WAZIRI wa
Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pemba Juma akizungumza na Walimu
Wakuu wa Skuli za Sekondari Kisiwani Pemba katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari
Madungu Chake chake Pemba.
Na. Suleiman Juma
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo
ya Amali Zanzibar, Mh. Riziki Pembe Juma amewataka Walimu Wakuu wa skuli za
sekondari kisiwani Pemba kuendelea kushirikiana zaidi na wazazi katika
kuhakikisha ufaulu mkubwa wa wanafunzi unaongezeka.
Mh. Riziki ameyasema hayo
wakati akizungumza na walimu wakuu wa skuli za Sekondari kisiwani Pemba katika
ukumbi wa skuli ya sekondari Madungu.
Alisema, ufaulu wa wanafunzi
unakwenda sambamba na upatikanaji wa ushirikiano wa dhati kati ya walimu na
wazazi wa wanafunzi.
Mh. Waziri alieleza kuwa,
hivi sasa wazazi wamekua na muitiko mkubwa na wa dhati kuunga mkono jitihada
mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kuboresha sekta ya elimu nchini.
“Tuendelee kuzidisha
mashirikiano baina yetu na wazazi wenzetu katika kulipeleka mbele jahazi la
elimu kwani sote ni wasimamizi na tutakwenda kuulizwa kile ambacho
tunakisimamia”. alieleza.
Hata hivyo aliwapongeza
walimu hao kwa kazi kubwa wanayoifanya
kuhakikisha kiwango cha ufaulu kinaongezeka kwa kasi kubwa kila mwaka nchini
licha ya changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo.
Mapema akimkaribisha mgeni
rasmi katika mkutano huo Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
Zanzibar, Dk. Idrisa Muslim Hija alieleza kuwa, serikali inajivunia mafanikio
makubwa yaliyotokana na jitihada za walimu hao kwani kila mwaka kiwango cha
ufaulu kwa wanafunzi kimekua kikiridhisha.
Akitoa nasaha zake kwa
walimu wakuu hao, Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Nd.
Mohamed Nassor Salim alisema walimu wanalo jukumu kubwa la kuwafundisha
wanafunzi kwa nia thabiti wakizingatia jicho la serikali linawaangalia walimu
katika kuifanya jamii kuwa na maadili na uzalendo wa Taifa lao.
Aidha, aliwataka walimu
kutofanya biashara wakati na muda wa kazi ili waweze kufundisha kwa umakini na
umahiri mkubwa.
Nao, walimu hao walieleza
changamoto zinazowakabili ikiwemo upungufu mkubwa wa walimu wa masomo ya
sayansi katika skuli mbalimbali za sekondari kisiwani humo.
Hata hivyo, Waziri wa Elimu
na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pemba Juma aliwataka walimu wakuu hao
kupeleka taarifa za walimu wa sayansi ambao hawajaajiriwa ili changamoto hiyo
ipate kutatuliwa haraka.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu
na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Dk. Idrisa Muslim Hija akimkaribisha Waziri wa Elimu
na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mh. Riziki Pembe Juma kuzungumza na Walimu Wakuu
wa skuli za sekondari kisiwani
Walimu Wakuu wa skuli za
sekondari kisiwani wakipokea nasaha kutoka kwa WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pemba
Juma katika Ukumbi wa Skuli ya Sekondari Madungu Chake Chake Pemba.
(Picha na Ali Othman - Pemba)
No comments:
Post a Comment