Habari za Punde

Mwenyekiti UWT Mkoa wa Magharibi Unguja Bi. Zainab Ahimiza Mikutano ya Wadi

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Magharibi Kichama Bi. Zainab Ali Maulid, akizungumza na Wajumbe wa Wadi ya Mwanakwerekwe , wakati wa ziara yake. 
Na. Is-Haka Omar.
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT), Mkoa wa Magharibi Zainab Ali Maulid, amezitaka ngazi za wadi ndani ya mkoa huo kufanya vikao vya kawaida na kikatiba kwa mujibu wa miongozo ya katiba na kanuni za umoja huo.
Wito huo aliutoa wakati akiwahutubia wajumbe wa Baraza la UWT wadi ya Mwanakwerekwe katika mkutano wa baraza hilo, uliofunguliwa kwa niaba ya mikutano yote iliyofanyika ya mabaraza 14 yaliyopo katika wilaya ya Dimani Unguja.
Alisema ufanisi wa kiutendaji ndani ya umoja huo unatokana na utekelezaji wa maelekezo ya vikao halali vinavyotoa maazimio na maelekezo ya utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili wanachama, viongozi na watendaji wa UWT.
Alisema vikao ndio sehemu pekee ya kujitathimini na kupanga mikakati ya utendaji wa shughuli mbali mbali za UWT hasa katika wakati wa sasa wa kuelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Alisema kila mwanamke ndani ya umoja huo anatakiwa kuwahamasisha wanawake wengine hasa waliokuwa hawajajiunga na UWT na CCM kuweza kujiunga ili wanufaike na siasa bora zinazoendeshwa na CCM.
Mwenyekiti huyo aliwakumbusha akina mama hao kwamba wanatakiwa kujipanga vizuri juu ya kuwahamasisha wanawake kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura pindi wakati wa zoezi hilo utakapofika.
Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo Zainab, aliwasisitiza wanawake hao kushiriki katika harakati za kukemea na kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwani vinakwamisha malengo ya vijana hasa wa kike.
Naye Mwenyekiti wa wadi hiyo, Amina Khalfan alisema watayafanyia kazi kwa vitendo maelekezo yote yaliyotolewa na Mwenyekiti huyo kwa lengo la kuimarisha shughuli mbali mbali za Umoja huo katika Wadi hiyo.
Kwa upande wake Mjumbe wa Baraza hilo ambaye pia ni Mwakilishi wa Viti Maalum, Mwanaidi Kassim Mussa aliwashauri viongozi wa wadi hiyo kuendelea kuwa wabunifu na kushirikiana na viongozi wa ngazi za juu za Umoja huo ili wasaidie kutatua kwa haraka changamoto zinazowakabili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.