Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba
akisalimiana na Bw. Khatib Ally mmoja wa wananchi waliojitokeza kumpokea katika
Kijiji cha Aghondi Wilayani Manyoni, Mkoani Singida. Waziri Makamba ametembelea
eneo hilo ambalo lina vichaka vya aina yake na vyakipekee barani Afrika. Wananchi
wa eneo hilo wamewasilisha ombi kwa Waziri Makamba la kuweka ulinzi wa kutosha
na namna bora ya kuhifadhi eneo hilo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Yussuf Makamba ,akimsikiliza Mwananchi anayeshughulikia na uhifadhi wa msitu wa hifadhi ya vichaka vya Itigi, huutumia msitu huo kwa ufugaji wa nyuki na kuvuna asili nyingi kupitia msitu huo.
Sehemu ya
vichaka adimu duniani vinavyopatikana Itigi, “Itigi thickets” katika bara la
Afrika vichaka kama hivyo vinapatikana Tanzania na Zambia pekee, viko hatarini
kutoweka kutoweka kutokana na shughuli
za kibinadamu.
Na.Lulu Mussa.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mheshimiwa January
Makamba hii leo amehitimisha ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Singida na
kuwasili katika Mkoa wa Tabora, ikiwa ni mwendelezo wa kukagua, kutathmini,
kuzungumza na viongozi, na wananchi kuhusu maeneo yanayopendekezwa kuhifadhiwa
kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira, sambamba na uanzishwaji na ufuatiliaji utekelezaji
wa Sheria ya Usimamizi Mazingira ya mwaka 2004 katika ngazi za Serikali za
Mitaa.
Katika
siku ya tatu ya ziara yake Mhe. Makamba ametembelea vichaka vya Itigi ‘Itigi
thicket” na kupata fursa ya kuzungumza na viongozi wa wilaya ya Manyoni juu ya
namna bora ya kuhifadhi eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 410,000 na kuahidi
kutuma wataalamu kuandaa andiko la Mradi utakaonufaisha wakazi wa eneo hilo
katika sekta uvunaji wa asali kwa njia ya kisasa zaidi.
“Ndani
ya muda mfupi nitatuma wataalamu wangu kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira NEMC, waje wakae na wataalamu wenu na kuandaa Mradi
utaonufaisha wakazi wa wanaozunguka eneo lote la msitu ili kutunza na kuhifadhi
rasilimali za asili zilizopo katika eneo hili” Makamba alisisitiza.
Katika
hatua nyingine Waziri Makamba amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Bi. Rahabu Jackson
kuwasilisha kwake majina wa watalaamu wa Mazingira ambao wana sifa za kuwa
Wakaguzi wa Mazingira ili waweze kuteuliwa kwa mujibu wa Sheria.
Pia,
ametoa wito wa Halmashauri kuingia makubaliano na Baraza la Taifa la Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ili kukasimu mamlaka kisheria ya kukagua na
kusimamia masuala ya mazingira kwa msukumo zaidi.
Vichaka
vya Itigi huwa na urefu wa mita 2-5 na katika Bara la Afrika vinapatikana
Tanzania na Zambia pekee vinawakilisha bioanuani ya kipekee duniani yenye
umuhimu kitaifa na kimataifa na uoto wake ni muhimu kwa mustakabali wa maisha ya binadamu
na wanyamapori.
Imebainika
kuwa vichaka vya Itigi viko hatarini kutoweka kutokana na shughuli za
kibinadamu kama vile kilimo cha kuhamahama, uchungaji wa mifugo, uchomaji wa
mkaa, uvunaji wa mazao ya misitu na uchimbaji wa madini. Hivyo kuna haja ya
kuchukua hatua za haraka kuhakikisha uhifadhi endelevu wa vichaka vya Itigi.
No comments:
Post a Comment