Habari za Punde

Waziri wa Michezo Vijana Utamaduni na Sanaa Awasilisha Hutuba ya Bajeti ya Wizara Yake leo.

Na Khadija Khamis  -Maelezo.
Waziri wa Vijana Utamaduni Sanaa na Michezo Balozi Ali Karume amesema Wizara yake inatarajia kutoa mafunzo na kuwasaidia vijana katika shughuli za Kilimo, Uvuvi, Biashara, Elimu ya Stadi za Maisha na Amali ili kuwawezesha vijana  kiuchumi na kijamii.
Hayo aliyaeleza wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Vijana Utamaduni Sanaa na michezo  ya mwaka 2018-2019 huko katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani.
Alisema lengo la mpango huo ni kuwasaidia vijana  kuweza kuratibu shughuli za maendeleo ya vijana ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kujiimarisha kiuchumi, kijamii na kisiasa na kuengeza  idadi ya ajira kwa vijana.
Aidha alisema katika kuufanikisha mpango huo ni kuhakikisha  wizara inautekeleza kwa ufanisi imepangiwa jumla ya shilling 457,448,000 ili kuwajengea uwezo vijana kiuchumi na kimaendeleo katika jamii.
Alifahamisha katika mpango huo ni pamoja na kusimamia uendelezaji wa Mabaraza ya Vijana katika ngazi zote na  kuyaendeleza mabaraza hayo kiuchumi ili kuhakikisha yanakuza ajira kwa vijana pamoja na kuratibu shughuli za mwenge wa uhuru kitaifa .
Alieleza katika kufanikisha hayo Wizara imejipanga kuyawezesha Mabaraza hayo kuwa na Ofisi ,Wafanyakazi pamoja na vifaa vya kufanyia kazi na  kufanyika mikutano yote ya mabaraza ya vijana kwa mujibu wa sheria pamoja na kuwajengea uwezo vijana kuweza kushiriki katika ngazi ya kutoa maamuzi katika Serikali na sekta binafsi.
Balozi Ali alisema katika kufanikisha hayo kumewekwa mpango wa kuimarisha huduma vifaa elimu na mazingira bora ya kazi kwa taasisi zinazotekeleza programu hii.
Hata hivyo Waziri huyo alisema katika programu kuu :SO102  ya Maendeleo ya Utamaduni Sanaa na michezo ina jukumu la kuhakikisha kuwa Utamaduni na Sanaa ya Zanzibar inawaendeleza wasanii kiuchumi ili kupunguza umasikini na kuifanya michezo kuwa ni sehemu ya  kujenga afya na ajira kwa jamii.
Alifahamisha kuwa matokeo ya muda mrefu ya programu hii ni kuwepo kwa soko la kazi za Sanaa ,uhifadhi wa utamaduni na kukuza michezo program hii imepangiwa jumla ya shilling 2,049,626,000.
Aidha alisema katika kufanikisha malengo shughuli mbalimbali zimepangiwa kutekelezwa zikiwemo kuandaa,kusimamia na kuratibu matamasha yote ya kiutamaduni pamoja na kulinda mila desturi na silka za wazanzibari kwa kushirikiana na jamii.
Alifafanua kuwa kusimamia kuhamasisha pamoja na kutoa elimu kuhusiana na matumizi bora ya lugha ya Kiswahili na lahaja zilizopo pamoja na kukiimarisha kikundi cha Taarabu cha Taifa na Vikundi vyengine vya Sanaa  .
Alisema katika kufanikisha mipango hiyo ni pamoja na kuwasaidia wasanii kwa kuwapa mafunzo mbali mbali ya  kuwaendeleza kiuchumina kupata fursa ya  kuendelea kuitumia studio ya muziki na filamu pamoja na kuwawekea mazingira bora ya kukuza sanaa zao .
Aidha alisema ni jukumu la Taasisi ambazo zinasimamia program hii ni  kusajili, kusimamia, kulinda kazi na haki za wasanii na wabunifu wa kazi mbali mbali pamoja na kuwapatia mirabaha yao na kuimarisha huduma vifaa elimu na mazingira bora ya kazi .

MWISHO
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.