Habari za Punde

Ufaransa Waibuka Kidedea Kombe la Dunia 2018.


Fainali za kombe la dunia 2018, zilizoanza Juni 14, hatimaye zimefika tamati leo Julai 15 huko nchini Urusi kwa Ufaransa kuibuka mabingwa kwa ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Croatia kwenye mchezo wa fainali uliomalizika usiku huu.

Mabao ya Ufaransa leo yamefungwa na Antoine Griezmann, Paul Pogba, Kylian Mbappé na lile la kujifunga la Mario Mandžukić huku ya Croatia yakifungwa na Ivan Perisic na Mario Mandžukić ambaye amekuwa mchezaji wa kwanza kujifunga na kufunga kwenye mchezo wa fainali.

Ufaransa imefanikiwa kutwaa taji lake la pili baada ya kutwaa la kwanza mwaka 1998, miaka 20 iliyopita ambapo moja ya wafungaji wa mabao ya Ufaransa leo Kylian Mbappé alikuwa hajazaliwa na leo akiwa na miaka 19 na siku 207, amekuwa mchezaji wa pili mdogo kufunga bao kwenye fainali ya kombe la dunia akitanguliwa na Pele ambaye alifunga mwaka 1958 akiwa na miaka 17 na siku 249.

Akiwa na kumbukumbu ya kuwa nahodha wa kikosi cha Ufaransa kilichotwaa ubingwa mwaka 1998, kocha wa Ufaransa Didier Deschamps, amekuwa binadamu wa tatu kuchukua kombe la dunia akiwa kama mchezaji na kocha, baada ya Mario Zagallo wa Brazil na Franz Beckenbauer wa Ujerumani. 

Baada ya mchezo kumalizika shirikisho la soka la kimataifa FIFA, limemtangaza mchezaji Luka Modrić wa Croatia kuwa mchezaji bora wa mashindano ikiwa ni mara ya pili mfululizo kwa tuzo hiyo kwenda kwa mchezaji ambaye tmu yake imefungwa baada ya Lionel Messi mwaka 2014.

Mbappe tena ambaye amekuwa na wakati mzuri katika fainali hizi akifunga mabao manne, ametangazwa kama mchezaji bora kijana wa mashindano. Thibaut Courtois wa Ubelgiji ameibuka mlinda mlango bora wa mashindano.

Naye mshambuliaji wa England Harry Kane ameibuka mfungaji bora wa fainali za kombe la dunia mwaka 2018, baada ya kufunga mabao 6 idadi sawa na mfungaji bora wa fainali za mwaka 2014 James Rodríguez.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.