Habari za Punde

CCM Zanzibar Yanena Mazito Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Jangombe Zanzibar.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ kizungumza na Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali vilioko Zanzibar, kuhusiana na kukamilika kwa ratiba za ufunguzi wa kampeni wa Uchaguzi Mdogo Jimbo la Jangombe unaotarajiwa kizinduliwa mwishoni mwa wiki hii.
BAADHI ya Waandishi wa Habari walioshiriki katika Mkutano huo wakifuatilia hotuba ya  Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’.

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar  kimesema tayari kimekamilisha taratibu zote za Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Jang’ombe na kumpata Mgombea Mteule Ramadhan Hamza Chande atakayepeperusha bendera ya CCM kuwania nafasi ya Uwakilishi katika Uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Octoba 27, mwaka 2018.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ huko Afisi Kuu ya CCM  Kisiwandui Zanzibar, amewasihi wanachama wa Chama hicho na wananchi kwa ujumla kutumia vizuri fursa hiyo kwa kumchagua kiongozi mwenye uwezo wa kutatua kwa haraka kero zitakazojitokeza katika jimbo hilo.
Aliwasihi wananchi kutumia vizuri nafasi hiyo kwa kumchagua Mwakilishi bora wa kuwaletea maendeleo katika nyanja zote  bila ubaguzi wa kisiasa , kidini na kikabila.
Alisema wananchi hao wanatakiwa kuwa makini kwa kutopoteza nafasi hiyo ikizingatiwa imebaki muda wa miaka miwili kufika uchaguzi Mkuu, hivyo mwakilishi watakaye mchagua ataweza kuendeleza mageuzi ya kimaendeleo yaliyoachwa na mtangulizi wake katika jimbo hilo.
“ Chagueni kiongozi mwadilifu aliyekuwa karibu ya wananchi kwa kusikiliza na kutatua kwa vitendo chagamoto zitakazojitokeza katika jamii ya Jang’ombe, na atakayekuwa na upeo na fikra za kubuni fursa mbadala za kunufaisha makundi yote ya wananchi wa Jang’ombe.”, alisema Dk. Mabodi
Alisema wananchi na Wana-CCM kwa ujumla wasiangalie sifa za mgombea pekee bali watathimini hata  uwezo, sera, ukomavu na mipango ya maendeleo ya  vyama tisa vilivyosimamisha wagombea na hatimaye kumchagua mgombea mmoja kutoka Chama chenye sifa za ziada.
Aliongeza kwa kufafanua kuwa kupitia Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, Chama Cha Mapinduzi kimetatua kwa kiwango kikubwa kero mbali mbali ndani ya Jimbo la Jang’ombe kwa kuwapekelea wananchi huduma bora za Afya, Maji Safi na Salama, elimu, umeme na kwa sasa kunaendelea ujenzi wa mitaro mikubwa itakayoondosha tatizo la kutwaama kwa maji katika Jimbo hilo.
Pia aliwataka viongozi mbali mbali wa Jimbo hilo wakiwemo masheha, viongozi wa dini, wazee pamoja na  vikundi mbali mbali vya kijamii kuondosha tofauti zao na badala yake kuhubiri mshikamano, Umoja na Utulivu ili Jang’ombe iwe na maendeleo endelevu.
Akizungumzia maandalizi ya Uchaguzi huo Dk. Mabodi alisema CCM imemteuwa mgombea wake Ramadhan Hamza kuwania nafasi hiyo kutokana na aliyekuwa Mwakilishi wa Chama hicho katika Jimbo hilo kutenguliwa baada ya kukabiliwa na makosa ukiukaji wa maadili ya CCM miezi kadhaa iliyopita.
Alieleza kuwa CCM itatarajia kuzindua rasmi kampeni zake za kumnadi mgombea   Octoba 14, mwaka 2018 ambapo mgeni rasmi atakuwa ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Ndugu Philip Mangula na zitafungwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein Octoba 25, mwaka huu.
Alisema  kupitia ufunguzi huo mgombea atakabidhiwa rasmi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ili aweze kuitafsiri kwa vitendo kwa kuendeleza kwa kasi maendeleo ya Jimbo hilo yaliyofanywa na viongozi mbali mbali wa CCM  waliopita.
Alisema mgombea atapata nafasi ya kunadi sera na vipaumbele vyake atakavyotakiwa kuvitekeleza kabla ya mwaka 2020, endapo wananchi wa Jimbo hili wakimuamini na kumpa dhamana ya kuwaongoza kwa kipindi cha miaka miwili.
