Habari za Punde

UTORO, NA UDHALILISHAJI UMEPUNGUA SHEHIA YA MZURI

Na.Mwandishi Wetu Kusini Unguja.           
Imeelezwa kwamba tatizo la utoro, udhalilishaji  wanafunzi kijinsia, uchakavu wa jengo la skuli pamoja na ukosefu wa maji safi na salama katika Shehia ya Mzuri wilaya ya Kusini Unguja ni miongoni mwa matatizo ambayo yameshapatiwa ufumbuzi kufuatia wana kijiji hao kupaza sauti zao na kuwataka viongozi wa Halmashauri kuwatatulia matatizo yao yanayowakabili.

Wakizungumza na Zanzibar Leo kwa nyakati tofauti wakazi wa Shehia ya Mzuri wamesema kuja kwa Mradi wa Kukuza Uwajibikaji (PAZA) kumewasaidia kwa kiasi kikubwa kuelezea matatizo yao na kufanyiwa kazi na Serikali.

Akiongea kwa niaba ya wananchi wenzake Bi Zawadi Hamdu Vuai (53) mkaazi wa shehia ya Mzuri amesema utoro na vitendo vya udhalilishaji kwa wanafunzi ambao ulikuwa ukifanyika katika shehia yao hivi sasa umepata afuweni kutokana wananchi kuelimishwa na kwenda kwenye vyombvo vya sheria kufuatilia.

“Vitendo vya udhalilishaji vilikuwa vikitusumbua sana na wananchi wa kijiji hiki walikuwa wagumu ukiwaambia wende kwenye vyombo vya sheria lakini sasa Alhamdulillah wananchi wetu wameelimika na wamepata muamko wa kuripotia matukio kama haya” alisema Mama huyo.

Hata hivyo Bi Zawadi amesema katika shehia yao kulikuwa na tatizo la utoro wa wanafunzi wanaokimbia masomo kutokana na sababu mbali mbali katika eneo hilo jambo ambalo husababisha waaambukiza wanafunzi wenzao wenye ari ya kusoma kupungua kwenda skuli na kudharau masomo yao.

Amesema baada ya mradi wa PAZA kuwahamasisha wananchi njia za kutatua matatizo yanayowakabili katika maeneo wanayoishi, ambapo vijana  wa shehia ya Mzuri, Nganani na Kajengwa wamechukua hatua   kufuata watoto watoro majumbani mwao na kuwapeleka skuli hali iyopelekea kupunguza utoro kwa watoto wao.


“Watoto wetu walikuwa watoro sana lakini tunashukuru tumefanikiwa kuwarejesha skuli na sasa wanaendelea na masomo yao lakini pia tunafuatlia nyendo zao kwa sababu wakiachia tu basi watardia utoro” aliongeza Mama huyo.

Katika hatua nyengine uhaba wa walimu uliokuwa ukiwakabili uongozi wa skuli nao kwa kiasi fulani umepatiwa ufumbuzi pamoja na majengo ya skuli ambao yalikuwa chakavu sasa yametengenezwa jambo ambalo huwapa moyo walimu na wafanyakazi wa skuli hiyo.


Naye Mkaazi wa shehiya ya Mzuri Rashid Haroun Rashid (29) amesema  ukarabati wa vyoo vya skuli ya Kusini ushakamilika ila ujenzi wa skuli ya maandali bado hivyo amewaomba wasimamizi wa Mradi  wa PAZA kuliangalia tatizo hilo kwa makini.

Aidha amesema hana budi kuushukuru Mradi wa PAZA kwa kuwaondolea shida ya maji katika eneo hilo kwani wananchi wameridhika kwa kupata maji safi na salama japokua yanatoka kwa mgao lakini wanaamin mradi ukiendelea maji yatapatikana yakutosha kwa wananchi wa kusini unguja.

Kwa upande wake Afisa Elimu Kusini Unguja,  Haji Mohamed Abdulla (58) akijibu suali la mwandishi aliyetaka kujua mfumo wa ufundishaji wanafunzi amesema wataendelea na Uwajibikaji kwa wanafunzi kwa kutoa huduma bora  na kuhakikisha ufundishaji unafanyika kwa kufuata mtaala.

Aidha amesema ofisini yake itaendelea na utaratibu wa kusimamia majengo ya skuli kuwa safi na mazima pamoja na kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika  mazingira bora na salama.

Mradi wa kukuza Uwajibikaji Zanzibar (PAZA) unatekelezwa na taasisi zisizo za kiserikali  Chama Cha wa Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Kwa upande wa Zanzibar, Waandishi wa Habari za Maendeleo (WAHAMAZA)  kwa upande wa Unguja na Jumuiya ya Uhifadhi wa Msitu wa Ngezi Pemba (NGENARECO) kwa upande wa Pemba na kusimamiwa na Mpango wa kusaidia watendaji wasio na kitaifa (ZANSAP) na kufadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya (EU).

Mradi huo wa mwaka mmoja lengo lake ni kuwasaidia wananchi kupaza sauti zao katika kuelezea shida na matatizo waliyonayo katika vijiji vyao ili yashughulikiwe na wahusika wakiwemo viongozi wa serikali za mitaa na serikali kuu ili kuchochea uwajiikaji na maendeleo kwa wananchi wote.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.