Habari za Punde

Tuzo ya Kiswahili ya Heshima ya Shaaban Robert Kuanza Kutolewa Mwakani.

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Tuzo ya Kiswahili ya Heshima ya Shaaban Robert inategemea kuanza kutolewa mwaka 2019 na Kampuni ya Maendeleo ya Kiswahili (KIDE - MAKI) kwa watu mbalimbali wanaoendelea kuienzi na kuikuza lugha ya Kiswahili.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amethibitisha hayo leo kwenye uzinduzi wa kumbukizi ya Shaaban Robert na Tamasha la Ustaarabu wa Mswahili uliofanyika katika ukumbi wa Baraza la Chuo cha Mt. John jijini Dodoma.
Dkt. Mwakyembe amesema kuwa tuzo hizo zitatolewa katika tamasha Kubwa la ‘Ustaarabu wa Mswahili’ litakalokuwa likifanyika kwa siku tatu za mwezi Januari kila mwaka.

“Tuzo hizo zitatolewa katika kilele cha tamasha hilo ambapo watu na taasisi mbalimbali zilizojipambanua kipekee katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili zitatunukiwa”, alisema Dkt. Mwakyembe.

Dkt. Mwakyembe ameongeza kuwa Serikali inaunga mkono juhudi zinazofanywa na wadau wa lugha ikiwemo Kampuni hiyo katika mambo yanayolenga kukuza, kueneza na kuendeleza lugha nchini.

Pia amefafanua kuwa juhudi hizo ni moja ya utekelezaji wa sera hivyo kinachotakiwa sasa ni ubidhaishaji wa lugha ya Kiswahili ili kiendelee kuleta manufaa na kuongeza tija kwa wananchi.

Akiongelea kuhusu Kumbukizi ya Hayati Shaaban Suleimani Juma Ufukwe (Shaaban Robert), Dkt. Mwakyembe amesema kuwa juhudi zake zimechangia sana kukua kwa lugha ya Kiswahili ambapo kwa hivi sasa ni lugha ya 10 kati ya lugha 6000 zinazozungumzwa duniani.
“Chemchem za mawazo yake, tifutifu za mielekeo yake, mboji za maarifa na mafunzo ya nguli na jabali wa Fasihi ya Kiswahili bado yanatuongoza vema hata leo katika maono ya nchi yetu ya kuwa na uchumi wa kati kupitia Tanzania ya viwanda”, alisema Dkt. Mwakyembe.
Aidha katika kumbukizi hiyo, Waziri Mwakyembe amezindua kitabu cha “Historia ya Kiswahili kwa Mtazamo Mpya” kilichotungwa na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo ambaye amebobea katika uandishi wa vitabu vya kifasihi, Prof. David Massamba.
Kitabu hicho kinatoa ufafanuzi wa kina kuhusu historia na asili/chimbuko la lugha ya Kiswahili na Waswahili na kuziba mapengo ya kuwepo kwa mkanganyiko au ukinzani wa wanazuoni mbalimbali kuhusu historia na asili  ya lugha ya Kiswahili na Mswahili ambao umedumu kwa muda mrefu sana.

Shaaban Robert alikuwa ni mwandishi nguli wa vitabu vyenye maudhui mbalimbali vikiwemo vya Kusadikika, Kufikirika pamoja na Adili na Nduguze, alizaliwa Januari Mosi, 1909 na kufariki June 22,1962.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.