliyokusudiwa  ya kuwahudumia Wananchi walio wengi Nchini.
Akizungumzia suala la Amani na Demokrasia uliyopo Nchini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alsema Nchi inandelea kujivunia Uhuru na Demokrasia iliyopo ambapo imewawezesha Wananchi kushiriki katika shughuli zao za Kiuchumi na Kijamii bila ya matatizo.
Balozi Seif alisema Jamii imeshuhudia pia Viongozi wa Kisiasa wakiendesha harakati zao za kuimarisha Vyama vyao huku Serikali ikisimamiz utekelezaji wa Ahadi zilizotolewa na kuzitekeleza.
Alitoa wito kwa Viongozi na Wananchi wote kuendelea kuitunza Amani iliyopo pamoja na kudumisha Mshikamano ili waweze kwa pamoja kushiriki kikamilifu katika Ujenzi wa Taifa.
Aliwahakikishia Wananchi wote kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ziko makini katika usimamizi wa Amani hiyo na kamwe hazitosita kuwachukuliuwa hatua zinazostahiki wale wote watakaohusika katika uvunjani wa Amani hiyo.
Akigusia suala la Maafa ambalo Taifa pamoja na Wananchi limekuwa likiathiri mfumo mzima wa Maisha ya kawaida ya kila siku hasa katika kipindi cha masika kinachosababisha majanga Balozi Seif  upo mpango mdogo wa kukabiliana na maafa kabla na baada ya kutokea.
Alisema huduma zinazotarajiwa kutolewa katika mpango huo ni uratibu wa shughuli za kukabiliana na Maafa ikiwemo kutoa Mafunzo kwa Jamii, kuwahudumia waathirika wa Majanga na Maafa pamoja na kuandaa na kutoa miongozo inayosimamia utekelezaji wa kazi za kukabiliana na Maafa.
Balozi Seif alifahamisha kwamba katika muelekeo huo mafunzo Maalum ya kujikinga, kuandaa na kukabiliana na maafa kwa Watu 1,977 kutoka katika Makundi ya Jamii na Taasisi za Serikali na zisizo za Kiserikali  yatatolewa katika nia ya kuimarisha Sekta hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alizipongeza  Taasisi zisizo ya Kiserikali na Jumuiya ya Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Wakulima kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwahudumia Wananchi katika nyanja mbali mbali.
Alisema bila shaka uwezo, taaluma na rasilmali wanazotumia zimekuwa ni chachu kubwa katika kuiletea Maendeleo Jamii pamoja na Serikali Kuu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliliomba Baraza la Wawakilishi kuidhinisha Jumla ya Shilingi Bilioni 57,142,200,000/-  ambapo shilingi Bilioni 41,609,500,000/- kwa Kazi za kawaida na shilingi Bilioni 15,532,700,000/- kwa kazi za Maendeleo kwa  Programu zote 11 za Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na Taasisi zake zote kwa Mwaka wa fedha 2018/2019.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.