Dk.Mabodi akizungumzia dhana ya CCM mpya na Tanzania Mpya alisema Chama Cha Mapinduzi kwa sasa kinaendelea na zoezi la uhakiki wa matumizi ya Fedha za Mifuko ya Maendeleo ya  Majimbo kwa Wabunge na Wawakilishi ili kujua fedha hizo zimetumika vipi kwa kuwanufaisha wananchi.
Alisema mbali na uhakiki huo pia Tume inayofanya zoezi hilo inafuatilia utekelezaji wa ahadi za viongozi hao zimetekelezwa kwa kiwango gani pamoja na kuhakiki Serikali imetekeleza kwa kiasi gani Ilani ya Uchaguzi ya CCM sambamba na uhakiki wa mali zote za CCM katika Mikoa yote ya Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu huyo Dk. Mabodi zoezi hilo linafanyika kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kiutendaji ndani ya Chama na Serikali zake ili wananchi na wanachama wa CCM kwa ujumla waendelee kunufaika na rasilimali za nchi yao.
Aliwashauri wananchi wa Jimbo la Jang’ombe kujitokeza kwa wingi katika kushiriki harakati mbali mbali ya Uchaguzi huo kuanzia hatua ya kampeni hadi siku ya Uchaguzi kwa kuepuka vitendo vyote vya uvunjifu wa amani  kwani zoezi hilo lipo kikatiba.
“ Tunajua safari ni ndefu kufikia 2020 lakini kiuhalisi tayari tushavuka malengo ya kutekeleza yake tuliyoahidi wananchi  ambayo yametekelezwa na Serikali ya Awamu ya Saba inayoongozwa na CCM chini ya usimamizi wa Rais wa Zanzibar  na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein.
Wazanzibar ni wastaarabu na wana utamaduni wa kihistoria wa kuvumiliana kisiasa na katika uchaguzi huu mdogo pia naamini zoezi hili litafanyika kwa hali ya amani na utulivu.”, alishauri Naibu Katibu Mkuu huyo.
Alibainisha kwamba hakuna kiongozi, Chama wala kikundi cha Kijamii chenye uwezo wa kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ama chaguzi ndogo ndogo zinazoendelea nchini zisifanyike kwani mazoezi hayo yapo kwa mujibu wa sheria ndani ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Sambamba na hayo aliweka wazi kwamba CCM inaendelea kusimamia ibara ya Tano ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2017 inayoelekeza kwamba kwa kufuata misingi ya kidemokrasia ushindi wa CCM ni lazima katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa Dola.
Akizungumzia zoezi la Usajili wa kuimarisha Taarifa za Vitambulisho linaloendelea katika Wilaya mbali mbali za Zanzibar hivi sasa, Dk. Mabodi amewataka wananchi kuendelea kujitokeza kwani zoezi hilo lina umuhimu mkubwa kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Alisisitiza kuwa zoezi hilo la uimarishaji wa taarifa za Vitambulisho kwa watu wenye sifa lina umuhimu mkubwa hasa katika mipango ya maendeleo ya nchi na taarifa mbali mbali za wananchi katika masuala ya kijamii.
Alisema Zanzibar sio nchi ya kwanza kufanya zoezi hilo bali hata nchi mbali mbali Duniani zimekuwa zikifanya zoezi hilo kwa kuwaweka wananchi wao katika mfumo rasmi wa vitambulisho wanavyovitumia katika shughuli mbali mbali za kijamii na kimaendeleo.
Alisema taarifa hizo zinazowekwa katika vitambulisho zinaisaidia serikali katika masuala ya sensa ya watu na makaazi, takwimu za kitaifa, hati za kusafiria, vizazi na vifo pamoja na masuala mengine yanayohusu ustawi wa Taifa.
Kupitia Mkutano huo amewataka Masheha kuhamasisha zoezi hilo lifanyike kwa ufanisi na wasiwe  vikwazo vya kuwakosesha wananchi haki zao za msingi na Kikatiba.
Pamoja na hayo amevitahadharisha baadhi ya Vyama vya Siasa kuacha tabia ya kuwapotosha wananchi na kuwazuia wasishiriki katika zoezi hilo kwani lipo kisheria na hata Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein amekuwa akisisitiza lifanyike kwa ufanisi.
CAPTION
Picha no. 0198- NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ akizungumza na Waandishi wa Habari Zanzibar juu ya masuala mbali mbali yakiwemo maandalizi ya Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Jang’ombe.
Picha no.0206-BAADHI ya Waandishi wa Habari walioshiriki katika Mkutano huo wakifuatilia hotuba ya  Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.