Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Issa Haji Gavu akifungua Mafunzo ya Siku Kumi kwa Wahudumu wa Viongozi na Wageni Zanzibar, Mafunzo hayo Yanatolewa na Wakufunzi kutona Taasisi ya China Natinal Research Institute of Food and Fermentation Industries Corporation Ltd.(CNRIFFI) uzinduzi huo umefanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amepongezwa kwa juhudi anazoendelea kuzichukua katika
kuhakikisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakuwa na wataalamu na nguvu
kazi yenye ujuzi na inayokwenda sambamba na mahitaji na mabadiliko ya karne ya
21.
Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi Gavu alitoa pongezi
hizo katika hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo ya Mapishi na Ukarimu yanayoendeshwa
na wakufunzi kutoka China, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa
Abdulwakil, Kikwajuni mjini Zanzibar.
Katika maelezo yake, Waziri
Gavu alieleza kuwa juhudi za Rais Dk. Shein zinafahamika katika kuhakikisha
kwamba kunakuwepo ushirikiano mzuri kati ya Zanzibar na Washirika wa maendeleo
katika suala zima la utoaji wa mafunzo na kuwajengea uwezo wafanyakazi katika
sekta zote muhimu za kiuchumi na kijamii hapa nchini.
Alitumia fursa hiyo
kutoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kukubali kuendelea
kutoa mafunzo hayo kwa kuzingatia ombi maalum kutoka kwa Rais Dk. Shein mara
baada ya kufanya mazungumzo na Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Xie
Xiaowu.
Alisema kuwa mafunzo
hayo ni miongoni mwa matunda ya jitihada za Rais Dk. Shein na kila mmoja
anathamini sana fursa hiyo inayotokana na juhudi zake katika kuwajengea uwezo
wafanyakazi.
Waziri Gavu aliwaeleza
washiriki wa mafunzo hayo wkamba wanaunga mkono kwa ukamilifu, maamuzi na
makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wa pande zote mbili ya kuendesha mafunzo
hayo hapa Zanzibar ili kuweza kutoa fursa ya kushiriki watendaji wengi zaidi
kwa mkupuo mmoja.
Aliongeza kuwa mwaka
huu wa 2018 wapo washiriki 50 na mwaka jana 2017 mafunzo hayo yalishirikisha
watendaji 30 hali ambayo ni ya kupiongezwa na inaonesha mafanikio makubwa kwa kuendesha
mafunzo hayo hapa Zanzibar ambapo itawapa fursa ya kufahamu masuala
watakayofundishwa katika mazingira ya nyumbani waliyoyazoea na wanayoyafanyia
kazi.
Aidha, Waziri Gavu
alitoa shukurani za dhati kwa Taasisi ya “China National Research Institute of
Food and Fermentation Industries Corporation Ltd” kwa kuendeleza ushirikiano
mzuri uliopop baina ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
na hatimae kukubali kuja tena hapa
Zanzibar kwa ajili ya kuendesha na kusimamia mafunzo.
“Jamhuri ya Watu wa
China na Zanzibar zina uhusiano wa kihistoria na kidugu, tuna jukumu la
kuhakikisha kwamba ushusiano huo unalindwa na kuendelezwa...njia moja ya
kufanya hivyo ni kuhakikisha kwamba tunashiriki vizuri katika mafunzo haya na
tunawapa wenzetu hawa mashirikiano yanayohitajika”,alisema Waziri Gavu.
Sambamba na hayo,
Waziri Gavu aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kujua kwamba wana jukumu la
kutoa huduma moja kwa moja kwa viongozi, wageni na watalii au kutoa mafunzo kwa
wanafunzi wanaotarajia kwenda kutoa huduma za aina hiyo baada ya mafunzo yao.
Aliwahimiza kuzingatia
kwa umakini mkubwa mambo watakayofundishwa ili waweze kwenda kuyatekeleza mambo
hayo kivitendo katika sehemu zao za kazi huku wakijiamini kwa kutoa michango na
kuuliza masuali kila wanapohisi hawajafahamu au wanapoona ipo haja ya kufanya
hivyo kwa faida ya washiriki wengine.
Nae Balozi Mdogo wa
China anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Xie Xiaowu alitoa pongezi kwa
kufunguliwa mafunzo hayo na kueleza kuwa China itaendelea kuiunga mkono
Zanzibar katika kuendeleza sekta mbali mbali za maendeleo yakiwemo mafunzo ya
ndani na nje ya nchi.
Alieleza kuwa Chuo
hicho kinachotoa mafunzo hayo kimeanza zoezi hilo kwa nchi zinazoendelea tokea
mwaka 2005 na kueleza kuwa tayari wameshaendesha mafunzo kwa watu wapatao 4600
kutoka nchi 133 zinazoendelea hadi mwishoni mwa Agosti mwaka huu 2018.
Balozi huyo alitumia
fursa hiyo kwa kutoa pongezi kwa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi kwa kusimamia vyema mafunzo hayo.
Pamoja na hayo, Balozi
Xie alieleza kuwa Rais wa China Xi Jinping katika mkutano wa Beijing hivi
karibuni aliahidi kuendelea kuziunga mkono nchi za Afrika katika kuendeleza
sekta mbali mbali za maendeleo ambapo hatua hiyo ni miongoni mwa ahadi hiyo.
Akizungumza katika
hafla hiyo ya ufunguzi wa mafunzo hayo Msaidizi wa Rais wa Taasisi ya “Cina
National Research Institute of Food and Fermentation Industries Corporation
Ltd” Bi Luo Yanqin alisema kuwa kutokana na Zanzibar kutegemea zaidi sekta ya
utalii katika uchumi wake, mafunzo hayo yanamsaada mkubwa katika kuimarisha
sekta hiyo hapa nchini.
Kiongozi huyo wa
Taasisi hiyo alieleza kuwa mafunzo hayo sio tu yatasaidia kupata uwelewa juu ya
utoaji wa huduma katika hoteli, ofisi na nyumba za viongozi lakini pia
yatajenga daraja la kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Zanzibar
na China.
Washiriki wa mafunzo
hayo, wametoka Ofisi mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ikiwemo
Ikulu na nyumba za makaazi ya Rais wa Zanzibar za Unguja, Pemba, Dar-es-Salaam
na Dodoma, Ofisi ya Baraza la Mapinduzi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar, nyumba za viongozi wastaafu, walimu kutoka Taasisi ya Utalii ya Chuo
Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), ambayo inatoa mafunzo ya mapishi na
uakarimu, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege pamoja na Hoteli ya Verde.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment