Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Afanya Ziara Kutembelea Mashamba ya Mpira Zanzibar.

 Balozi Seif akisisitiza jambo wakati akiiongoza Kamati ya Baraza la Mapinduzi ilipofanya ziara katika Mashamba ya Mipira Kichwele Mkoa wa Kaskazini Unguja.



Na.Othman Khamis OMPR.
Kamati  Maalum iliyoteuliwa na Baraza la Mapiznduzi Zanzibar ikiongozwa na Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi imefanya ziara maalum ya kuyakagua Mashamba ya Mipira  yaliyopo Unguja ili kutambua hali halisi ya ukubwa wa maeneo yake pamoja na mazingira yaliyomo ndani yake.
Wajumbe wa Kamati hiyo ambao ni pamoja na Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na baadhi ya Maafisa wa Taasisi za Serikali walipata wasaa wa kukutana na Wakulima waliowahi kufanyakazi kwenye Mashamba hayo Kichwele chini ya usimamizi wa Kampuni ya Agro Tex ambayo imefilisika kuendesha mradi huo.
Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar akiwa miongoni mwa Wajumbe wa Kamati hiyo Dr. Khalid Salum Mohamed aliwaeleza Wakulima hao kwamba  Serikali Kuu imefikia uamuzi wa Mashamba hayo kurejeshwa Wizara ya Kilimo ili kuangalia muelekeo wa matumizi mbadala hapo baadae.
Dr. Khalid alisema hatua hiyo imekuja baada ya Kampuni iliyoingia Mkataba na Serikali  ya Agro Tex kusitisha shughuli zake kabla ya kufikia Muda  halisi wa Miaka Minne ambapo matokeo yake kuacha madeni makubwa kwa Serikali, Benki ya Watu wa Zanzibar {PBZ} pamoja na waliokuwa Wafanyakazi wa Mashamba ya Mipira.
Alisema kwa mujibu wa Sheria na taratibu za Mikataba ya Uwekezaji inavyofungwa na kufikiwa, Serikali Kuu hulazimika kuagiza kufilisiwa kwa Mali zote za Muwekezaji  husika pale anaposhindwa kuendeleza Mkataba alioukubali kabla jambo ambalo Kampuni ya Agro Tex haikuwa na Mali ya kufidia.
Waziri wa Fedha alisema wafanyakazi wa iliyokuwa Kampuni ya Agro Tex wameumia sana na kuwaomba kuendelea kuwa na moyo wa uvumilivu huku Serikali ya Mainduzi ya Zanzibar ikiendelea kutafuta  namna ya kusawazisha Madeni hayo.
“ Madeni na Mikopo lazima itafutiwe utaratibu wa kusawazishwa hasa ikizingatiwa kwamba Wananchi hasa wale Wafanyakazi wa Kiwanda cha Mipira Kichwele wameumia sana lakini bado wanapaswa kuendelea kuvumilia ”. Alisema Dr. Khalid.
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo Maalum Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ziara yao imekuja kufuatia agizo la Baraza la Mapinduzi la kuitaka kuyakagua maeneo yote ya mashamba ya Mipira baada ya Kampuni ya Agro Tex kushindwa kuyaendeleza.
Balozi Seif alisema wakati Serikali Kuu ikiendelea kutafakari hatma ya Mashamba hayo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imepewa jukumu la kuandaa utaratibu wa Kisheria utakaotoa muelekeo halisi wa matumizi ya Mashamba hayo kwa hapo baadae.
Alisema Serikali inaelewa hali halisi ya mazingira ya kimaisha wanayopambana nayo Wananchi hao hasa katika kipindi chote ambacho Muekezaji wa mradi huo Agro Tex kusimamisha moja kwa moja  shughuli za uzalishaji huku akiacha madeni makubwa.
Mapema Meneja wa Shamba la Mipira Ndugu Ngwali Makame Haji alisema Mashamba ya mipira  yenye ukubwa wa Hekta 1,200 Unguja na Pemba yalianzishwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar  mnamo Mwaka 1977 na kuanza rasmi uvunaji  wa Utomvu Mwaka 1984.
Nd. Ngwali alisema kufuatia hatua ya Serikali kukaribisha miradi ya Uwekezaji Nchini kutoka  kwa Taasisi na Makampuni ya Nje Mashamba ya Mipira yalianza kukodishwa kwa zaidi ya Makampuni Manne kuanzia Mwaka 2004 hadi 2017.
Meneja huyo wa Shamba la Mipira aliufahamisha Ujumbe wa Kamati hiyo kwamba Wizara ya Kilimo hivi sasa inaendelea kulisafisha eneo la Hekta 187 za Miti ya Mipira kwa lengo la kufidia lile lililochukuliwa na Serikali kwa ajili ya Uchimbwaji Mchanga  huko Mahonda.
Nd. Ngwali alieleza kwamba licha ya kwamba hivi sasa hakuna shughuli zozote zinazoendelea kwenye Mashamba hayo lakini zipo changamoto zinazojichomoza kwenye mashamba hayo ambazo kama hazikuchukuliwa hatua zinaweza kuleta athari hapo baadae.
Alisema baadhi ya changamoto hizo alizitaja kuwa ni pamoja na wingi wa magugu kwenye Mashamba hayo, ukataji ovyo wa Miti na baadhi ya wakulima  wapatao 200 kulima mazao madogo madogo katika Hekta 137 za Mashamba tofauti ya Mipira.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati Maalum ya kukagua Mashamba ya Mipira  ni pamoja na Waziri wa Fedha Dr. Khalid Salum Mohamed, Waziri wa Nchi anayesimamia Tawala za Mikoa Mh. Haji Omar Kheir, Waziri wa Biashara  Balozi Amina Salum, Waziri wa Ardhi Mh. Salama Aboud pamoja na Waziri wa Kilimo Mh. Rashid Ali Juma.
Wengine ni Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Manaibu Makatibu Wakuu pamoja na Wakurugenzi, Mameneja na Maafisa wengine waliomo ndani ya  Wizara hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.