Habari za Punde

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Amani Unguja Mhe. Abdi Ali Mzee Mrope, Amewataka WanaCCM Kuimarisha Ushirikiano Ndani ya Chama.

Na Mwashungi Tahir      Maelezo  Zanzibar.
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Amani Abdi Ali Mzee Mrope amewataka wanachama wa Chama hicho kuwa na mashirikiano ili waweze kuimarisha na kukijenga kwa madhumuni kupata nguvu na kiweze kusonga mbele.
Hayo aliyasema  huko katika ukumbi wa Tawi la Kilimani wakati alipokuwa akizungumza na wajumbe wa halmashauri kuu na wajumbe wa kamati ya siasa wa tawi hilo ikiwa ni miongoni mwa ziara yake ya kutembelea matawi kwa lengo la kukagua uhai wa chama katika wilaya yote.
Alisema lengo la ziara hiyo  ni kuimarisha chama  na kujenga mshikamano  katika chama hichi  na  iwapo kutakua na wanachama watakuwa na  mashirikiano mazuri chama chetu kitaimarika zaidi na kuweza kupata ushindi kwa kishindo ifikapo 2020.
Pia mwenyekiti huyo aliwataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi wawe na mashirikiano  na kuimarisha vijana kwa kuwasomesha madarasa ya itikadi  kwa lengo ya kuwakusanya pamoja na kuwahamasisha  kwenye chama.
Aliwaomba wanachama walipe ada kwa lengo la kukikuza chama  na kuendeleza mshikamano kwani ndio ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi na kuwataka wabunge na wawakilishi  washuke  majimboni kwa lengo la kuwasikiliza wanachama wao.
“Tuendeleze mshikamano wetu  kwani ndio njia ya mafanikio zaidi ya kufanya chama kisonge mbele na kuweza kuleta maendeleo zaidi”. Alisema Mrope.
Aidha alitoa wito  kwa kusema ushindi unakuja  kwa kujipanga ngazi zote ikiwemo shina , wadi , tawi hadi kufikia Makao Makuu  na huo ndio utaratibu wa chama chetu.
Nae Mwakilishi wa Jimbo La Mpendae Mohammed Said Dimwa aliwaomba wanachama cha Mapinduzi kutekeleza Ilani ya chama kwa lengo la kufanikiwa majukumu yake.
Vile vile aliwaomba wananchama kuzingatia majukumu yetu kwa kukikuza chama na kuwataka ziara hii kujitokeza kwa wingi katika matawi yetu ili tuimarishe na kupelekea kupata mafanikio zaidi.
Sambamba na hayo  mjumbe wa kamati ya siasa wilaya ya Amani Hariri Abdullah Bori alisema shughuli za chama haziwezi kuimarika bila ya kuwa na vikae katika matawi yetu na kuelekezana kazi zet kwani bila ya vikao hatuwezi kufanya shughuli zetu kwa Ufasaha.
Ziara hiyo itahusisha mambo yafuatayo ikiwemo   kuimarisha vikao, ulipaji wa ada , kuingiza wanachama wapya katika chama na kuziimarisha maskani kwa lengo la kuzidisha uhai wa chama.
Mwisho.
Imetolewa na Idara ya Habari Maelezo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.