Habari za Punde

Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan Azungumza na Mabalozi wa Nchi za Misri, Ethiopia na Spain. Walioko Nchini Tanzania.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Balozi mpya wa Spain nchini Mhe. Francisca  Pedros (kushoto) aliyefika kujitambulisha ofisini kwa Makamu wa Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Balozi mpya wa Spain nchini Mhe. Francisca Pedros (kushoto) mara baada ya kumaliza mazungumzo ofisini kwa Makamu wa Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam. 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiagana na Balozi mpya wa Spain nchini Mhe. Francisca Pedros (kushoto) mara baada ya kumaliza mazungumzo ofisini kwa Makamu wa Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam.
(Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 31 Januari, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Mabalozi kutoka nchi 3 ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Balozi wa kwanza kukutana na Makamu wa Rais, alikuwa Mhe. Gaber Mohamed Abulwafa Balozi mpya wa Misri hapa nchini ambaye alifika kwa lengo la kujitambulisha na pia kuzungumzia mambo mbali mbali ya kuimarisha uhusiano baina ya nchini  mbili ambao ulianzishwa na waliokuwa marais wa nchi hizi, Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais Gamal Abdel NasserHussein wa Misri.
“Misri itaendelea kutoa ushirikiano katika masuala ya Elimu, Afya na masuala ya teknolojia ya ujenzi wa miundombinu yenye tija kwa mataifa haya mawili” alisema Balozi huyo.
Mwisho Balozi huyo mpya wa Misri aliahidi kusimamia miradi yote ambayo ipo kwenye makubaliano baina ya Serikali hizi.
Kwa upande wake Makamu wa Rais alimpongeza na kumkaribisha Tanzania pamoja na kumhakikishia ushirikiano mzuri katika kazi zake akiwa hapa nchini na kumueleza kuwa kwa miaka mingi uhusiano kati ya Misri na Tanzania umezidi kuimarika.
Balozi wa Pili kukutana na kuzungumza na Makamu wa Rais alikuwa Mhe. Francisca Pedros, Balozi mpya wa Spain hapa nchini ambaye Makamu wa Rais alimpongeza kwa kuwa Balozi wa kwanza mwanamke kuteuliwa kuja kuitumikia nchi yake hapa nchini.
Balozi wa Tatu kukutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Makamu wa Rais ni Balozi wa Ethiopia nchini Mhe. Yonas Yosef Sanbe ambaye alimueleza Makamu wa Rais furaha yake ya kuwa hapa na kuona namna mahusiano ya nchi hizi mbili yameboreka ambapo alisema kuwa
“nafarijika kuona namna ambavyo wanawake wanapewa nafasi za juu katika uongozi katika nchi hizi mbili”
Makamu wa Rais pamoja na mambo mengine alimpongeza Balozi huyo wa Ethiopia kwa kuwa Balozi wa kwanza mwenye makazi yake hapa Tanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.