Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi leo imezindua rasmi sera ya Diaspora ya Zanzibar yenye lengo la
kujenga mazingira yatakayowaezesha wanadiaspora kushiriki na kuwafanya waweze
kutoa mchango wao kwa maendeleo ya Zanzibar.
Akizungumza katika hafla maalum ya
uzinduzi wa sera hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Mheshimiwa Issa Haji Ussi Gavu, amesema kuweko kwa sera hiyo hivi
sasa kutaiwezesha Serikali kuchukua hatua mbali mbali za kisekta ambazo
zitaelezea na kutoa maelekezo kuhusiana na masuala muhimu ya Diaspora na
maendeleo ya Zanzibar.
Amefahamisha kuwa kufuatia uzinduzi
huo, Serikali hivi sasa itakuwa na fursa nzuri ya kuwashajihisha Wanadiaspora
wote kushiriki katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi, sambamba na kuainisha
fursa na wajibu wa wanadiaspora wa Zanzibar popote walipo.
Katika utekelezaji wa sera hiyo,
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaijengea uwezo Idara inayoshughulikia masuala
ya Diaspora kwa kuipatia wataalamu, nyenzo za kutekeleza majukumu yake pamoja
na kuifanya kuwa kituo muhimu cha kupata taarifa zinazohusiana na masuala ya
Diaspora.
Vile vile Mheshimiwa Gavu amesema
kuzinduliwa kwa sera hiyo kutaiwezesha Serikali kusimamia kikamilifu taarifa
zinazohusiana na masuala ya Diaspora na kuwashirikisha rasmi wanadiaspora kwa
lengo la kurahisisha kujenga imani na kuimarisha mashirikiano kati yao na
Serikali.
Aidha, Serikali kupitia sera hiyo inakusudia
kutumia taaluma na ujuzi wa wanadiaspora kwa maendeleo ya Zanzibar na kuratibu
masuala ya utumaji wa fedha kutoka kwa wanadiaspora kwani amesema, fedha hizo
zinachangia sehemu kubwa katika jitihada za maendeleo.
Sambamba na hatua hiyo, Serikali itawatumia
wanadiaspora katika jitihada za Uwekezaji Vitega Uchumi pamoja na kuimarisha
sekta ya Utalii ambayo imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika kuchangia pato la
taifa.
Hafla hiyo ambayo ilifanyika katika
ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi uliopo Kikwjuni Mjini Zanzibar,
ilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Salum Maulid Salum, Wanadiaspora wa Zanzibar na Waandishi mbali mbali
wa habari waliopo Zanzibar.
Akimkaribisha Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Salum Maulid
Salum amesema kuzinduliwa kwa sera hiyo ni matunda ya jitihada za muda mrefu za
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kujenga mafahamiano mazuri kati ya
Serikali na Wanadiaspora.
No comments:
Post a Comment