Habari za Punde

Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar Kuongeza Posho la Wanafunzi Wanaosoma Nje.

Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar.
Bodi ya Mikopo Zanzibar itaongeza posho kwa wananfunzi wanaosoma nje ya Zanzibar kuanzia bajeti ya mwaka 2018/2019 ili kuwaondoshea usumbufu wanafunzi wanapokuwa masomoni.
Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar Iddi Khamis Haji ameeleza hayo Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Amani Abeid Karume wakati wa kuwapokea wanafunzi 11 waliomaliza shahada ya kwanza ya uandishi wa habari kwa kutumia lugha ya Kichina.
Alisema Serikali imekuwa ikijitahidi kuwapatia posho wanafunzi wanaosoma nje  ili kukidhi mahitaji yao  ingawa baadhi ya wakati zimekuwa zikichelewa lakini kuanzia Bajeti ijayo Serikali imejipanga na itaongeza posho na kuwatumia kwa wakati.
Mkurugenzi Iddi alisema Zanzibar ilitumia shilingi million 215 kwa wanafunzi hao 11 katika kipindi cha miaka minne walipokuwa nchini humo kwa nauli ya kwenda na kurudi China na posho la kujikimu kwa chakula na Serikali ya China iligharamia masomo, makaazi, huduma za afya na huduma nyengine za lazima.
Alifahamisha kuwa hivi sasa kuna wanafunzi 34 wanaoendelea na masomo ya shahada ya kwanza kwa lugha ya Kichina nchini humo na mwaka huu wanatarajia kupeleka wanafunzi wengine 10 na amewataka vijana wenye sifa ikiwemo kujua lugha ya kichina kuomba nafasi hizo.
Alieleza kuwa wameanza mazungumzo na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China  ili wanafunzi wanaomaliza shahada ya kwanza waweze kujiunga na masomo ya shahada ya pili na wameonyesha nia ya kukubali ombi hilo.
Wanafunzi hao wamesema kipindi chao cha miaka minne ya masomo nchini China  kilikuwa kizuri licha ya changamoto ndogo ndogo zilizojitokeza ikiwemo kumudu kuitumia lugha ya Kichina katika masomo, ufinyu wa fedha pamoja na kuchelewa  fedha na hali ya hewa ya huko.
Waliiomba serikali kuwaangalia katika suala la ajira ili wapate nafasi ya kuutumia  ujuzi walioupata  wa lugha ya Kichina na uandishi wa habari hasa wakati huu ambapo soko la watalii kutoka China linaongezeka.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.