Habari za Punde

Ifahamu Sera ya Diaspora Zanzibar


DIBAJI

#Sera ya Diaspora ya Zanzibar inafafanua misingi ya kufaidika na michango ya Wanadiaspora wa Zanzibar kwa maendeleo ya Zanzibar kiuchumi na kijamii, wakati huo huo inaweka wazi mahitaji yao kwa kuweka utaratibu mzuri utakaosaidia kujenga uaminifu na utakaowavutia Wanadiaspora hao kuimarisha mahusiano na Nchi Yao ya asili.

# Kazi ya kuandaa Sera hii ilifanywa na Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kupitia vikao vya kukusanya maoni kutoka kwa Wanadiaspora wenyewe na kupata mapendekezo muhimu yaliyosaidia katika kutengeneza Sera hii. Aidha, mchakato wa kutayarisha Sera hii uliendelea kwa kufanya mapitio ya nyaraka rasmi na zisizo rasmi zilizochapishwa zenye uhusiano wa moja kwa moja na Sera hii.Vile vile, majadiliano yalifanywa katika makundi maalum, watu mbalimbali mashuhuri Serikalini, Taasisi Binafsi, Asasi za Kiraia, Wanadiaspora waliorejea nyumbani na hatimae kwa wanachama wa Jumuiya za Diaspora.
# Masuala ya Diaspora Yana umuhimu mkubwa na yanafahamika kuwa ni nguzo muhimu katika maendeleo ya nchi. Hii ndio sababu iliyopelekea kuliingiza suala hili katika Sera na hatimae kuingizwa rasmi katika mikakati ya maendeleo ya Zanzibar.
# Sera hii imeweka Dira, Dhamira, malengo na muundo wa kitaasisi uliowazi na utakaowezesha Diaspora kwa ufanisi mkubwa kuchangia maendeleo ya nchi yao ya asili.

# Serikali imejizatiti kuhakikisha kuwa Sera ya Diaspora ya Zanzibar inatekelezwa kwa ufanisi na inatoa matokeo yaliyokusudiwa.

# Katika kuhakikisha utekelezaji wa Sera ya Diaspora ya Zanzibar unafanikiwa, uwekaji wa mazingira mazuri na uanzishaji mfumo bora zaidi wa kisheria katika uendeshaji wa suala la Diaspora ni jambo la msingi.

# Kwa kuzingatia hilo, Serikali itahakikisha Idara inayosimamia Wazanzibari wanaoishi nje ya Nchi inafanya kazi kwa kushirikiana na wadau wengine katika kufuata taratibu zilizowekwa na Sera.

# Muda uliopangwa kufikia lengo unahitaji kuchungwa vizuri na kuwekewa miundombinu mizuri kwa ajili ya ufuatiliaji na tathimini.

# Pamoja na Utangulizi, Sera hii kwa ujumla ina sehemu kuu tano; 


Sehemu ya kwanza inaelezea historia na hali halisi ya Diaspora wa Zanzibar, Dira, Dhamira, Tunu na Miongozo ya Sera. 

Sehemu ya pili ya Sera inafafanua Diaspora wa Zanzibar.

Sehemu ya tatu inaonesha Mantiki na Malengo ya Sera. 

Sehemu ya nne inatoa Matamko ya Kisera na Mikakati na Malengo ya Sera. 

Sehemu ya tano na ya mwisho,  inaelezea kazi na majukumu ya Taasisi mbalimbali ambazo ni wahusika katika utekelezaji wa Sera hii na mapendekezo ya taratibu za ufuatiliaji na tathimini yake.


# Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi inawashukuru Wahusika wote, Taasisi na watu binafsi waliochangia katika kuifanikisha Sera hii ya Diaspora Zanzibar.

# Matarajio yetu ni kwamba matokeo ya utekelezaji wa Sera hii yatasaidia katika kuonesha umuhimu wa Wanadiaspora katika kuchangia maendeleo ya Nchi yao na vile vile kuimarisha ukuaji na ustawi wa Wanadiaspora.

DIBAJI HII IMETOLEWA NA :-

WAZIRI WA NCHI OFISI YA RAIS NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHE ISSA HAJI USSI GAVU

IMEANDALIWA NA :-

IDARA YA HABARI ( MAELEZO) ZANZIBAR 
MEI 9, 2018

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.