Habari za Punde

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud Awaapisha Makatibu Tawala.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud akimuapisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Mjini Magharibi A Ndg. Said Haji Mrisho, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Vuga Zanzibar. 
MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohamed Mahmoud, akimuapisha Katibu Tawala, Mkoa wa mjini Magharibi, Saleh Mohamed Juma, hafla iliofanyika ofisi za Mkuu wa Mkoa Vuga
Na.Mwinyimvua Nzukwi. 
MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud amewaapisha Makatibu Tawala wa Mkoa wa Mjini Magharibi na wilaya ya Magharibi ‘A’ walioteuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein hivi karibuni na kuwataka kuzingatia sheria katika utendaji wao.
Akizungumza katika hafla hiyo, Ayoub aliwataka Makatibu hao kutambua changamoto zinazowakabili wananchi wa mkoa huo na kutumia hekma katika utatuzi wa kero hizo.
Alisema katika utendaji wa majukumu yao watakutana na aina mbali mbali za watu jambo linalowapasa kuwa na mashirikiano ya pamoja na watendaji wengine wa mkoa huo.
“Kwa mujibu wa sheria nyinyi ndio wasaidizi wakuu wa mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya lakini pia makatibu wa kamati za usalama hivyo mtambue mna wajibu mkubwa lakini aliyewateua ana matarajio kuwa hamtamuangusha”, alisema Ayoub.
Aidha aliwaahidi makatibu hao kuwapatia ushirikiano na kuwataka kuwa viungo kati ya viongozi wa serikali kuu na serikali za mitaa.
Akitoa nasaha katika hafla hiyo Mkuu wa Mkoa Mstaafu wa mkoa huo maalim Abdallah Mwinyi Khamis aliwataka wateule hao kuwa tayari kubadilika kutokana na aina ya majukumu mapya yanayowakabili.
“Sijui mna uzoefu wa mambo gani mliyokuwa mkiyafanya huko mlipotoka lakini katika majukumu yenu mapya mnatakiwa kujifunza namna bora ya kushughulikia watu”, alisema maalim Abdallah.
Naye Meya wa Manispaa ya Zanzibar Khatib Abdulrahman Khatib aliwataka Makatibu Tawala hao kufanya kazi kwa mashirikiano na viongozi wengine ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Nawapongeza kwa kuteuliwa kuwa sehemu ya uongozi wa mkoa wetu hivyo ipo haja ya kuzingatia kutekeleza majukumu yenu kwa pamoja na huo ndio wa kiutendaji ndani ya mkoa huu”, alisema Meya Khatib.
Naye Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Magharibi Kichama Mohammed Rajab Soud aliwataka kuzingatia utendaji kazi za chama na serikali hivyo wanapaswa kuhimiza maendeleo ya wananchi.
“Mnapokuwa katika kazi zenu mtambue kuwa pamoja na nyenzo nyengine mnatakiwa kutumia ilani ya uchaguzi ya CCM kwani huo ndio mwongozo tunaotumia”, alisema Rajab.
Wakitoa shukrani baada ya kula kiapo hicho katibu tawala wa mkoa wa mjini magharibi saleh mohammed juma na katibu tawala wa wilaya ya mjini said haji mrisho waliwataka watendaji wa taasisi zilizomo katika mkoa huo kuwapa ushirikiano ili kutimiza wajibu wao.
“Zaidi ya shukrani tunaomba mtupe mashirikiano toka kwenu ili kufanikisha malengo ya serikali yetu na matarajio ya aliyetuteua kushika wadhfa huu”, alisema Saleh kwa niaba ya Katibu tawala wa wilaya ya Magharibi ‘A’.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.