Habari za Punde

McCain: Simba Aliyepigana Vita Hadi Mwisho

Na.Anthony Zurcher, mwandishi wa BBC Amerika Kaskazini.
John McCain alizaliwa mnamo 29 Agosti, 1936 Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vikiwa vimekaribia, mwanzoni mwa 'Karne ya Marekani', wakati ambapo Marekani ilikuwa kileleni kisiasa, kijeshi na kitamaduni.
Ni kuanzia wakati huo ambapo Marekani ilianza kuwa taifa kuu duniani hasa baada ya vita hivyo.
Amefariki katika kipindi ambacho kinatazamwa kama mwanzo wa mwisho wa ubabe wa Marekani, wakati ambao taifa hili linaanza kujifikiria ndani badala ya nje, linafikiria kujenga ukuta kuwazuia wahamiaji wasiingie ndani, na kimsingi linatafakari kujikinga dhidi ya ulimwengu.
Maisha ya seneta huyo kutoka Arizona yanaakisi safari hii ya Marekani.
Aliteseka, na taifa lake liliteseka, kutokana na vita vya Vietnam.
Kama mwanasiasa wa umri mdogo, alijaribu kushawishiwa na mamlaka na pesa, na alipatikana katika sakata ya kujipatia ushawishi na umaarufu ambayo karibu ikatishe maisha yake ya kisiasa.
Mara ya kwanza alipojaribu kuwania urais mwaka 2000, alijaribu kutumia wimbi la watu kutoridhishwa na watala na watu waliodhibiti siasa kwa muda mrefu. Alijaribu kuvutia hisia za Wamarekani za kutaka uhalisia, mtu aliyeakisi matamanio yao.
Hilo lilitimia katika kuchaguliwa kwa Donald Trump mwaka 2015.
Mwaka 2008, aliteuliwa na chama cha Republican kuwania urais, lakini hakuweza kuhimili wimbi la Barack Obama, mgombea wa kwanza mwenye asili ya Afrika, pamoja na hali kwamba uchumi wa Marekani ulikuwa unaporomoka.
McCain hakufanikiwa kushinda urais alivyotamani.
Maishani mwake, alikuwa anaitetea Marekani ambayo inashiriki kikamilifu katika shughuli za dunia.
Miaka yake ya mwisho, alitofautiana vikali na Trump kuhusu mwelekeo wa chama cha Republican na maadili yaliyofaa kukumbatiwa na chama hicho.
Ni swali wazi kuhusu iwapo mtazamo kama wake una matumaini katika chama hicho.
McCain hata hivyo alilipigania lile aliloamini lilikuwa kweli na la haki. Kubaliana naye au usikubaliane naye, lakini huo ni ujumbe tosha kuwa kwenye kaburi lake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.